• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:55 AM
Afiza wa zamani wa KDF asema polisi walitaka kumtia adabu

Afiza wa zamani wa KDF asema polisi walitaka kumtia adabu

Na RICHARD MUNGUTI

AFISA wa Majeshi ya Kenya (KDF) aliyesimamishwa kazi Jumatatu alitoboa kortini siri ya polisi mbele ya hakimu mkuu Martha Mutuku.

Lucas Lengesa Andika aliyekabiliwa na mashtaka mawili ya kujifanya afisa wa polisi na kupatikana na pingu alifichua kortini kuwa “afisa wa polisi aliyenikamata alinieleza wazi wazi atanitoa ujinga tunaokuwa nao sisi maafisa wa KDF.”

Lengesa alifichua kuwa yeye ni afisa wa jeshi la nchi kavu na aliahidiwa “kutolewa ujinga na udaku kwa kutengenezewa kesi na kuwekelewa.”

Alikuwa akihudumu katika kampi ya kijeshi iliyoko Isiolo. Kwa sasa mshtakiwa huyo alisema hana kitambulisho cha kitaifa.

Lengesa alimweleza Bi Mutuku kuwa alikutana na maafisa wa polisi wakishika doria kisha “akaitishwa kitambulisho.”

“Naomba kukueleza kwa Kiswahili mheshimiwa,” Lengesa aliomba mahakama. “Eleza,” Bi Mutuku alimruhusu.

Mshtakiwa huyo alifichua kuwa yeye ni afisa wa KDF aliyesimamishwa kazini. “Mimi sina kitambulisho cha kitaifa kwa vile nilipoajiriwa kazi katika KDF kitambulisho changu kilichukuliwa na kuwekwa hadi wakati ule nitakapostaafu,” Lengesa alimweleza hakimu.

Mshtakiwa huyo aliendelea, “Niliposimamishwa niliwaeleza maafisa hao wa polisi sina kitambulisho kwa vile nimesimamishwa kazini. Lakini wakaapa watanifundisha somo kwa vile maafisa wa KDF huwa na utoto mwingi sana.”

Lengesa alisema afisa huyo wa polisi alimweleza kuwa “atamtengenezea kesi hadi ajute.”

Mahakama ilifahamishwa Lengesa alipelekwa kituo cha polisi cha Central aliposhtakiwa kujifanya afisa wa polisi na kupatikana na pingu.

“Naomba hii mahakama inisaidie vile iwezavyo kwa vile nikuonewa nimeonewa na afisa aliyenitia nguvuni alitaka kulipiza kisasi alicho na idara ya majeshi,” alisema Lengesa.

Mshtakiwa aliachiliwa kwa dhamana ya Sh100,000 pesa tasilimu kisha akaelezwa amweleza hakimu atakayesikiza inayomkabili.

“Lakini mheshimiwa naomba unikinge na uwongo huu wa polisi. Nimewekelewa tu. Ningelitoa pingu wapi na siko kazini?” alisema Lengesa.

Kesi itatajwa Januari 18, 2021.

You can share this post!

Miguna aahidi kuzima ufisadi Nairobi

Chifu asimamishwa kazi kwa kutafuna hongo ya Sh30,000