• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 5:50 AM
Wanasiasa sasa watumia mzozo wa mipaka kusaka kura

Wanasiasa sasa watumia mzozo wa mipaka kusaka kura

Na LUCY MKANYIKA

HUKU wanasiasa wakijiandaa kwa uchaguzi mkuu wa Agosti, suala la mzozo wa mipaka baina ya Taita Taveta na majirani zake limekuwa moja ya ajenda za viongozi hao, licha ya kuwa halijapata suluhu kwa miaka mingi.

Kaunti hiyo imekuwa ikizozania maeneo ya Makina (Kwale) Mtito Andei (Makueni) na Rombo (Kajiado) na licha ya ahadi za wanasiasa, mizozo hiyo bado haijasuluhishwa.

Baadhi ya wenyeji wa maeneo hayo walidai kuwa mzozo huo umesababisha wakazi hao kutengwa huku serikali hizo zikikunja mikono kutoa huduma kwao.

Mnamo Machi, mahakama ya Mombasa iliamuru kaunti ya Taita Taveta kuchukua ushuru katika maeneo ya Mtito Andei na Makina kwa niaba ya Makueni na Kwale mtawalia.

Vile vile, mahakama hiyo iliamuru Tume ya Ardhi kutatua swala hilo ambalo limekuwa tatizo kwa miaka mingi.

Wiki jana, Gavana Granton Samboja alizuru mji wa Mtito Andei na kuamuru waziri wake wa Fedha, Bw Andrew Kubo, kuchukua ushuru kutoka kwa wafanyibiashara wa eneo hilo.“Ninashukuru korti kwa kuamuru kuwa tuchukue ushuru katika maeneo haya.

Ninachoomba ni kuwa wananchi wadumishe amani wakati swala hili linatatuliwa,” akasema. Wanasiasa wanaopigania viti mbalimbali, wamesema kuwa watalipa suala hilo kipaumbele.

Wawaniaji wa useneta Bw Godwin Kilele, Bw Mwandawiro Mghanga na Bi Anna Kina, walisema kuwa watahakikisha kuwa maeneo hayo yanabaki katika kaunti hiyo. “Nitahakikisha kuwa tunamaliza vita hivi vya mipaka ili tuchukue ushuru katika maeneo hayo,” akasema.

Hata hivyo, mwanakamati wa kamati ya kutatua mzozo huo wa mpaka katika eneo la Makina, Bw Sammy Malalo, alipinga uamuzi wa korti wa kuitaka kaunti ya Taita Taveta kuchukua ushuru katika eneo hilo.

‘Mahakama ingeamuru kuwa suala la ushuru lisisimamiwe na kaunti yoyote hadi pale mzozo huu utakapomalizika,’ akasema.

Miaka miwili iliyopita Gavana Samboja alitia saini mkataba na mwenzake wa Kajiado Bw Joseph Ole Lenku, ili kumaliza mzozo wa Rombo.

Hata hivyo, baadhi ya wenyeji wa eneo hilo walielekea mahakamani ili kupinga mkataba huo kwa madai kuwa alipeana kipande cha ardhi kwa kaunti ya Kajiado.

  • Tags

You can share this post!

Kilio uhaba wa mafuta ukiendelea

Mwashetani aahidi kukuza vipaji vya vijana wasanii

T L