• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 2:10 PM
AKILIMALI: Mkulima analala pazuri kwa kufuga kondoo kwa ajili ya sufu na nyama

AKILIMALI: Mkulima analala pazuri kwa kufuga kondoo kwa ajili ya sufu na nyama

Na RICHARD MAOSI

NYANDA za juu katika Bonde la Ufa, ni mwafaka kwa ufugaji wa kondoo hasa kwa ajili ya uzalishaji wa nyama na manyoya (sufu).

Kondoo wenye sufu na miili mikubwa ni wa kupendeza, wepesi kuelekezwa, watiifu na wamekuwa wakichangia asilimia kubwa ya pato la kitaifa.

Ni wanyama wanaoweza kufugwa kwa gharama nafuu, kutokana na uwezo wao mkubwa wa kukabiliana na aina mbalimbali ya maradhi.

Mfugaji anapaswa kuwateua kulingana na sifa zao, kwa kuzingatia ushauri anaopata kutoka kwa mtaalamu wa mifugo.

Erick Kiprotich kutoka eneo la Mlango, Kaunti ya Nandi akiwalisha baadhi ya kondoo wake eneo la Biribiriet. Picha/ Richard Maosi

Wazo la watu kuwa mfugaji wa kondoo ni lazima awe wa kuhamahama kutoka sehemu moja hadi nyingine, limepitwa na wakati.

Katika maisha ya kisasa kuna maeneo maalum ya kufuga kondoo kabla ya kuwahamisha kwingineko nyasi zinapopungua.

Erick Kiprotich Kirior kutoka eneo la Biribiriet, Mlango kaunti ya Nandi anasema alianza kufuga kondoo 2007 ili kujiongezea kipato.

Akizungumza na Akilimali alisema mradi mtu atambue siri ya kufuga kondoo, bila shaka ataepuka ushindani mkali kutoka kwa wakulima wakubwa waliojistawisha.

Akiwaelezea wenzake kuhusu ufugaji bora wa kondoo. Picha/ Richard Maosi

“Kondoo waliagizwa kutoka mataifa ya ulaya. Kwa mfano, Merino ni wenye asili ya Uhispania na spishi nyinginezo zilizoagizwa kutoka Uingereza,” akasema.

Anasema kwa sababu wafugaji wengi huazimia kuwafuga kondoo kwa ajili ya nyama tu, yeye huwafuga kwa sababu ya sufu na kuuza yaani ufugaji biashara.

Kaunti jirani ya Uasin Gishu huagizia bidhaa kutokana na wanyama hawa, wanaoweza kumpa mkulima tija nzuri kila mwisho wa mwezi.

Erick anafuga spishi ya Merino wenye vichwa vyeusi.

Mtambo anaotumia kusaga chakula cha kulisha kondoo msimu wa kiangazi. Picha/ Richard Maosi

Erick anaongezea kuwa katika hatua za mwanzo, kibanda cha kondoo kinahitaji kuwa katika sehemu ambayo ni salama wasije wakashambuliwa na wanyama.

Aidha, sehemu hiyo isiwe ya kufanya maji kutuama hasa ijapo majira ya msimu wa mvua nyingi.

Hiyo inamaanisha kuwa ni lazima mkulima atie juhudi nyingi,na jasho kwa kununua kondoo dume wenye nguvu wanaojamiiana na wale wa kike ili kuendeleza kizazi.

Malisho

Erick anasema msimu wa baridi shadidi ni baina ya Aprili na Julai na wakati huo malisho huwa yanapatikana kwa wingi mashambani.

Chakula cha mabaki ya mahindi na ukoko wa unga kilichosagwa kuwalisha kondoo. Picha/ Richard Maosi

“Hata hivyo msimu wa kiangazi sisi hulazimika kuwapelekea kondoo malisho katika makazi yao na kuwapimia lishe wasije wakataabika kama walivyozowea msimu wa mvua,” akasema.

Wakati mwingine msimu wa kiangazi yeye hulazimika kuwalisha kondoo na mabaki ya nyasi yaliyokauka kwa kuchanganya vyema na aina ya shayiri ili kuongezea lishe ladha.

