• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Mashabiki wa Liverpool hawanitaki, wanataka Klopp asalie kuwa kocha wao – Steven Gerrard

Mashabiki wa Liverpool hawanitaki, wanataka Klopp asalie kuwa kocha wao – Steven Gerrard

Na MASHIRIKA

KOCHA wa Rangers, Steven Gerrard, amesema ingawa kubwa zaidi katika maazimio yake ni kuwa mkufunzi wa Liverpool siku moja, anatarajia kwamba Jurgen Klopp atasalia ugani Anfield kuendelea kudhibiti mikoba ya miamba hao kwa “miaka mingi zaidi”.

Chini ya Klopp, Liverpool wamepoteza jumla ya mechi sita zilizopita za nyumbani kwa mpigo kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL). Ni matokeo ambayo yanadidimiza matumaini yao ya kumaliza kampeni za msimu huu ndani ya mduara wa nne-bora na hatimaye kufuzu kwa soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) muhula ujao.

Baada ya kupigwa na Fulham 1-0 ugani Anfield wikendi iliyopita, Klopp alikiri kwamba msimu huu wa 2020-21 ndio wa kusikitisha zaidi katika taaluma yake ya ukocha. Ni kauli ambayo ilifasiriwa na mashabiki kuwa ishara za mkufunzi huyo kutaka kuondoka Liverpool huku tetesi zinazomhusisha na uwezekano wa kuyoyomea Real Madrid au Bayern Munich zikishika kasi.

Gerrard ambaye ni kiungo na nahodha wa zamani wa Liverpool, aliongoza waajiri wake Rangers kutia kapuni ufalme wa Ligi Kuu ya Scotland kwa mara ya kwanza baada ya miaka 10. Ni ufanisi ambao tayari umeibua gumzo kuhusu uwezo wake wa kudhibiti mikoba ya Liverpool iwapo Klopp atahiari kuondoka ugani Anfield.

“Mashabiki wa Liverpool hawanitaki kuwa kocha wao kwa sasa. Wanataka Klopp aendeleze kazi nzuri ambayo amekuwa akifanya ugani Anfield. Mimi nawaunga mkono mashabiki hao asilimia mila fil mia,” akasema Gerrard wakati akihojiwa na ITV.

“Sidhani tunapaswa kuwa na gumzo la aina hii kwa wakati huu. Klopp ni miongoni mwa wakufunzi bora zaidi duniani kwa sasa na anawaniwa na timu maarufu ulimwenguni. Namstahi sana na natarajia aendelee kuwa kocha wa Liverpool kabla nihitimu kuwa mrithi wake,” akaongeza Gerrard, 40.

Klopp ambaye pia amewahi kunoa Mainz na Borussia Dortmund, tayari amesema atakataa ofa ya kuwa kocha mpya wa Ujerumani na azma yake ni kusalia kambini mwa Liverpool hadi mkataba wake wa sasa utakapotamatika rasmi mnamo 2024. Timu ya taifa ya Ujerumani itasalia bila kocha mwishoni mwa Julai 2021 wakati ambapo mkufunzi wa sasa Joachim Loew anatarajiwa kuondoka baada ya kukamilika kwa fainali za Euro 2021.

Gerrard aliyechezea Liverpool jumla ya mechi 710, aliwahi kuwa kocha wa chipukizi wa kikosi hicho kabla ya kupokezwa mikoba ya ukufunzi kambini mwa Rangers mnamo 2018.

Liverpool walinyanyua taji la EPL msimu uliopita wa 2019-20 wakijivunia pengo la alama 18 kati yao na Man-City walioambulia nafasi ya pili. Hadi Liverpool walipopigwa na Burnley mnamo Januari 2021, miamba hao wa soka ya Uingereza hawakuwa wamepoteza mechi yoyote ya nyumbani kutokana na mapambano 68 ya EPL.

Kwa sasa wanashikilia nafasi ya nane kwa alama 43 huku pengo la pointi 22 likitamalaki kati yao na viongozi wa jedwali la EPL, Man-City. Liverpool wamepoteza jumla ya mechi sita mfululizo katika EPL kwa mara ya kwanza tangu 1953-54.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Uhuru hana nia njema kisiasa – Linda Katiba

Dortmund wadengua Sevilla na kutinga robo-fainali za UEFA...