• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Polisi wafumania watu 3 wakinyakua ardhi ya Ikulu

Polisi wafumania watu 3 wakinyakua ardhi ya Ikulu

NA TITUS OMINDE

Idara ya usalama mjini Eldoret imekamata watu watatu ambao walipatikana wakijenga ua katika sehemu ya ardhi ambayo inamilikiwa na Ikulu ndogo katika eneo la Eldoret Mashariki.

Afisa mkuu wa polisi Eldoret Mashariki Bw Richard Omanga alisema kuwa watu hao walikamatwa kupitia kwa ushirikiano kati ya maafisa wa polisi wakiongozwa na mkuu wa kaunti ndogo ya Kesses Bw Nobert Komora.

Inadaiwa kuwa watu hao walikuwa wafanyakazi wa kampuni moja ya kibinafsi ambayo maafisa wa usalama hawakuwa tayari kuiweka hadharani kwa kile walichokitaja kama kulinda uchunguzi wao.

Kwa mujibu wa Bw Omanga, maafisa wa GSU ambao wanalinda eneo hilo wamewekwa kwa tahadhari baada ya tukio hilo lililotajwa kama ujasiri usiokuwa wa kawaida.

“Ni kweli kuna watu ambao walikamatwa wakijenga ua katika ardhi ya ikulu ndogo, kama polisi hatuna habari zaidi kuhusu tukio hilo kwani maswala ya ardhi yako chini ya serikali ya kaunti,” alisema Bw Omanga

Bw Omanga ambaye alionekana kama kwamba hakutaka kuzungumzia tukio hilo alisema kuwa uchunguzi ungali unaendelea hivyo basi hawezi akazungumza mengi kuhusu kisa hicho.

Hata hivyo, inadaiwa kuwa wale ambao walikamatwa walitumwa katika ardhi hiyo ya mmoja wa wale ambao wamewahi kuhudumu kama wasimamizi wa ikulu wakati wa utawala wa Nyayo.

Tukio hilo limewadia wakati ambapo tume ya maadili na ufisadi nchini imetoa tahadhari dhidi ya unyakuzi wa ardhi ya umma mjini Eldoret.

Kwa mujibu wa EACC, ardhi ya shule za umma, ardhi ya jeshi ya ekari 4,000 ni miongoni mwa ardhi nyingine za umma ambazo ziko hatarini kunyakuliwa.

Wakati tume ya kitaifa ya ardhi ilipozuru kaunti ya Uasin Gishu miaka miwili iliyopita iliambiwa kuwa vyeti vya umiliki ardhi ya umma mjini Eldoret ikiwa ni pamoja na makao makuu ya kaunti ya Uasin Gishu, hospitali ya kaunti, shule za umma zilizokuwa za manispaa zimo mikononi mwa watu binafsi.

You can share this post!

Sonko amsafirisha Conjestina hadi Nairobi kwa matibabu

Serikali sasa kufuatilia mawasiliano ya WhatsApp

adminleo