Yeye hulisha kondoo wake wenye umri wa mwaka mmoja na zaidi kwa mboga, anazokuza katika shamba lake, mbali na kuongezea lishe za ziada.

Kondoo waliokomaa hujisakia michicha, inayokuwa pembeni ya shamba lake akisema wanyama hawa wana tabia ya kuchagua sana malaji.

Sehemu inayotumika kulisha kondoo. Picha/ Richard Maosi

Isipokuwa kondoo jike wenye ujauzito wanaohitaji uangalifu wa karibu, na mchanganyiko wa lishe nyinginezo ili kuwafanya wawe katika hali nzuri wasije wakazurura kila sehemu wakijitafutia lishe.

Kujifungua

Anasema kondoo wengi hujifungua bila matatizo wala kuhitaji msaada wa mfugaji, aghalabu mara mbili au tatu kila mwaka.

Mkulima akibahatika anaweza kuambulia pacha au hata mapacha na hii ni faida zaidi ya maradufu ikizingatiwa mwana-kondoo huchukua muda mfupi sana kukomaa(miezi mitatu).

Baada ya miezi mitatu au zaidi anasema wanakondoo wanaweza kujitegemea ndiposa madume na majike yanayosalia hupelekwa kwenye viwanda vya nyama.

Mtambo wa kupiga maji kunywesha kondoo. Picha/ Richard Maosi

Anasema kondoo anapohitimu miaka miwili yeye huwa tayari kujaamiana na madume kwa ajili ya kuleta kizazi.

Erick anasema kufuga kondoo ni kazi anayojivunia,yeye hulazimika kukata manyoya mara moja kila mwaka na kuuza kwenye viwanda vinavyotengeneza nguo na blanketi.

“Mimi huwaajiri watalamu wa kukata manyoya kulingana na idadi ya kondoo wanaokatwa manyoya kila siku,” alisema.

Anasema kondoo jike ndio huwanda vizuri na kutoa kiwango kizuri cha sufu ambacho ni baina ya kilo 4.5 na sita.

Kazi inayofuata ni kupakia sufu vizuri katika makasha yasiyokuwa na unyevu kwa ajili ya usafirishaji katika masoko ya nje, akiwahakikishia wanunuzi kuwa sufu ya kondoo ni bora kuliko za kutengenezwa viwandani.

Kulingana na Erick ni muhimu kwa mkulima kuhakikisha kondoo wake wanalala katika sehemu iliyo safi wasije wakapata kupe wala chawa.

Hili utagundua pale anapowashwa na kujikuna kwenye ukuta au ua.Anashauri kuwa hatua hiyo huwaachia vidonda vingi endapo wataumia.

Eneo ambamo kondoo hunywa maji. Picha/ Richard Maosi

Aidha hali hiyo huharibu ubora wa sufu na kupoteza thamani yake kwa sababu hunyonyoka kutoka milini na kuwa nyepesi.

Amefanya kuwa jambo la kawaida kuwanywesha kondoo dawa ya kuwakinga dhidi ya maradhi ya vimelea vya bakteria na minyoo.

Ili kuwaepusha dhidi ya maradhi ya midomo na miguu,yeye huwaepusha kutangamana na kondoo wengine ambao wanaweza kuwa wameadhirika.

Kiprotich anasema mkulima anaweza kuvuna hela nzuri anapouza kondoo aliyekomaa, kati ya 12000-15000 kulingana na uzani.

Waagizaji wengi humiminika nyumbani kwake msimu wa sikukuu kama vile pasaka au Krismasi kununua sufu,nyama au kondoo akiwa hai.

Anasema kazi ya kufuga kondoo haina ushindani mkubwa kwa sababu sio wakulima wengi waliozamia kilimo cha sampuli hii, kilichozoeleka sana bara Ulaya.

You can share this post!

Wito kwa wazazi mitaani wapeleke wana kwa taasisi za ufundi

AKILIMALI: Ufugaji ng’ombe kwa makini na kuwapa lishe...

adminleo