• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
AKILIMALI: Ukistaajabu ya kuku wa kienyeji basi hujui ya kuku wa Kifaransa

AKILIMALI: Ukistaajabu ya kuku wa kienyeji basi hujui ya kuku wa Kifaransa

Na CHARLES ONGADI

NI katika kijiji cha Mabambani eneo la Majengo Kanamai kaunti ya Kilifi ambako tunakutana na Abdulmumin Mohammed, 23, mfugaji maarufu wa kuku spesheli kutoka nchini Ufaransa.

Tofauti na kuku wa kawaida, aina ya kuku hawa wana kimo kifupi sana na wenye manyoya yaliyotapakaa hadi miguuni mwao.

Ni nadra sana kwa wafugaji wengi wa kuku hasa maeneo ya Pwani kuweza kumudu kuwafuga kuku hawa wanaohitaji umakini, usafi wa hali ya juu na kujitolea.

“Nilipewa mayai ya kuku hawa na rafiki yangu aliyekuja nayo kutoka nchini Ufaransa na baada ya kuyaweka katika mashine spesheli yakaangua vifaranga baada ya kipindi fulani,” asema Abdulmumin ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa nne katika Chuo Kikuu cha Pwani.

Kuna aina mbili ya kuku hawa; Silky walio na manyoya meupe na Bantam walio na manyoya meusi wote wakiwa na umbo dogo na la kuvutia.

Aghalabu kuku hawa hutumiwa kama kivutio kwa wageni katika boma na hoteli nyingi za kitalii zilizo mwambao wa Pwani.

Aidha, nyama ya kuku hawa ni tamu na huuzwa kwa bei ghali. Mara nyingi hupatikana tu katika hoteli hizi za kitalii na maeneo ya burudani.

Kipindi cha miezi sita

Abdulmumin anafichulia Akilimali kwamba huchukua takriban miezi sita kwa kuku hawa kukua na kukomaa tayari kuanza kutaga mayai.

Hata hivyo, anasema kwamba kuku aina ya Silky hutaga kati ya mayai sita hadi nane wakati aina ya Bantam hutaga kati ya mayai 10 hadi 20.

Abdulmumin anaongeza kwamba ili kufaulu katika ufugaji wa aina hii ya kuku, mfugaji anapaswa kuwa makini kila wakati kwa kujihami kwa dawa za kukabiliana na mkurupuko wa magonjwa.

“Kila baada ya wiki mbili ninahakikisha kuku wangu wamepata chanjo kutoka kwa Daktari anayenitembelea hapa ili kuzuia magonjwa na wadudu hatari kwa usalama wao,” asema Abdulmumin aliyeanza ufugaji akiwa kinda wa miaka tisa pekee.

Kulingana na mfugaji huyu, kuku hawa wanakula vyakula kama tu kuku wa gredi ijapo kwao wanaweza kula vyakula vya kawaida kama mahindi, mtama na ikizidi hata ugali.

Wanapendeza sana unapowatazama na mara nyingi hununuliwa na mabwanyenye wanaowafuga majumbani mwao kama pambo sawa na wenye hoteli za kifahari maeneo ya Pwani.

Abdulmumin anasema kwamba ameweza kujilipia karo yake katika Chuo Kikuu na pia kutumiza baadhi ya mahitaji yake muhimu kutokana na ufugaji wa kuku hawa.

Kuku mmoja aina ya Silky anauza kwa kiasi cha Sh7,000 na mara nyingi huuzwa wawili wawili kwa Sh14,000 wakati aina ya Bantam anauza kwa Sh3,500 na hupunguza bei hadi Sh6,000 wakiwa wawili.

Anasema kwamba biashara yake hunoga inapokaribia mwezi wa Desemba na huuza kati ya kuku 15 hadi 20 jambo analokiri limekuwa likimwingizia pato zuri kila mwaka.

Hata hivyo, Abdulmumin anakiri kwamba amekuwa akipata changamoto ya kupata soko nchini jambo ambalo humlazimisha kuvuka boda hadi mjini Arusha nchini Tanzania ambako wateja wake wamekuwa wengi.

“Wengi hutaka kuwafuga kuku hawa ila wengi hudai kwamba hawana soko la haraka kutokana na bei yao ghali,” asema Abdulmumin.

Hata hivyo, Abdulmumin anasema kwamba baadhi ya mabwanyenye hasa wanasiasa maarufu nchini wamekuwa wateja wake wa dhati huku wengine wakilazimika kusafiri kutoka Nairobi, Thika na hata Kisumu kuja kununua kuku hawa.

Anakiri kwamba ufugaji wa kuku hawa unalipa ila unahitaji uvumilivu kutokana na kwamba huchukua kipindi kirefu kabla ya kupata soko.

Anasema juhudi zake kuwahimiza wafugaji wenzake zimegonga mwamba kutokana na wengi wao kushindwa kuvumilia.

You can share this post!

AKILIMALI: Utaratibu mwafaka wa kukuza nyasi kwa ajili ya...

Serikali yakana njaa imeua Wakenya, madaktari wataka...

adminleo