• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 6:55 AM
Wagombea urais 55 wahatarisha uchaguzi

Wagombea urais 55 wahatarisha uchaguzi

NA LEONARD ONYANGO

USIMAMIZI wa Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, hasa kiti cha urais unatarajiwa kukumbwa na changamoto tele iwapo watu wote 55 waliotuma maombi ya kuwania urais wataidhinishwa kushiriki.

Hofu kuu ni kuwa idadi hiyo kubwa ya wawaniaji inaongeza uwezekano wa uchaguzi kuahirishwa, endapo yeyote kati ya wagombeaji hao ama mgombea mwenza atafariki baada ya kuidhinishwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Kifungu cha 138 (8) (b) cha Katiba kinasema: “Uchaguzi utaahirishwa iwapo mwaniaji au mgombea mwenza atafariki kabla ya siku ya uchaguzi.”

Katiba inasema hali kama hiyo ikitokea na uchaguzi kuahirishwa, mwingine mpya utaandaliwa ndani ya siku 60 kutoka siku ambayo uchaguzi wa kwanza ulipaswa kufanyika.

Hivyo, hali kama hiyo ikitokea, uchaguzi mwingine utafanyika kufikia Oktoba 7.

Kulingana na mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati, watu 40 wametuma maombi ya kuwania urais kupitia tiketi ya kujitegemea, nao 14 watatumia vyama na mmoja muungano wa kisiasa.

MATOKEO KUCHELEWA

Wawaniaji wakuu ni Naibu wa Rais William Ruto ambaye atawania urais kwa chama cha United Democratic Alliance (UDA) na kinara wa ODM Raila Odinga atakayetumia tiketi ya muungano wa Azimio la Umoja One Kenya.

Wataalamu wanasema idadi hiyo kubwa ya wagombeaji pia ina uwezo wa kufanya shughuli ya kupiga kura kwenda polepole pamoja na kuharibika kwa kiasi kikubwa cha kura zitakazopigwa.

“Ikiwa wote 55 wataidhinishwa kuwania urais, IEBC italazimika kuchapisha karatasi ndefu au hata kijitabu cha kura. Hii ina maana wapiga kura watachukua muda mrefu kutafuta jina la mwaniaji wanayemtaka.

“Matokeo yake ni kuwa shughuli ya kupiga kura itaenda kwa mwendo wa polepole kuliko kawaida na hivyo vituo vya kupigia kura huenda vitakuwa na foleni ndefu sana watu wakingojea kupiga kura,” anasema mtaalamu wa uchumi na mdadisi wa masuala ya kisiasa, George Mboya.

Pia huenda vituo vya kupigia kura vikachelewa kufungwa ama idadi kubwa ya wapiga kura wafungiwe nje muda ukiisha.

Kutangazwa kwa matokeo ya kiti cha urais nayo yanatarajiwa kuchukua siku kadha ikizingatiwa maafisa wa IEBC wanahitajika kusoma matokeo ya kila mwaniaji wa urais katika vituo vyote 52,481, shughuli ambayo itachukua muda mwingi kuliko kawaida kutokana na idadi kubwa ya wagombeaji.

Katika chaguzi za awali, kuchelewa kutangazwa kwa matokeo ya urais kumekuwa moja ya chimbuko la taharuki na madai ya wizi wa kura.

Mara baada ya watu wanaomezea mate urais kuidhinishwa rasmi kuwa wagombea watakuwa kwenye darubini ya IEBC kuhakikisha hawavunji kanuni na sheria za uchaguzi.

RASLIMALI ZAIDI

Hiyo inamaanisha tume hiyo italazimika kuajiri maafisa zaidi kufuatilia mienendo ya wawaniaji wote wa urais.

Serikali nayo italazimika kutumia raslimali zaidi kuwapa ulinzi wawaniaji hao wa urais na wenza wao, lakini watahitajika kutuma maombi.

Utafiti wa kura ya maoni uliofadhiliwa na kampuni ya Nation Media Group wiki iliyopia unaonyesha kuwa Dkt Ruto na Bw Odinga wako nguvu sawa kwa asilimia 42 kila mmoja.

Hiyo inamaanisha kuwa uwezekano wa wengine 53 kushinda ni finyu mno.

Bw Nixon Kukubo na Nazlin Omar ambao walipata kura kura 5,929 na 8,624 mtawalia katika uchaguzi wa 2077 ni miongoni mwa wawaniaji 40 waliotuma maombi ya kugombea kwa tiketi ya kujitegemea.

KUJITAFUTIA SIFA

Bw Kukubo anasema kinachomsukuma kuwania urais ni hamu ya kutaka kupambana na ufisadi.

Muimbaji wa Injili Reuben Kigame, ambaye pia anagombea urais kwa tiketi ya kujitegemea, anasema analenga kuangamiza umaskini.

Prof George Wajackoyah wa chama cha Roots ameshikilia kuwa lengo lake kuu la kuwania urais ni hamu ya kutaka kuhalalisha bangi nchini.

Lakini wataalamu wa masuala ya saikolojia wanasema wengi wa wawaniaji wa urais wamejitosa katika kinyang’anyiro hicho kwa lengo la kujitafutia sifa na wala sio kushinda uchaguzi.

“Wengi wanawania kujitafutia umaarufu na sifa kwamba wamewahi kugombea urais. Mtu anaposikia jina lake likitajwa kila wakati siku ya kutangaza matokeo anajihisi vyema,” anasema Bi Nancy Karwitha, mtaalamu wa saikolojia.

Idadi hiyo kubwa ya wawaniaji hasa wa kujitegemea pia imezua minong’ono kutoka kwa baadhi ya wanasiasa wakidai wamefadhiliwa na wapinzani wao kama njama ya wizi wa kura.

  • Tags

You can share this post!

KPA: Mbinu mpya ya ajira yapingwa kortini

Serikali ya Kenya yakosolewa kwa kupuuza sekta ya ufugaji

T L