• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 10:50 AM
Nitakaa na Ruto sako kwa bako, aapa Jumwa

Nitakaa na Ruto sako kwa bako, aapa Jumwa

Na CHARLES LWANGA

MBUNGE wa Malindi, Aisha Jumwa ameapa kuendelea kumpigia debe Naibu Rais William Ruto kuwa rais 2022. Hii ni licha ya tishio kutoka kwa chama chake cha ODM la kuwaadhibu wabunge waasi.

BI Jumwa alizungumza siku moja baada ya kiranja wa walio wachache bungeni Junet Mohamed kueleza nia ya ODM kumwondoa mbunge huyo katika kamati ya Utumishi wa Bungeni (PSC) yenye mamlaka makubwa.

Katika kikao cha wanahabari jana mjini Malindi, mbunge huyo, ambaye alikuwa mmoja wa wandani wakuu wa Kiongozi wa ODM Raila Odinga eneo la Pwani, alisema hatakubali kutishwa na mtu yeyote kuhusu misimamo yake ya kisiasa.

“Hatutakubali kutishwa. Kama nilivyosema awali, sina mgogoro wowote na ODM wala kiongozi wa chama. Lakini msimamo wangu kumuunga mkono Bw Ruto kuwa rais 2022 hautabadilika. Huo ni uamuzi wangu,” akasema.

Bi Jumwa aliongeza kuwa haijalishi kama ODM kitakuwa na mgombeaji wa urais 2022 lakini msimamo wake wa kisiasa utabaki kuwa anamuunga mkono naibu rais.

“Sioni kama kuna shida yoyote na msimamo huo, na hili halifai kuwa suala linaloibua utatanishi katika ODM,” akasema.

Kulingana naye, ripoti kwamba chama kimenuia kumwondoa katika kamati ya bunge ni uvumi kwani hajapokea mawasiliano yoyote rasmi kutoka kwa Spika wa Bunge Justin Muturi kuhusu suala hilo.

“Sijafanya kosa lolote. Ninafuata tu nyayo za Raila Odinga, na ninataka kusema kuwa sina ubishi wowote dhidi ya chama, viongozi wake wala wanachama wengine. Wadhifa niliopewa katika PSC haukuwa wa hisani bali ni haki ya Wapwani baada ya kukipa chama kura nyingi katika Uchaguzi Mkuu uliopita,” akasema.

Aliongeza: “Sisi ni washirika katika ODM na kila mmoja anajua tulivyochangia pakubwa chamani wakati wa uchaguzi uliopita. Kwanza tulipewa nafasi chache sana katika ODM.”

Kulingana naye, msimamo wake kumfuata Bw Ruto ulitokana na muafaka wa Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta kuleta umoja wa kitaifa, na pia unalenga kufanikisha malengo ya maendeleo yanayoendelezwa na serikali kuu.

Kwenye barua iliyoandikwa kwa spika wa bunge, Bw Mohammed, ambaye pia ni Mbunge wa Suna Mashariki, alitaka apewe mwongozo wa jinsi ya kumwondoa Bi Jumwa kutoka wadhifa huo wa PSC.

Kuna wabunge karibu kumi wa upinzani kanda ya Pwani ambao wamekuwa wakihudhuria msururu wa hafla za Bw Ruto katika eneo hilo, huku wengine wao wakitangaza wazi kuunga mkono maazimio yake ya urais.

Baadhi yao, akiwemo Bi Jumwa, walihepa kuhudhuria mkutano wa chama cha ODM mnamo Jumatatu uliosimamiwa na Bw Odinga mjini Mombasa.

Lakini Bi Jumwa alisema alikuwa amearifu chama mapema kwamba hakuwa nchini kwa hivyo hangehudhuria mkutano huo.

You can share this post!

‘Mchungaji’ achoma nyumba mkewe kumtomzalia...

Mkuu wa ATPU aamriwa kufika kortini

adminleo