• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:10 PM
Mataifa 16 yathibitisha kushiriki tenisi za kimataifa jijini Nairobi

Mataifa 16 yathibitisha kushiriki tenisi za kimataifa jijini Nairobi

Na CHRIS ADUNGO

JUMLA ya mataifa 16 yamethibitisha kushiriki mapambano ya kimataifa ya tenisi kwa chipukizi almaarufu International Tennis Federation (ITF) World Junior Championship yatakayoandaliwa katika uwanja wa Nairobi Club kati ya Januari 18 na Februari 6, 2021.

Miongoni mwa nchi ambazo tayari zimepata idhini ya kuwakilishwa kwenye kipute hicho ni Uturuki, India, Ufaransa, Afrika Kusini, Amerika, Canada, Misri, Denmark, Italia, Uingereza na Ubelgiji.

Mataifa mengine yanayotazamiwa kuthibitisha ushiriki wao kufikia mwisho wa wikendi hii ni Bulgaria, Israel, Poland, Nepal, Russia, Uswisi, Ureno, Japan, Uswidi, Ujerumani, Korea Kusini, Tunisia, Austria, Finland, Zimbabwe, Pakistan na Slovakia.

Kinara wa Shirikisho la Tenisi la Kenya (TK), Nancy Nduku amesema mashindano hayo yataandaliwa chini ya uzingativu wa kanuni zilizotolewa na Wizara ya Michezo katika juhudi za kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

“Maandalizi yetu yameanza na droo rasmi ya kipute hicho itafanyika mwishoni mwa wiki ya pili ya mwezi huu Januari 2021. Tunatarajia mataifa zaidi kuthibitisha ushiriki wao kufikia mwisho wa Januari 3,” akasema Nduku.

Tenisi ni miongoni mwa fani mbalimbali za michezo zilizoidhinishwa na Wizara ya Michezo kurejelea shughuli za kawaida mnamo Novemba 2020 ingawa chini ya uzingativu wa masharti ya kudhibiti msambao wa ugonjwa wa Covid-19.

Tangu wakati huo, TK imefanikiwa kuandaa mashindano matatu kwa chipukizi na kategoria tofauti za kikosi cha watu wazima kwa minajili ya kujifua kwa mapambao yajayo ya kimataifa.

“Mashindano ambayo tumeshiriki hadi kufikia sasa yamewapa wanatenisi wetu jukwaa mwafaka la kujiweka sawa kwa kipute tukakachokiandaa mwaka huu. Tumefanya yote ambayo yanastahili kutenda na nina matumaini kwamba mapambano hayo ya kimataifa yatafana,” akasema Nduku katika kauli iliyoshadidiwa na Rais wa TK, James Kenani.

Kenya itawakilishwa na wanatenisi Rosehilda Asumwa, Alicia Owegi, Cynthia Cheruto na Faith Urasa katika kategoria ya wasichana huku Zayan Varani, Brian Nyakundi, Edward Mwakio, Sayush Bhandari, Daniel Mbuvi na Vincent Githinji wakiunga kikosi kitakachotegemewa kwa upande wa wavulana.

You can share this post!

Watumiaji mitandao ya kijamii wafurahia mvua siku ya kwanza...

Salah afichua azma ya kuwapungia Liverpool mkono wa kwaheri