• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 5:50 AM
Uhuru aibua mbinu mpya kuzima Ruto

Uhuru aibua mbinu mpya kuzima Ruto

ONYANGO K’ONYANGO NA MWANGI MUIRURI

MRENGO wa Rais Uhuru Kenyatta katika Azimio umebuni mikakati mipya ya kujaribu kuzima ushawishi wa Naibu Rais William Ruto katika eneo la Mlima Kenya ili kuimarisha nafasi ya Raila Odinga kushinda urais Agosti 9.

Mipango hiyo inalenga kuhakikisha kuwa Bw Odinga anapata angalau zaidi ya kura milioni 2.5 katika eneo hilo lenye zaidi ya kura 5.5 milioni.

Mbinu hizo ni pamoja na Rais Kenyatta kufanya ziara eneo hilo, kubuniwa kwa kamati za kampeni za azimio kuanzia ngazi ya vituo vya kupiga kura, kushinikiza wagombeaji viti Jubilee wamfanyie kampeni Bw Odinga, kampeni za nyumba kwa nyumba na vikao vya mashauriano vijijini vikuhusisha viongozi wa kidini, wazee na jamii.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Jubilee, Kanini Kega jana aliambia Taifa Leo kwamba watategemea kamati ndogo kusimamia kampeni za Jubilee na kumpigia debe Bw Odinga.

Kaunti 10 za Mlima Kenya zina thuluthi moja ya jumla ya kura za kitaifa. Kaunti hizo ni Kiambu iliyo na kura 1,293,309, Nakuru (1,050,367), Meru (780,858),Tharaka Nithi (234, 618), Embu (337,627), Nyeri (492,046), Kirinyaga (378,580), Murang’a (628,416), Laikipia (265,842) na Nyandarua (362,357).

Bw Kega alisema imewalazimisha kubuni mikakati hiyo mipya kuyeyusha umaaruru wa Dkt Ruto eneo la Mlima Kenya, akieleza kuwa watatumia ‘mbinu za Mau Mau’ za kufikia wapiga kura mashinani badala ya mikutano ya hadhara.

Kulingana na Katibu Mkuu wa Jubilee, Jeremiah Kioni, mbinu nyingine ambayo watatekeleza ni kutembea nyumba moja hadi nyingine kuwashawishi wakazi.

Katika mbinu ya kushawishi wagombeaji wa Jubilee wamfanyie kampeni Bw Odinga, imeibuka kuwa wale ambao wanahofia kufanya hivyo wataadhibiwa kwa kunyimwa pesa za kampeni.

WAGOMBEAJI KUNYIMWA PESA

Pendekezo hilo lilitolewa na vigogo wa Azimio kutoka eneo hilo waliokutana na Bw Odinga mnamo Jumanne katika Hoteli ya Thika Greens.

Pendekezo hilo pia liliungwa mkono na Bw Odinga mwenyewe.Onyo hilo limejiri huku baadhi ya wawaniaji wakionekana kususia kujihusisha na Bw Odinga na badala yake kujinadi kama wagombea wa chama cha Jubilee huku baadhi wakiwaambia wakazi wapigie kura mwaniaji urais wampendaye.

“Wale ambao wamedhihirisha kujitolea kupigania Azimio watapata kiwango kikubwa cha ufadhili kutoka kwangu. Msiwe na shaka kuhusu hilo. Tayari nimeagiza tuwe na kamati zinazosimamia kampeni za wadi, eneobunge na kaunti na kuziunganisha na kitengo kinachosimamia kampeni ya urais kinachoongozwa na aliyekuwa Tuju,” alisema Bw Odinga.

Mrengo wa Jubilee pia unajaribu kushawishi viongozi wa kidini na kijamii kumfanyia kampeni Bw Odinga.

“Tunafanya vikao vya mashauriano na wakazi vijijini tukisaidiwa na viongozi wa kijamii na wazee,” akasema Mwakilishi wa Kike wa Murang’a, Sabina Chege.

VIKAO VIJIJINI

Kulingana na mchanganuzi wa siasa, Javas Bigambo, Bw Odinga anapasa kuacha kumtegemea sana Rais Kenyatta kumfanyia kampeni Mlima Kenya iwapo anataka kuzoa kura.

“Raila anahitajika kutia bidii Mlima Kenya bila kumtegemea Uhuru. Anahitaji kushikana na watu wanaoweza kumsaidia kukubalika eneo hilo,” akasema Bw Bigambo.

Aliongeza kuwa huenda Bw Odinga akajiharibia Agosti 9 iwapo ataweka nguvu zake zote Mlima Kenya na kusahau maeneo ambayo yamekuwa ngome zake za kisiasa.

“Imani ya Raila kuwa anachohitaji pekee ili kushinda urais ni kura za Mlima Kenya huenda ikamharibia kwa vile Mlima Kenya ungali telezi kwake. Achunge asije akasahau ngome zake za kisiasa.”

  • Tags

You can share this post!

Wakulima kulipia zaidi mbolea ya CAN uhaba ukitarajiwa

DCI wachunguza bunduki iliyoua mtoto wa mbunge

T L