• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Wanasiasa waanza harakati za kusaka mrithi wa Maraga

Wanasiasa waanza harakati za kusaka mrithi wa Maraga

Na BENSON MATHEKA

KAMPENI kali inaendelea chini kwa chini kumtafuta mrithi wa Jaji Mkuu David Maraga anayetarajiwa kustaafu mapema mwaka ujao huku wanasiasa wakitaka wadhifa huo ushikiliwe na mtu wanayeweza kushawishi kwa urahisi.

Wadadisi wanasema kuna wakuu serikalini ambao tayari wameanza juhudi za kuthibiti Tume ya Huduma ya Mahakama (JSC) ambayo kwa wakati huu ina jukumu la kikatiba la kumtafuta Jaji Mkuu na kuajiri majaji.

“Kuna juhudi za kuthibiti JSC. Tayari imewekwa chini ya ofisi ya Mwanasheria Mkuu ilhali kikatiba usimamizi wa mahakama, kama mhimili wa tatu wa serikali, inapaswa kuwa huru. Ni sawa na kumweka Jaji Mkuu chini ya Mwanasheria Mkuu kwa sababu, ndiye mwenyekiti wa JSC. Lengo hapa ni kuhakikisha serikali inathibiti shughuli zote za JSC hasa wakati huu wa kutafuta mrithi wa Bw Maraga,” asema wakili James Wakahiu.

Bw Maraga na Chama cha Wanasheria (LSK) wameshutumu hatua ya Rais Uhuru Kenyatta ya kuweka JSC chini ya ofisi ya Mwanasheria Mkuu, wakisema ni kinyume cha katiba.

Kulingana na wadadisi, wanasiasa wenye ushawishi hawataki Jaji Mkuu mwenye misimamo dhabiti.

“Ni wazi kuwa wanasiasa hawataki Jaji Mkuu anayeweza kubatilisha matokeo ya kura ya urais alivyofanya Maraga kwenye uchaguzi mkuu wa 2017. Kwa ufupi, wanasiasa hawataki mahakama huru na kwa kumtafuta mrithi wa Maraga, macho yote yamo kwenye uchaguzi mkuu wa 2022,” asema Bw Wakahiu.

Akiwa Jaji Mkuu, rais wa mahakama ya juu na mwenyekiti wa JSC, Jaji Mkuu ana ushawishi mkubwa katika maamuzi ya nchi na wanasiasa hawataki mtu huru. Wao hutaka anayetekeleza ajenda zao ilivyokuwa kwenye katiba ya zamani, ambapo ni rais alikuwa akimteua Jaji Mkuu.

Wadadisi wanasema kwamba uchaguzi mkuu ujao unatarajiwa kuwa na ushindani mkali, na kesi yoyote ya kuupinga inaweza kuwasilishwa katika Mahakama ya Juu ambapo Jaji Mkuu atatekeleza wajibu mkubwa.

Duru zinasema kuwa wanasiasa wenye ushawishi hawataki Jaji Mkuu kuteuliwa miongoni mwa majaji wa sasa. Hisia zao ni kuwa majaji wa sasa wako na misimamo mikali kwa sababu hawako moja kwa moja chini ya serikali kuu. Mamlakani ya kuteua majaji ni ya JSC na kazi ya Rais ni kuwaapisha tu.

Kulingana na wakili Ken Obuya, kuna uwezekano JSC itasukumwa kumteua Jaji Mkuu anayeegemea serikali kuu.

MSIMAMO WA KADRI

“Kuna shinikizo na vitisho vinavyoweza kutokea ili makamishna wa JSC wamteue Jaji Mkuu mwenye misimamo wa kadiri au chaguo la walio mamlakani. Anaweza kuwa jaji anayehudumu ama mtu kutoka nje anayetimiza vigezo vya kikatiba,” asema.

Dkt Willy Mutunga, mtangulizi wa Bw Maraga hakuwa jaji alipoteuliwa Jaji Mkuu wa kwanza chini ya katiba ya 2010. Pia mrithi wake Prof Githu Muigai hakuwa jaji. Wote hao walikuwa wahadhiri wa sheria.

Bw Obuya anasema kwamba misimamo ya Jaji Mkuu inajenga au kuvuruga malengo ya wanasiasa na ndio sababu wanafuatilia kwa makini kushawishi urithi wa Maraga.

Uteuzi wa Maraga mwaka wa 2016 ulitanguliwa na kampeni kali ambapo chama cha Jubilee kilishinikiza mabadiliko katika sheria ya JSC, ili Rais akabidhiwe majina matatu ya watu walioongoza mahojiano ateue mmoja. Duru zinasema kwamba mawakili wenye ushawishi, majaji na wanasiasa wamekuwa wakikutana kupanga mrithi wa Maraga.

Jaji Maraga mwenyewe anaweza kuamua kustaafu mapema ili kupatia JSC nafasi ya kutafuta mrithi wake, lakini wadadisi wanasema hatua hii inaweza kusababisha kizungumkuti kwa kuwa Naibu Wake Philomena Mwilu tayari amepakwa tope kwa madai ya ufisadi.

Akiamua kustaafu mapema, ni Bi Mwilu anayefaa kushikilia hadi mrithi ateuliwe.

Baadhi ya mawakili wanahisi kuwa madai ya ufisadi dhidi ya Bi Mwilu yalikuwa sehemu ya kumuondoa katika urithi wa Maraga.

Uteuzi wa Jaji Mkuu ni zoezi linalochukua zaidi ya miezi mitatu, na kuna wanaotaka Maraga astaafu mapema ili kutoa nafasi ya mrithi wake kutafutwa na kumpa muda ajiandae kwa uchaguzi mkuu wa 2022. Mtangulizi wake Mutunga aliondoka mwaka mmoja mapema.

You can share this post!

FUNGUKA: ‘Si uchawi, ni mapenzi’

Mikakati anayohitaji Mudavadi kukabili papa na nyangumi...

adminleo