Wamiliki wa matatu Mlima Kenya walia huduma ya reli imemeza riziki yao

Na CHARLES WASONGA

CHAMA cha wamiliki wa matatu (MOA) eneo la Mlima Kenya kimeomba kufanya mkutano na maafisa wa Shirika la Reli Nchini (KRC) kujadili suala la nauli.

Hii ni baada ya zaidi ya wasafiri 5,000 kuamua kutumia huduma ya gari moshi kati ya Nairobi na Nanyuki msimu wa Krismasi, na kuwanyima wahudumu wa matatu biashara.

Shirika la KRC linatoza nauli ya Sh200 kutoka Nairobi kwenda Nanyuki ilhali matatu zinalipisha Sh600 kwa wastani kwa safari hiyo hiyo. Hali hii ilipelekea wasafiri wengi kuamua kutumia usafiri wa gari moshi, hatua ambayo ilipelekea wahudumu wa matatu kupoteza mapato ya kima cha Sh3 milioni.

“Tunapoteza biashara kwa sababu abiria wengi wamevutiwa na nauli ya chini inayolipishwa na gari moshi. Hii inatokana na hali kwamba Kenya imekumbatia soko huria,” akasema Mwenyekiti wa MOA, tawi la Mlima Kenya Michael Kariuki kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Jumatano.

“Hata hivyo, nauli inayotozwa inapasa kuwa ile ambayo inajali masilahi ya washindani wote katika sekta ya uchukuzi wa umma,” akaongeza.

Bw Kariuki alisema ajenda kuu ya mkutano huo, ambao hakubainisha utafanyika lini, ni kujadili namna ya kusawazisha nauli zinatozwa mbinu hizo mbili za usafiri.

Safari ya kwanza ya gari moshi kutoka Nairobi kwenda Nanyuki ilifanyika mnamo Desemba ambapo abiria 1,500 walilipa nauli ya Sh200 kwenda Nanyuki. Wale waliokuwa wakielekea vituo kama Murang’a na Nyeri walilipishwa nauli ya chini hata zaidi.

Masharti yaliyowekwa na serikali kudhibiti msambao wa virusi vya corona yameathiri pakubwa sekta ya uchukuzi wa umma. Hii ni kwa sababu magari ya uchukuzi yamelazimishwa kubeba abiria wachache ili kupunguza mtagusano kati ya wasafiri.

Kwa mfano matatu inayobeba abiria 14 imelazimika kubeba watu 8 na ile inayobeba abiria 35 ikilazimishwa kubeba watu 20 pekee. Pamoja na ongezeko la bei ya mafuta, hali hii imewaathiri zaidi wahudumu wa matatu na kupunguza faida yao kipindi hiki cha janga la corona.

Hata hivyo mnamo Oktoba 19, 2020, mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Matatu nchini Simon Kimutai alipuuzilia mbali madai kuwa kuanzishwa kwa huduma za uchukuzi wa gari moshi kutaathiri sekta ya matatu.

Mwenyekiti huyo alisema kuwa kile ambacho kinaipa sekta hiyo wasiwasi ni jinsi serikali kuu imeibagua sekta hiyo katika utekelezaji wa masharti ya kuzuia msambao wa Covid-19.

Bw Kimutai alisema serikali haikutenda haki kwa kuziruhusu ndege na magari moshi kubeba idadi kamili ya abiria huku ikilazimisha matatu kubeba asilimia 60 pekee ya idadi kamili ya abiria.

“Kile tunauliza ni haki. Kanuni ya umbali wa mita moja kati ya mtu mmoja na mwingine haipasi kutekelezwa katika sekta ya matatu pekee huku ndege na gari moshi zikiruhusiwa kubeba idadi kamili ya abiria,” akasema Bw Kimutai.

Habari zinazohusiana na hii