• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
Ushawishi wa Kalonzo Pwani wafifia 2022 ikinukia

Ushawishi wa Kalonzo Pwani wafifia 2022 ikinukia

Na LUCY MKANYIKA

USHAWISHI wa kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka katika eneo la Pwani unaendelea kudidimia huku wanachama wake wakigura chama hicho uchaguzi mkuu unapokaribia.

Baadhi ya wanasiasa hao sasa wanajihusisha na chama cha ODM kinachoongozwa na Raila Odinga na United Democratic Alliance (UDA) chake William Ruto.

Kuondoka kwa aliyekuwa Seneta wa Mombasa Hassan Omar, ambaye alikuwa nguzo kuu katika Wiper Pwani, kulififisha chama hicho kilichopata umaarufu eneo hilo chini ya mwavuli wa uliokuwa muungano wa Nasa.

Kwa upande mwingine Mbunge wa Kisauni Ali Mbogo yuko katika kambi ya Dkt Ruto licha ya kuwa mwanachama wa Wiper.

Katika Kaunti ya Taita Taveta, Gavana Granton Samboja ambaye alichaguliwa kwa tiketi ya chama cha Wiper, amebadili msimamo na sasa anajiunga na kambi ya Bw Odinga.

Amekuwa akiungana na Bw Odinga katika mikutano yake ya hadhara eneo la Pwani na amemwalika kiongozi huyo wa ODM kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo katika Kaunti hiyo.

Kiongozi huyo wa ODM amevuna umaarufu mkubwa Pwani tangu uchaguzi mkuu wa 2007.

Gavana Samboja anashirikiana na Gavana wa Mombasa Hassan Joho kumfanyia kampeni Bw Odinga kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Ingawa gavana huyo wa Taita Taveta amekana kugura chama cha Wiper, uamuzi wake kuunga mkono azma ya Bw Odinga kuingia Ikulu, umeibua tetesi kuwa anapanga kujiunga na ODM.Kwenye mahojiano wiki jana, Bw Samboja alishikilia kuwa angali mwanachama wa Wiper.

“Hata kiongozi wangu wa chama anafanya kazi na Bw Odinga. Yeye ni kiongozi wa hadhi ya kitaifa na amekuwa akishirikiana na kila mtu,” akasema.

Bw Samboja alisema anaunga mkono azma ya Bw Odinga kuingia Ikulu kutokana na kujitolea kwake kupigania kurejelewa kwa demokrasia katika taifa.

“Kiongozi wa chama changu anafaa kusubiri hadi 2027. Tumpe Bw Odinga nafasi alete mabadiliko nchini. Ndiye kiongozi wa kipekee ambaye yuko tayari kushirikisha eneo hili la Pwani katika serikali yake,” akasema.

Bw Samboja alisema Wapwani hawataendelea kuwa wapiga kura tu, bali watashirikiana na viongozi wengine kuunda serikali ijayo.Bw Musyoka alikuwa mgombea mwenza wa Bw Odinga katika chaguzi za 2013 na 2017.

Hata hivyo, ameapa kutomuunga mkono tena akisema kuwa sharti awanie urais.Wanasiasa waliosalia katika Wiper wakati huu ni pamoja na aliyekuwa Waziri na Mbunge wa Matuga Chirau Ali Mwakwere (Kwale), wabunge; Ali Wario (Garsen) na Danson Mwashako (Wundanyi).

Ingawa Bw Musyoka bado anashabikiwa kwa wingi katika kaunti za eneo la Ukambani, amekuwa akikabiliwa na upinzani kutoka kwa magavana wa kaunti hizo kama Alfred Mutua (Machakos), Kivutha Kibwana (Makueni) na Charity Ngilu (Kitui).

Miezi michache iliyopita Profesa Kibwana aligura Wiper na kujiunga tena na chama Muungano ambacho anataka kukitumia kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Mwaka jana, Johnstone Muthama na aliyekuwa Naibu Gavana wa Nairobi Jonathan Mueke waligura Wiper na kujiunga na chama cha UDA.

You can share this post!

Kaunti lawamani kuhusu ubomoaji

Ruto kutua Kisii kuzima ushawishi wa Matiang’i