• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 4:48 PM
Mwanaume avamia shule kwa nyundo na kujeruhi watoto 20

Mwanaume avamia shule kwa nyundo na kujeruhi watoto 20

MASHIRIKA na PETER MBURU

MWANAUME mmoja nchini Hong Kong alivamia shule ya msingi katika Jiji la Beijing akiwa amejihami kwa nyundo na kuwajeruhi vibaya watoto 20 Jumanne, serikali ya nchi hiyo ilisema.

Watoto watatu walipata majeraha mabaya katika vamizi hilo la saa za asubuhi, serikali ya Beijing ikasema kupitia mitandao ya kijamii.

Mwanaume huyo wa miaka 49 ambaye alikuwa akifanya kazi ya ujenzi katika shule hiyo baadaye alikamatwa na polisi na kuzuiliwa.

Alisemekana kuchukua hatua hiyo baada ya shule kukataa kumpa kandarasi mpya ya kazi yake baada ya muda wa kandarasi ya awali kukamilika.

Habari ya polisi ilisema kuwa mwanaume huyo aliwavamia wanafunzi kwa nyundo aliyokuwa akifanya kazi nayo walipokuwa madarasani, na akawajeruhi katika harakati hizo.

Katika video iliyosambaa mitandaoni, mwalimu mkuu wa shule hiyo aliwaambia wazazi kuwa mshukiwa alivamia watoto katika madarasa sita tofauti.

Wazazi walioshtuka walifika katika shule hiyo kwa wingi wakitaka kujua ikiwa watoto wao walikuwa salama.

Tukio hilo lilivutia umma mkubwa kutokana na hali kuwa shule hiyo iko kati mwa jiji kuu la China.

Mnamo Aprili mwaka uliopita, mwanaume aliyejihami kwa kisu aliua watoto tisa na kujeruhi wengine 10 katika shule moja China.

Miezi miwili baadaye, mwanaume mwingine aliyekuwa akichomelea kisu aliua wanafunzi wawili na kujeruhi watu wengine wawili nje ya shule moja jijini Shanghai.

Mnamo Oktoba, mwanamke aliyekuwa na kisu aliua wanafunzi 14 katika shule ya chekechea eneo la Kusini Magharibi mwa China.

Mwezi uliopita, watu wanane waliuawa na zaidi ya 20 kujeruhiwa wakati mwanaume aliyejihami kwa kisu alivamia basin a kuliendesha hadi mahali palipokuwa na msongamano wa magari eneo la Kusini Mashariki mwa China, mkoa wa Fujian.

Wataalam wamesema kuwa hasira za kijamii miongoni mwa watu zimekuwa zikishuhudiwa kwa wingi kutokana na hali ya ukosefu wa ajira miongoni mwa watu wengi na kuzidi kushuhudiwa kwa tofauti za kimaisha.

You can share this post!

Gwiji wa ngwenje Jeff Bezos na mkewe kutalikiana

Watu wasahaulifu sana wana akili nyingi – Utafiti

adminleo