• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 7:50 AM
Wawaniaji walia hakuna demokrasia kwa mchujo

Wawaniaji walia hakuna demokrasia kwa mchujo

NA WANDISHI WETU

SHUGHULI ya mchujo katika vyama vikubwa vya kisiasa imekumbwa na utata huku baadhi ya wawaniaji wakilia kuchezewa mchezo mchafu.

Baadhi ya wawaniaji sasa wanataka kurejeshewa fedha zao walizolipa kusaka tikiti hizo. Wengine wanalia kuachwa nje katika mazungumzo kabla ya wapinzani wao kukabidhiwa tikiti ya moja kwa moja.

Jana, Bw Zachariah Baraza aliyekuwa akimezea kiti cha ugavana wa Bungoma kupitia tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA), alidai kurejeshewa Sh500,000 alizokuwa amelipa kabla ya tiketi ya muungano wa Kenya Kwanza kukabidhiwa kwa Spika wa Seneti, Ken Lusaka.

Chama cha UDA kimetangaza kuunga mkono Bw Lusaka ambaye analenga kumng’oa Gavana Wycliffe Wangamati anayewania wadhifa huo kupitia chama cha Democratic Action Party – Kenya (DAP-K).

“Nimempa kiongozi wa UDA Naibu wa Rais William Ruto makataa ya siku saba kunirejeshea hela zangu. La sivyo nitaelekea kortini,” akasema Bw Baraza ambaye ametangaza kuwa atawania ugavana kama mgombea wa kujitegemea.

Katika Kaunti ya Nakuru, wawaniaji wanaomezea mate viti kupitia tiketi ya chama cha UDA, jana walidai kura za mchujo zinazofanyika leo, huenda zikakumbwa na udanganyifu.

Wawaniaji wa viti mbalimbali katika eneobunge la Kuresoi Kaskazini jana waliandamana pamoja na wafuasi wao wakidai kulikuwa na njama ya udanganyifu katika kura za mchujo za leo.

“”Tunataka kuhakikishiwa kuwa maafisa wanaosimamia uchaguzi huo ni watu wa kuaminika.

Bw Leonard Borr, mwaniaji wa ubunge wa Kuresoi Kaskazini, alidai kuwa kulikuwa na njama ya kuiba kura.

“Wasimamizi wa kura za mchujo wamekuwa wakimpigia debe mpinzani wangu. Sitaruhusu kusimamia kura za mchujo,” akasema Bw Borr.

Aliyekuwa mtangazaji wa kituo cha redio cha Kameme Njogu wa Njoroge anayemezea mate ubunge wa Njoro, jana alidai hajui maafisa ambao wameteuliwa kusimamia kura za mchujo katika eneobunge lake.

“Tuliambiwa kuwa kura za mchujo za UDA zingekuwa huru na wa haki. Sisi tuliamini mambo yamebadilika. Tuliamini yule atashinda atashinda kwa haki na wala sio kupitia wizi.

“Lakini kufikia sasa, hatujui ni akina nani wanasimamia uchaguzi,” akalalama Bw Njoroge aliyekuwa ameandamana na wawaniaji wenzake wa ubunge Njoro wanaodai kuchezewa shere.

Jana, mitandao ya kijamii ilisheheni picha za vyeti vya UDA vya uteuzi – hali ambayo ilizua tumbojoto miongoni mwa baadhi ya wawaniaji kuwa wanapoteza wakati kwa kuwa maamuzi tayari yamefanywa na vigogo wa chama.

Wawaniaji tele wa ODM kutoka Kaunti ya Homa Bay jana walipigwa na butwaa baada ya kubaini kuwa, chama hicho hakitafanya kura ya mchujo katika baadhi ya maeneobunge leo.

Kulingana na ratiba iliyotolewa na Bodi ya Uchaguzi (NEB) ya ODM, kura za mchujo zitafanyika kusaka mwaniaji wa Mwakilishi wa Wanawake, wabunge wa Ndhiwa na Karachuonyo na madiwani wa wadi zote.

Hiyo inamaanisha kuwa kura za mchujo hazitafanyika katika maeneobunge ya Homa Bay Mjini, Kabondo Kasipul, Kasipul, Suba Kusini , Rangwe na Suba Kaskazini japo waliopewa tiketi hawajatangazwa.

Aliyekuwa Gavana wa Nairobi Evans Kidero – ambaye amegura ODM na kutangaza kuwania ugavana kama mgombea wa kujitegemea – alishutumu ODM kwa kumchezea shere baada ya vigogo wa chama hicho kualika wapinzani wake jijini Nairobi kukubaliana bila yeye kufahamishwa licha ya kulipa ada ya Sh500,000.

Katika Kaunti ya Siaya, viti vya ugavana na useneta havitapigiwa kura, kwa mujibu wa NEB ya ODM.

Hiyo inamaanisha kuwa Seneta wa Siaya James Orengo na Bw Oburu Oginga watapewa tiketi ya moja kwa moja huku wapinzani wao wakiachwa kwenye mataa.

Chama cha Wiper pia kimeshutumiwa kwa kumchezea mchezo mchafu Mbunge wa Kisauni, Ali Mbogo aliyepewa tikiti lakini baadaye gavana wa zamani wa Nairobi Mike Sonko pia akakabidhiwa tikiti sawa. Bw Mbogo sasa anashinikizwa kuwa mwaniaji mwenza wa Bw Sonko.

BRIAN OJAMAA, LEONARD ONYANGO, ERIC MATARA

  • Tags

You can share this post!

Mahakama ya Rufaa sasa yairuhusu IEBC kutoa zabuni ya...

Azimio waweka mikakati ya kumvumisha Raila magharibi

T L