Mreno aliyetuma droni kwa makazi ya Ruto ashtakiwa

Na MWANGI MUIRURI

Mtalii aliyekamatwa Machi 29 kwa madai ya kutuma droni ya ujasusi hadi katika makao rasmi ya Naibu wa Rais Dkt William Ruto mtaani Karen ameshtakiwa.

Bw Piotrukasz Litwiniuk ambaye ni raia wa Ureno alishtakiwa kwa makosa manne ambayo ni kuingiza droni hiyo nchini bila kibali kinachohitajika, kuitumia nchini bila idhini inayohitajika, kuihudumu bila kujisajili na pia kukosa kuisajili droni hiyo–makosa yanayokaa mzunguko wa barabara.

Kwa kina, upande wa mashtaka ulielezea mahakama kwamba muundo wa droni hiyo ni Mavic Air2 yenye utambulisho MA2UE3W na ambayo iliingizwa nchini January 7 kupitia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Moi Jijini Mombasa.

Alikiuka sheria za Kenya kwa kuitumia Machi 29 akiwa jirani wa Dkt Ruto na ambapo walinzi waliokuwa wakiwajibikia Usalama wa makazi hayo waliiona angani na wakaifuatilia hadi kuiona ikirejea bomani mwa Mreno huyo.

Mama Rachel Ruto akiwa ndiye bibiye Naibu wa Rais ndiye aliripoti kisa hicho katika kituo cha polisi cha Hardy ambapo timu ya Uchunguzi wa Jinai ilitumwa kupeleleza zaidi.

Mbele ya Hakimu Martha Mutuku wa mahakama ya Milimani, Litwiniuk alikanusha mashtaka hayo na akaachiliwa na bodi ya Sh200,000 pesa taslimu au mdhamini wa Sh500,000, kesi ikitengwa kusikizwa kwa wiki mbili zijazo.

Droni ya jirani yamtia hofu mke wa Ruto

Na MARY WAMBUI

POLISI Jumanne walimhoji raia wa Uingereza ambaye mtambo wake wa kupiga picha angani (droni) ulipaa katika eneo la nyumba ya Naibu Rais, Dkt William Ruto katika mtaa wa Karen, Nairobi.

Kulingana na Kamanda Mkuu wa Polisi eneo la Nairobi, Bw Augustine Nthumbi, droni hiyo ya Bw Hind Jeremy, 37, ilisababisha hofu ilipoonekana na mkewe Naibu Rais, Bi Rachel Ruto.

“Bi Ruto alisema alikuwa ndani ya nyumba mwendo wa saa tisa alasiri siku ya Jumatatu, alipoona kifaa hicho kikipaa kwenye boma lao kutoka kwa Mwingereza huyo ambaye wanapakana naye,” akasema Bw Nthumbi.

Polisi walifika katika nyumba hiyo ya Dkt Ruto na kuchukua kifaa hicho, kabla ya kumwita Mwingereza huyo kwa mahojiano.

Bw Nthumbi alisema kuwa uchambuzi unafanywa ili kujua yaliyomo kwenye droni hiyo.

“Mtambo huo wa droni haujakuwa na kiambatisho chochote cha kutia wasiwasi kulingana na uchunguzi wa awali. Hata hivyo, tulichukua kadi iliyokuwa ndani ili tujue walikuwa wakipiga picha za aina gani na kwa lengo lipi,” alisema Bw Nthumbi.

Kulingana na ripoti, wageni waliokuwa wamemtembelea mwanume huyo ndio waliobeba mtambo huo, waipige picha nyumba yake na kisha wampe kifaa hicho kama zawadi.

Kisa hicho bado kinafanyiwa uchunguzi zaidi na Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) Nairobi, Kitengo cha Polisi cha kupambana na Ugaidi (ATPU) na Huduma ya Kitaifa ya Uchunguzi pamoja na mamlaka ya Safari za Angani.

NGILA: Sheria ya kupiga droni marufuku inaumiza Wakenya

Na FAUSTINE NGILA

NIKIPITIA video za mafuriko msimu huu wa mvua, nilimhurumia mno mwanamume mmoja anayeonekana kukwama katika ‘kisiwa’ kidogo katikati ya Mto Athi.

Kulingana na ripoti kwenye vyombo vya habari, mwanamume huyo kwa jina Vincent Musila alisalia katika eneo hilo ndogo la nchi kavu kwa siku tatu huku mvua ikiendelea kunyesha na maji ya mto yakiongezeka.

Hakuwa na namna yoyote ya kujiokoa, huku mamia ya wakazi wakitazama kwa umbali wasijue la kufanya kumuokoa au kumpa chakula au vazi lenye joto akisubiri kuokolewa.

Ingawa serikali hatimaye ilileta helikopta iliyombeba na kumuondolea dhiki hiyo, nilisalia kuishangaa kwa ilani ya kisheria mpya iliyobuni hapo Novemba 7.

Kulingana na Mamlaka ya Usafiri wa Angani (KCAA), kwa sasa ni hatia kwa mtu yeyote kuendesha droni za kisasa katika anga ya Kenya, iwe kwa manufaa ya filamu, usalama au uokoaji.

Ilani hiyo inaeleza kuwa yeyote atakayenaswa akifanya hivyo atasukumwa ndani mwaka mmoja au kupigwa faini ya Sh100,00, au adhabu zote mbili.

Lakini nikizungumza na mkuu wa kampuni ya droni, simu na mtandao wa 5G, Nokia Bw John Harrington, niling’amua kuwa droni zimekuwa zikitumika katika mji wa Sendai, nchini Japan kuwaokoa watu wakati wa majanga ya tsunami na mafuriko, jambo ambalo limesaidia kuokoa maelfu ya watu.

Droni hutumiwa kuwapelekea watu waliokwama vyakula, maji na nguo, huku pia zikiwaondoa kutoka maeneo ya hatari na kuwapeleka maeneo salama kupitia mawasiliano ya teknolojia ya mawimbi ya 4G LTE.

Hapa Kenya, tumeshuhudia sera hasi ambazo badala ya kusaidia wananchi wakati wa majanga, zinachangia katika kuwadunisha zaidi.

Iweje serikali ipige marufuku ubunifu katika matumizi ya droni, licha ya kujionea watu wengi wakiathirika na hata kufariki wakati huu wa mvua?

Vipi isitambue umuhimu wa teknolojia katika kuwahamisha wakazi walio katika maeneo ya mafuriko na kuwapa chakula?

Na si mafuriko tu, maporomoko ya ardhi yamechangia watu wengi kupoteza makazi yao na kulala kwenye baridi usiku kucha huku wakinyeshewa wasipate msaada.

Ni wakati wa kuwa na utu kwa binadamu wenzetu. Teknolojia ambayo ingemsaidia Bw Musila kufika kwake nyumbani inafaa kurejeshwa.

Haifai kwa KCAA kupiga droni marufuku kwa kuwa serikali imekuwa inatuhadaa inaposema imejitayarisha kukabiliana na majanga haya.

Kusubiri siku tatu kisha uchukue hatua hakutaokoa watu wengi. Tunahitaji droni ziwepo ili tukuze ubunifu wetu katika matumizi yake, mojawapo ikiwa ni suluhu kwa kuokoa au kuwatumia vyakula waathiriwa wa majanga walio maeneo ya mbali yasiyofikika na binadamu.