• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
UFISADI: Maraga na Kihara watofautiana

UFISADI: Maraga na Kihara watofautiana

NA CECIL ODONGO

JAJI Mkuu David Maraga na Mwanasheria Mkuu Kihara Kariuki jana walitofautiana kuhusu namna uchunguzi na maamuzi ya kesi za ufisadi zimekuwa zikiendeshwa.

Tofauti hizo zilijitokeza wakati wa kuapishwa kwa mkuu mpya wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi(EACC) Twalib Mbarak katika majengo ya mahakama ya Juu jijini Nairobi.

Bw Kariuki alionekana kumlenga Bw Maraga aliposema Wakenya hawajaridhishwa na namna idara ya mahakama imekuwa ikishughulikia kesi za ufisadi.

“Naweza kusema hapa Bw Jaji mkuu kwamba matarajio ya Wakenya hayajatimizwa. Tumechukua muda mwingi katika kuzungumza ilhali hatujapata matokeo mazuri ya kuwapa Wakenya ambayo ni wajibu wetu kisheria,”

“Ingawa mahakama ni idara huru, uhuru wake haufai kuwa kizingiti au kisingizio cha kutowajibika na kukosa kufanya mambo kwa ukweli. Idara ya mahakama inafaa kuhakikisha kwamba kesi hizi zinakamilika haraka na haziendelei milele,” akasema Bw Kihara.

Aidha Bw Kihara pia alishtumu ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa mashtaka ya umma(DPP) kwa kufanya uchunguzi usiozaa ushahidi tosha wa kusaidia kuwahukumu wafisadi na kutaka kila idara kuwajibika vilivyo ili kutokomeza uovu huo.

Lakini Bw Maraga alijibu akisema mahakama haiwezi kuwahukumu wafisadi bila ofisi ya DPP kuwapa ushahidi wa kutosha huku akisisitiza kwamba idara hiyo haifai kulaumiwa kutokana na kufeli kwa kesi nyingi za ufisadi.

“Idara ya mahakama ipo tayari kushughulikia kesi hizi. Vita dhidi ya ufisadi vitafanikiwa iwapo vitatekelezwa kulingana na sheria na mwongozo wa kikatiba. Asasi zinazofanya uchunguzi zinafaa kuleta mahakamani kesi baada ya kufanya uchunguzi wa kina na wakiwa na matumaini ya kuzishinda kesi zao,” alisema Bw Maraga.

“Tumefikia kiwango ambacho Wakenya ni werevu na wanajua wakati tunashiriki sarakasi kwa kisingizo kwamba tunapigana na ufisadi,” akasema Bw Maraga akionekana kujitetea na kulaumu ofisi ya DPP.

Mkuu mpya Bw Twalib naye aliahidi kwamba atahakikisha mali yote ya umma iliyoibwa imerejeshwa na pia kujizatiti kuwahamasisha Wakenya kuhusu ufisadi.

“Naomba uungwaji mkono kutoka kwa idara ya mahakama, ofisi ya DPP, vyombo vya habari na Wakenya wote. Naahidi kwamba nitatumia rasilimali zilizopo kupigana na ufisadi na kuwakabili wafisadi,” akasema Bw Mbarak aliyechukua nafasi ya Halakhe Waqo.

Muda wa Bw Waqo wa miaka sita kama Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC ulikamilika mwaka jana.

Mwenyekiti wa EACC Askofu Eliud Wabukhala naye aliahidi kwamba atashirikiana na Bw Mbarak na kumsaidia katika juhudi zake ili kuzidisha vita dhidi ya ufisadi.

Bw Wabukala aliongeza kwamba tume hiyo imekuwa ikikabiliwa na shinikizo kutoka kwa baadhi ya wanasiasa ili kubadili namna makachero wake wamekuwa wakiwakamata wafisadi ila akaitetea akisema huwa wanafuata sheria na kuzingatia haki za wanaokamatwa.

Alisisitiza kwamba EACC itafanya kila juhudi kushirikiana na asasi nyinginezo kama Idara ya Upelelezi na afisi ya DPP pamoja na mahakama ili kufanikisha vita dhidi ya ufisadi.

Msajili Mkuu wa mahakama Ann Amadi aliongoza kuapishwa kwa Bw Mbarak ambaye uteuzi wake uliidhinishwa na mahakama mwaka 2018.

You can share this post!

Mwanachuo auawa na wenzake akijaribu kuvunja ofisi

Serikali ya Lamu yaacha wanafunzi kwenye mataa

adminleo