• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 2:25 PM
TAHARIRI: Mradi wa nyumba za bei nafuu utawafaa Wakenya

TAHARIRI: Mradi wa nyumba za bei nafuu utawafaa Wakenya

NA MHARIRI

Serikali ya Jubilee ilipochukua hatamu za uongozi katika muhula wake wa pili mwaka jana, ilibuni mikakati minne ya maendeleo maarufu kama Ajenda Nne Kuu.

Miongoni mwa nguzo muhimu za ajenda hizi ni kujenga makazi au nyumba za bei nafuu kwa wananchi katika miji mbalimbali, hasa Nairobi. Mradi huu ukifanishwa, tatizo la uhaba wa makao utakuwa umetatulika.

Huu utakuwa ufanisi mkubwa na utampa Rais Kenyatta sifa tele aondokapo madarakani 2022.

Wakenya wengi wanaishi katika mitaa ya mabanda kama Mathare, Kibera na Mukuru na wako katika hatari ya kuambukizwa magonjwa yatokanayo na uchafu.

Hivyo, makazi ya bei nafuu yatawafaa watu hawa na hata kuinua maisha yao na familia zao.

Hivi majuzi, Kaunti ya Nairobi imekuwa ikifukuzana na watu/watoto wanaorandaranda mitaani maarufu kama chokoraa ikitaka kuwaondoa katikati ya jiji. Aghalabu wengine ni watu wasiokuwa na makao rasmi, wao hulalalala tu barabarani jijini.

Ikiwa watu kama hawa wanaweza kupata makazi haya ya bei nafuu, maisha yao yataboreka zaidi na fujo hizi za kufukuzana na askari wa jiji zitaisha.

Nyumba za bei nafuu kwa wakazi wa mabanda na makao yasiyolipiwa kwa wasiokuwa nayo ni jambo lenye natija kubwa na ufumbuzi kwa uhaba wa makao bora kwa wananchi.

Mkakati huu unapaswa kutekelezwa kwa uangalifu mkubwa ili usikumbwe na ufisadi wa aina yoyote. Ni mpango ambao utampa Rais Kenyatta sifa na staha anayoisaka baada ya kuondoka madarakani. Kwa miaka mingi, atakumbukwa kama kiongozi aliyeondoa mitaa ya mabanda na kuwapa wananchi wa Kenya makazi bora yenye heshima.

Ufanisi katika shughuli hii utakuwa kama kuua ndege watatu kwa jiwe moja: Kuwapa makao wasiokuwa nayo, kuondoa mitaa ya mabanda na kupunguza viwango vya umaskini.

Takwimu za ripoti ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2014 zaonyesha kuwa asilimia 56 ya Wakenya wanaishi katika mitaa ya mabanda. Idadi hiyo si ndogo!

Kwa hivyo wazo la kuwapa Wakenya makao ya bei nafuu lilikuja wakati mwafaka na litawafaa Wakenya.

You can share this post!

WANDERI: Mauaji ya zamani yachunguzwe kuanika waliohusika

AKILIMALI: Kijana aungama anautambua utamu wa mapapai

adminleo