• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
Salah afichua azma ya kuwapungia Liverpool mkono wa kwaheri

Salah afichua azma ya kuwapungia Liverpool mkono wa kwaheri

Na MASHIRIKA

KOCHA Jurgen Klopp wa Liverpool amefutilia mbali tetesi kwamba nyota Mohamed Salah hafurahii kabisa maisha yake mjini Merseyside na yuko radhi kuondoka uwanjani Anfield mwishoni mwa msimu huu wa 2020-21.

Katika mahojiano yake na gazeti la Mundo Deportivo la Uhispania mnamo Ijumaa, Salah, 28, alikiri kwamba alifadhaishwa na hatua ya Klopp kumnyima fursa ya kuvalia utepe wa unahodha katika mchuano wao wa mwisho wa makundi ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) dhidi ya FC Midtjylland ya Denmark.

Beki Trent-Alexander Arnold ndiye aliyeaminiwa ukapteni wakati wa gozi hilo lililoshuhudia Liverpool wakiambulia sare ya 1-1 ugenini.

Isitoshe, Salah ambaye ni raia wa Misri, alikiri kwamba huenda akashawishika kutua kambini mwa Real Madrid au Barcelona nchini Uhispania iwapo ataagana na Liverpool ambao kwa mujibu wake, “wameonekana kumpuuza katika michuano mingi ya msimu huu tangu ujio wa Diogo Jota kutoka Wolves”.

“Salah yuko katika hali thabiti kimawazo na kimwili. Anajivunia fomu nzuri na sioni lolote litakalochangia kuondoka kwake Liverpool hivi karibuni,” akasema Klopp.

Katika mechi ya mwisho akivalia jezi za Liverpool, Salah aliondolewa mapema dhidi ya Newcastle United waliowalazimishia sare tasa uwanjani St James’ Park.

Awali, alikuwa ametokea benchi dhidi ya Crystal Palace na kuongoza waajiri wake kusajili ushindi mnono wa 7-0 ugani Selhurst Park mnamo Disemba 19 kabla ya kuwaongoza waajiri wake kusajili sare ya 1-1 dhidi ya West Bromwich Albion mnamo Disemba 27 uwanjani Anfield.

Ushindi mnono dhidi ya Palace ulisaidia Liverpool kusherehekea Krismasi ya mwaka 2020 wakiwa kileleni mwa jedwali la EPL kwa msimu wa tatu mfululizo. Liverpool ambao ni mabingwa watetezi wa EPL walipitwa na Manchester City mnamo 2018-19 licha ya kudhibiti kilele cha jedwali kwa muda mrefu.

Salah kwa sasa anajivunia jumla ya mabao 13 kapuni mwake kutokana na mechi 16 za EPL hadi kufikia sasa muhula huu wa 2020-21.

You can share this post!

Mataifa 16 yathibitisha kushiriki tenisi za kimataifa...

Wanaraga wa Kenya Harlequins wamdumisha Benjamin Ayimba...