• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 3:31 PM
Uhuru anahepa BBI?

Uhuru anahepa BBI?

Na WAANDISHI WETU

KIMYA cha Rais Uhuru Kenyatta kuhusu ripoti ya jopo la maridhiano (BBI) kimeanza kukera baadhi ya viongozi wanaotaka itolewe wazi kwa umma mara moja.

Jopo la BBI lilitangaza kukamilisha ripoti yake mnamo Oktoba 23 lakini tangu wakati huo, hakuna habari zozote zimesikika kutoka Ikulu kuhusu mipango ya kuwezesha wahusika walioiandaa kuiwasilisha kwa Rais.

Duru zimesema kuna uwezekano Rais Kenyatta anasubiri hadi uchaguzi mdogo wa Kibra ukamilike ndipo apokee ripoti hiyo.

Ingawa hilo halingeweza kuthibitishwa, uchaguzi mdogo wa Kibra umezua joto kali la kisiasa lililowateka Kiongozi wa ODM Raila Odinga na Naibu Rais William Ruto wanaopigia debe wagombeaji wa vyama vyao.

Bw Odinga ni mshirika wa Rais katika kufanikisha shughuli za BBI, huku Dkt Ruto akisema hakufai kuwa na mapendekezo ya kuongeza nyadhifa za uongozi serikalini kupitia kwa BBI.

Jana, viongozi kadhaa wa Mlima Kenya walisema kile wanachotaka ni nafasi ya kuichanganua ripoti kwa kina ndipo watoe msimamo wao halisi kuhusu kama wataunga mkono au kuipinga.

“Hatujasema tunapinga marekebisho ya katiba lakini tunachotaka ni kwamba ripoti itolewe wazi ili isomwe kwa kina,” akasema Waziri wa Kilimo, Bw Mwangi Kiunjuri alipokuwa katika eneo la Githiga, Kaunti ya Laikipia ambapo aliandamana na viongozi wengine wa Mlima Kenya.

Wananchi wengi walitarajia ripoti hiyo ingetolewa wiki iliyopita baada ya Rais kurudi nchini kutoka ziara za Japan na Urusi lakini kufikia jana, hapakuwa na dalili yoyote kuhusu suala hilo.

Ijumaa iliyopita, shughuli pekee iliyotangazwa kwa umma ambayo ilifanyika Ikulu ilihusu ufadhili wa mabasi ya shule yaliyotolewa na Rais Kenyatta kwa Shule ya Walemavu wa Macho ya Thika, ile ya Archbishop Eliud Wabukala ACK Malakisi na Shule ya Upili ya Wasichana ya Nyiro.

Wakati huo, Rais alitoa pia ufadhili wa miche 100 ya miti ya kiasili kwa kila shule.

Jana, Rais Kenyatta alihudhuria ibada maalumu ya maombi kwa maafisa wa usalama wa taifa katika Kanisa la Holy Family Basilica jijini Nairobi.

Mbunge Mwakilishi wa Kaunti ya Embu, Bi Jane Wanjuki alisema inahitajika ripoti ya BBI itolewe wazi kwa umma ndipo viongozi watoe msimamo kwa njia inayofaa.

“Tunataka mapendekezo ya BBI yatolewe ili tujue kama tutayaunga mkono au la,” akasema, na kuongeza kwamba hakuna vile wanaweza kusema wanaunga mkono kitu ambacho hawajaona wala kukisoma.

Hata hivyo, wengine walisema inastahili wananchi wawe na subira hadi wakati Rais ataona ni wakati mwafaka kupokea ripoti hiyo kisha baadaye itolewe wazi kwa umma.

“Tunangojea kwa unyenyekevu ripoti hiyo na tunawaomba Wakenya kutoanza kujadili ripoti ambayo hatujaiona,” akasema Seneta wa Pokot Magharibi, Bw Samuel Poghisio ambaye anaunga mkono BBI.

Rais Kenyatta amewahi kusema kwamba ripoti itakapotolewa atazunguka nchini kuivumisha pamoja na Bw Odinga na vigogo wengine wa kisiasa wanaounga mkono handisheki.

Inasubiriwa kuonekana jinsi hali ya kisiasa itakavyokuwa, endapo Dkt Ruto ataamua kuendelea kupinga mapendekezo yatakayopigiwa debe na Rais.

Viongozi wa Mlima Kenya wanahofia huenda kuna pendekezo la kuwapa wabunge jukumu la kuchagua Waziri Mkuu mwenye mamlaka makubwa, ilhali eneo hilo lina maeneobunge machache huku wakilalamika wakazi wao ni wengi mno.

Ripoti za Valentine Obara, George Munene, Steve Njuguna na Oscar Kakai

You can share this post!

Polisi majambazi

Mariga ataka bangi ihalalishwe

adminleo