• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Viongozi wamtafuna Atwoli kusema Ruto hatakuwa debeni 2022

Viongozi wamtafuna Atwoli kusema Ruto hatakuwa debeni 2022

NA BENSON AMADALA

WANDANI wa Naibu Rais Dkt William Ruto kutoka Magharibi mwa nchi jana walimkashifu Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU) Francis Atwoli kutokana na matamshi yake akiwa Kisiwani Lamu kwamba jina la Dkt Ruto halitakuwa kwenye orodha ya wawaniaji wa Urais 2022.

Viongozi hao waliojumuisha aliyekuwa Seneta wa Kakamega Dkt Bonny Khalwale, Spika wa Seneti Ken Lusaka, mbunge wa Kimilili Dismus Baraza, Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu miongoni mwa wengine walimkemea kinara huyo wa wafanyakazi na kusema Dkt Ruto anaungwa mkono na wafuasi wengi kuliko idadi ya wafanyakazi anaowasimamia.

“Hatujui Bw Atwoli anazungumza kwa niaba ya nani kwa kuwa tunajua yeye ni kiongozi wa wafanyakazi ambao idadi yao haiwezi kulinganishwa na wafuasi wa Dkt Ruto. Aliamua kunilaani kwa kumuunga mkono Naibu Rais ila anafaa kufahamu kuwa laana hiyo haitanishika kamwe,” akasema Dkt Khalwale katika Shule ya Msingi ya Township, Kakamega wakati wa mchango wa Kanisa la Salvation Army, hafla iliyohudhiriwa na Dkt Ruto.

Bw Barasa naye alisema ufuasi anaojivunia Dkt Ruto eneo la Magharibi na maeneo mengine ya nchi hauwezi kulinganishwa na ule wa wapinzani wake.

Gavana wa Kiambu ambaye aliandamana na Dkt Ruto aliwataka wakazi wa eneo la Magaharibi kuwaiga wananchi wa Kiambu ambao alisema watampigia kura Naibu Rais katika uchaguzi wa 2022.

Akihutubu, Dkt Ruto aliwakashifu viongozi wanaoeneza propaganda dhidi yake akisema hayo hayatamzuia kuwajibikia wananchi.

“Watu wanaotembelea waganga kila mara hutumia muda wao kueneza propaganda kunihusu kwa sababu mimi huenda kanisani kuomba na Wakristo wengine na kutoa sadaka yangu,” akasema Dkt Ruto.

You can share this post!

Mkutano wa Raila wachemsha siasa Bonde la Ufa

‘Tangatanga’ wataka wapinzani watimuliwe Jubilee

adminleo