• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
Wengine wengi kupata tiketi za bwerere ODM

Wengine wengi kupata tiketi za bwerere ODM

Na WINNIE ATIENO

CHAMA cha ODM kimedokeza kuwa, idadi ya wanasiasa watakaopewa tikiti moja kwa moja kuwania viti katika uchaguzi ujao itaongezeka katika siku zijazo.

Mwenyekiti wa ODM tawi la Mombasa, Bw Mohammed Khamis, alipuuzilia mbali wanaokashifu hatua ya chama hicho akisema inatambuliwa katika sheria za chama kwa hivyo wanachama walifaa kutarajia hayo tangu mapema.

Katika ukanda wa Pwani, baadhi ya wanasiasa wanaotarajiwa kupewa tikiti bila kupitia kura ya mchujo ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa Kilimo Prof Hamadi Boga kugombea ugavana wa Kwale, mbunge wa Likoni, Bi Mishi Mboko na mwenzake wa Jomvu, Bw Badi Twalib.

“Sheria inakubali ODM itoe tikiti moja kwa moja hasa kwa wagombea ambao hawana upinzani na wale ambao imethibitishwa kupitia kwa utafiti wa kisayansi kwamba wana nafasi bora ya kushinda uchaguzini. Wanachama wanaotaka tikiti walielezwa haya katika mkutano wa kitaifa wa wajumbe,” akasema Bw Khamis, katika mahojiano na Taifa Leo.

Sheria za ODM huruhusu bodi ya uchaguzi kuzingatia makubaliano kati ya wagombeaji, matokeo ya kura ya maoni kutafuta aliye maarufu zaidi, tikiti ya moja kwa moja kwa wale ambao hawana wapinzani, na kura ya mchujo huwa ni ya mwisho iwapo hatua nyingine zitagonga mwamba.

Hata hivyo, Bw Khamis alisema hana habari kuhusu wagombea waliopewa tikiti ya moja kwa moja kwa sasa kwani shughuli hiyo, kulingana naye, inafanywa katika afisi ya kitaifa ya chama.“Uamuzi unatoka makao makuu huko Nairobi.

Isitoshe, vyama vingine kama vile UDA, Jubilee vimeamua kuwapa baadhi ya wagombea tikiti moja kwa moja.

Mbona ikifikia ODM ndio kunaibuka maswali?’ akauliza.Kulingana naye, chama kitazingatia pia uaminifu wa mwanasiasa kabla apewe tikiti.

‘Huwezi kuwa umekaa katika chama kwa miaka 20 na mtu ameingia juzi halafu huyu mgeni ndiye anapewa tikiti. Tunazingatia pia uaminifu wa mgombeaji,” akasema.

Hata hivyo, katika Kaunti ya Kilifi, mwenyekiti wa chama tawi hilo, Bw Teddy Mwambire, amewahakikishia wagombea kwamba hakuna aliyepewa tikiti.Kumekuwa na baadhi ya wanasiasa ambao huzunguka kudai kuwa tayari washapewa tikiti za kuwania viti kupitia kwa ODM.

“Hakuna mtu yeyote aliyepewa tikiti ya chama cha ODM Kilifi. Wale wanaotanganza kwamba wamepewa tikiti ni waongo. Wanajaribu kueneza uvumi ili wagombea wetu waingie woga na kukihama chama chetu. Lakini uzuri ni kuwa kila mwaniaji wetu yuko chamani,” akasema mbunge huyo wa Ganze.

Huko Kwale, uamuzi wa maafisa wa ODM kutangaza kuwa Prof Boga atapewa tikiti umezua joto la kisiasa huku baadhi ya wafuasi wa chama wakiapa kukihama wakidai hakuna usawa.Wiki iliyopita ODM ilisema itaandaa kura ya mchujo katika kaunti zote isipokuwa 26 mwezi ujao.

Maeneo ambapo hakuna kura ya mchujo ni Mlima Kenya, Kaskazini Mashariki na Bonde la Ufa. Ratiba ya ODM iliyochapishwa wiki iliyopita inaonyesha kuwa mchujo utafanyika kaunti ya Kilifi Aprili 4.Katika Kaunti ya Kilifi tikiti ya ugavana ODM inawaniwa na aliyekuwa waziri msaidizi Gideon Mungaro, naibu Gavana Gideon Saburi na Spika wa Bunge la Kaunti ya Kilifi Jimmy Kahindi.

Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, anatarajiwa kuwania kiti hicho kupitia UDA.Mombasa, wanaotaka tikiti ya ODM kuwania ugavana ni mfanyabiashara Suleiman Shahbal, naibu gavana William Kingi na Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir.

Kura ya mchujo itakuwa Aprili 6, iwapo hakutakuwa na makubaliano kati yao kufikia wakati huo.Hata hivyo, Dkt Kingi ameonyesha dalili za kuchukua mkondo tofauti wa kisiasa baada ya kushirikiana na Mbunge wa Kisauni, Bw Ali Mbogo, ambaye anataka kuwania ugavana kupitia kwa Wiper huku pia akimpigia debe Bw Said Twaha kuwa mbunge Mvita.

Bw Twaha anawania kiti hicho kupitia Chama cha Pamoja African Alliance (PAA) kinachoongozwa na Gavana wa Kilifi, Bw Amason Kingi. Dkt Kingi amekuwa naibu wa gavana Hassan Joho tangu 2017.

  • Tags

You can share this post!

#KCPE2021: Watahiniwa 11,523 walihepa mtihani

Himizo wananchi wachukue bima ya afya kupunguza gharama ya...

T L