• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 1:20 PM
Uhuru awashusha hadhi mawaziri Charles Keter na Simon Chelugui

Uhuru awashusha hadhi mawaziri Charles Keter na Simon Chelugui

 

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta Jumatano alifanya mabadiliko madogo katika Baraza lake la Mawaziri yaliyohusisha mawaziri wanne na makatibu kadhaa wa wizara katika kile kimeonekana kama kuwashusha hadhi mawaziri wanaoegemea upande wa Naibu Rais Dkt William Ruto.

Katika mabadiliko hayo Waziri wa Kawi Charles Keter alihamishwa hadi Wizara ya Ugatuzi ambayo ilipokonywa idara mbili muhimu. Hizo ni Idara ya Mipango Maalum na Ustawi wa Maeneo Kame (ASALs) zilizopelekwa katika Wizara ya Utumishi wa Umma na Jinsia chini ya Waziri Prof Margaret Kobia.

Japo Waziri Simon Chelugui alidumishwa katika Wizara ya Leba, Idara ya Maslahi ya Kijamii iliondolewa na kuhamishwa hadi wizara inayosimamiwa na Prof Kobia.

Waziri Dkt Monica Juma alihamishwa hadi Wizara ya Kawi kutoka Wizara ya Ulinzi ambako nafasi yake ilipewa Eugene Wamalwa ambaye awali alisimamia Wizara ya Ugatuzi.

Kimsingi, mawaziri walionekana kushushwa hadhi katika mabadiliko hayo ni Charles Keter na Simon Chelugui.

Kwa upande mwingine Prof Kobia ameongezewa mamlaka zaidi baada ya wizara yake kupanuliwa na kuhamishiwa Idara za Maslahi ya Kijamii, Maeneo Kame na Mipango Maalum.

Vile vile, Rais Kenyatta aliwahamisha makatibu wachache wa Wizara. Meja Jenerali Gordon Kihalangwa alihamishwa kutoka Idara ya Ujenzi hadi Idara ya Kawi.

Naye Joseph Njoroge alihamishwa kutoka Idara ya Kawi hadi Idara ya Uchukuzi huku Solomon Kitungu akipelekwa Idara ya Ujenzi na kutoka Idara ya Uchukuzi.

You can share this post!

Hatimaye Bomet yauza majanichai Iran

Wabunge wakiri IEBC imepungukiwa na fedha za uchaguzi