• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 2:10 PM
AKILIMALI: Anajivunia ufanisi mkuu katika ufugaji wa aina mbalimbali za ndege wa nyumbani

AKILIMALI: Anajivunia ufanisi mkuu katika ufugaji wa aina mbalimbali za ndege wa nyumbani

Na CHARLES ONGADI

NI wafugaji wachache sana huzingatia ufugaji wa batamzinga kama kitega uchumi mkoani Pwani licha ya ufugaji huo kuwa na tija.

Hata hivyo, Bw Joseph Juma ambaye ni mfugaji maarufu wa kuku, bata, sungura, kanga eneo la Makande, Mombasa, kaamua kuvalia njuga ufugaji wa batamzinga.

“Tofauti na mifugo wengine, ufugaji wa Bata mzinga unahitaji umakini mkubwa ambao ukizingatiwa faida inaweza kuonekana kwa haraka sana,” anasema Bw Juma alipotembelewa na Akilimali majuzi.

Kulingana na Bw Juma, ufugaji wa bata-mzinga unahitaji kujitolea, subira na kujituma kwa mfugaji ili kupata faida.

Anasema kwamba alinunua bata-mzinga wake wa kwanza kutoka kaskazini mwa nchi ya Uganda alikoenda kwa ziara ya kikazi.

Kinyume na kuku ambaye huchukua takribani siku 21 ili kuangua mayai yake, bata mzingi huchukua kipindi cha siku thelathini ili kuangua.

Tofauti na wanyama wengine, Bw Juma anaeleza kwamba ni vigumu sana kwa bata mzinga kuvamiwa kiholela na magonjwa.

“Batamzinga ana uwezo wa kustahimili hali ngumu na magonjwa ya kila aina tofauti na wafugaji wengi wanavyodhania,” anasema Juma.

Hata hivyo, mara wanapoangua mayai, nyuni hao uhitaji chanjo ya kwanza ili kuwaepusha na aina mbalimbali za magonjwa.

Bw Juma anayefuga zaidi ya batamzinga 20, wa kike na wa kiume, anasema kwamba punde wanapoanguliwa vifaranga uhitaji joto, mazingira safi na hewa safi kila mara.

Ili kufikia uzani unaohitajika, batamzinga uhitaji malisho mazuri ikiwemo wishwa, mahindi, mboga za sukuma Wiki zilizokatatwakatwa vipande na nyanya.

Bw Juma anasema kwamba amefaulu katika ufugaji wa batamzinga kutokana na kupatikana kwa urhisi kwa vyakula hivyo anavyotoa katika soko kuu la Kongowea.

Anasema kwamba ndege hawa wake aghahalabu huwa na uzani wa kati ya kilo 12 hadi 15 uzani ambao hupendwa sana na wafanyibiashara wengi wanaofika kununua bidhaa hii.

Anauza bata mzinga mmoja aliyekomaa kwa kati ya Sh4,500 na Sh5,500 kwa wateja wake ambao huwa ni wenye hoteli za kifahari Pwani.

Kama walivyosema wahenga kwamba kibaya chajiuza na kizuri chajitembeza, Bw Juma anaeleza kwamba mara nyingi wateja wake huja wenyewe kwake kutafuta bidhaa hiyo.

Anasema katika likizo ya Desemba 2018 aliuza Batamzinga 10 na kuweza kujitengezea hela nzuri.

Mbali na ufugaji wa kanga, bata wa kawaida, kuku na sungura, Bw Juma asema kwamba ufugaji wa bata mzinga umeweza kumnyanyua juu kiuchumi kutokana na kwamba imeweza kumwezesha kuwafunza wanawe wawili hadi chuo kikuu.

Mbali na kuchuma hela lakini kinachompatia motisha kuendeleza ufugaji hasa wa Batamzinga ni pale wanafunzi wa vyuo mbali mbali wanapomtembelea kutafuta ushauri.

“Mara nyingi ninaridhika ninapowapatia wanafunzi kutoka vyuo mbali mbali ushauri ambao baadaye uwasaidia katika maisha yao ya baadaye,” anasema mfugaji huyu.

Ushauri wake ni kwa vijana ambao hawana kazi kujizama katika ufugaji wa batamzinga ambao hauna wafugaji wengi Pwani na taifa kwa ujumla.

Anasema kwamba ufugaji wa batamzinga hauna ushindani kama ulivyo katika ufugaji wa kuku hivyo faida yake huwa ni ya uhakika licha ya kwamba mfugaji anahitajika kusubiri kipindi cha mwaka mmoja.

Kwa sasa Bw Juma anasaidiana na watoto wake katika kuendesha ufugaji wa batamzinga ambao ni nadra sana mkoani Pwani.

You can share this post!

Griezmann akubali kugura Atletico na kutua Barcelona

Matiang’i aahidi kumaliza genge la mauaji eneo la...

adminleo