• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 6:55 AM
Uhuru hana nia njema kisiasa – Linda Katiba

Uhuru hana nia njema kisiasa – Linda Katiba

VALENTINE OBARA na IBRAHIM MUSUNGU

VUGUVUGU linalopinga marekebisho ya katiba, limetaja uhasama ulioibuka kati ya wanachama wa ODM na serikali ya Rais Uhuru Kenyatta kama ishara kuwa Mpango wa Maridhiano (BBI) si tiba kwa changamoto za kisiasa nchini.

Vuguvugu hilo la Linda Katiba linalojumuisha viongozi wa kisiasa na wa mashirika ya kutetea haki za raia, Jumanne lilisisitiza kuwa mapendekezo ya kurekebisha katiba kupitia kwa BBI yatanufaisha viongozi wachache pekee.

Msimamo wa viongozi hao wakiwemo Kiongozi wa Narc-Kenya, Bi Martha Karua, mtaalamu wa masuala ya uchumi, Dkt David Ndii, aliyekuwa Jaji Mkuu Willy Mutunga na wengine, ni tofauti na waasisi wa BBI.

Kwa mujibu wa wanaounga mkono marekebisho ya katiba yanayopigiwa debe na Rais na waziri mkuu wa zamani, Bw Raila Odinga, mapendekezo ya kurekebisha katiba yatatoa nafasi ya kuwepo waziri mkuu na manaibu wake, na pia kumpa mamlaka kiongozi wa upinzani.

“Kadri muda unavyosonga, handisheki imeondokea kuwa mpango wa Uhuru kudhibiti hatima ya kisiasa ya Kenya wala si mpango wa kuleta umoja wa Wakenya,” washirika wa Linda Katiba wakasema kwenye taarifa iliyotolewa Nairobi.

Katika taarifa hiyo iliyotolewa siku ya maadhimisho ya ya miaka mitatu ya handisheki baina ya Rais Kenyatta na Bw Odinga, viongozi wa Linda Katiba walisema malalamishi ya ODM yamebainisha wazi tatizo kuhusu haki za uchaguzi haliwezi kusuluhishwa kupitia kwa maelewano ya wanasiasa wachache.

Baadhi ya viongozi wa ODM wakiwemo Seneta wa Siaya, James Orengo na Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed walidai kuna maafisa serikalini wanaokula njama ya kusambaratisha ODM kabla ya 2022.

Inaaminika malalamishi hayo yalisababishwa na matukio ya uchaguzi mdogo wa Matungu, ambapo wanachama wa ODM wanaamini uchaguzi haukuwa huru.

Awali, Rais pamoja na vigogo wengine wa kisiasa walikuwa wamepanga kufanya mkutano mkubwa kuadhimisha handisheki ambapo wanasiasa wanaounga mkono BBI wangekutana kujadili mikakati ya kupigia debe marekebisho ya katiba.

Hata hivyo, mpango huo ulionekana kuvurugwa na uhasama ulioibuka wikendi. Rais Kenyatta jana Jumanne alikuwa na shughuli nyingi katika Ikulu ya Nairobi.

Alifanya mkutano wa Baraza la Usalama na Amani katika Umoja wa Mataifa kupitia video, kisha akawa na mkutano mwingine na Rais wa Baraza la Ulaya, Bw Charles Michel aliyekuwa amemtembelea.

Ilisemekana kulikuwa na mpango wa Rais kukutana na Bw Odinga ili kutuliza joto lililoibuka kuhusu BBI, lakini mkutano huo haukuwa umefanyika kufikia wakati wa gazeti hili kuchapishwa.

Licha ya matamshi yake ya wikendi, Bw Orengo jana Jumanne alidai kuwa muafaka kati ya Rais na Bw Odinga ni wa kudumu na haujayumbishwa kamwe na chochote.

Kulingana naye, lalama alizoibua zilihusu watumishi wa umma wanaotaka kuhujumu uhuru wa uchaguzi mkuu ifikapo 2022, na hilo halihusiani na masuala ya handisheki.

“Handisheki bado iko thabiti. Uvumi unaonendelea haufai kuaminika na wananchi. Mambo bado ni imara na hatubabaiki,” akasema Bw Orengo.

Alizungumza pembezoni mwa mkutano wa maseneta unaofanywa katika Kaunti ya Mombasa, kujadili matayarisho ya mswada wa BBI. Akiongea wakati wa kufungua rasmi mkutano huo katika hoteli ya Sarova Whitesands, Spika wa Seneti, Bw Kenneth Lusaka alisema mkutano huo utasaidia viongozi kushikamana na kuzingatia kile mambo yatakayofaidi taifa hadi miaka ya usoni.

You can share this post!

Mtaa wa Buxton wasalia mahame

Mashabiki wa Liverpool hawanitaki, wanataka Klopp asalie...