• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 10:50 AM
Kocha Pochettino kumsajili Dele Alli mwezi huu wa Januari akianza kudhibiti mikoba ya PSG

Kocha Pochettino kumsajili Dele Alli mwezi huu wa Januari akianza kudhibiti mikoba ya PSG

Na MASHIRIKA

KOCHA Mauricio Pochettino anatarajiwa kumfanya kiungo Dele Alli wa Tottenham Hotspur kuwa sajili wake wa kwanza kambini mwa Paris Saint-Germain (PSG).

Kwa mujibu wa magazeti mengi nchini Ufaransa, mkufunzi huyo wa zamani wa Spurs amepiga hatua kubwa katika mazungumzo yatakayomshuhudia akipokezwa mikoba ya PSG waliomtimua kocha Thomas Tuchel.

Pochettino ambaye ni raia wa Argentina, hajawahi kupata kikosi cha kumwajiri tangu afurushwe kambini mwa Spurs miezi 13 iliyopita.

Japo amekuwa akimezea mate fursa ya kudhibiti mikoba ya Manchester United, Pochettino yuko pua na mdomo kukitwaa chombo cha PSG ikizingatiwa ukubwa wa kiwango cha ufufuo wa Man-United chini ya Ole Gunnar Solskjaer katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita.

Mbali na kuwafanya Man-United kuwa wagombezi halisi wa taji la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu, Solskjaer amewaongoza waajiri wake kutinga nusu-fainali za Carabao Cup ambapo kwa sasa watakutana na Manchester City mwanzoni mwa mwezi huu wa Januari.

Kwa mujibu wa gazeti la L’Equipe, Pochettino anatarajiwa kutambulishwa rasmi kwa mashabiki na wachezaji wa PSG kufikia Jumatatu katika hatua itakayomshuhudia akirejea kufunza kikosi alichowahi kukichezea kati ya 2001 na 2003.

Kubwa zaidi katika maazimio yake ni kumshawishi Alli kuagana na Spurs na kutua PSG katika muhula mfupi ujao wa uhamisho wa wachezaji mwezi huu.

Ingawa Alli alikuwa na uhakika wa kuunga kikosi cha kwanza cha Spurs chini ya Pocheetino, sogora huyo raia wa Uingereza amekuwa akisugua benchi ya waajiri wake chini ya kocha Jose Mourinho.

Alli, 24, amepangwa katika kikosi cha kwanza cha Spurs mara tano pekee hadi kufikia sasa msimu huu na aliondolewa uwanjani baada ya dakika 56 pekee wakati wa mechi ya robo-fainali ya Carabao Cup dhidi Stoke City mwishoni mwa Disemba 2020.

Alli alilaumiwa pakubwa na Mourinho kwa bao lililofungwa na Stoke City kwenye mchuano huo.

“Mchezaji wa haiba na kiwango chake anastahili kuwa mbunifu na achangie mabao badala ya kuwa kiini cha matatizo ya kikosi chake,” akasema Mourinho.

Tuchel ambaye ni raia wa Ujerumani alipokezwa mikoba ya PSG mnamo Juni 2018 na akawaongoza waajiri wake kutia kapuni mataji mawili ya Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1), taji la French Cup na ubingwa wa French League Cup.

Chini ya ukufunzi wake, PSG walitinga pia fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 2019-20 ila wakazidiwa maarifa na Bayern Munich ya Ujerumani iliyowanyuka 1-0 kwenye fainali iliyochezewa jijini Lisbon, Ureno.

PSG kwa sasa wanashikilia nafasi ya tatu kwenye Ligue 1 kwa alama 35, moja nyuma ya viongozi Lille na Olympique Lyon.

Isitoshe, miamba hao wa soka ya Ufaransa wamefuzu tayari kwa hatua ya 16-bora ya UEFA msimu huu wa 2020-21 na watakutana na wapambe wa soka ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga), Barcelona.

Kutimuliwa kwa Tuchel, 47, kulijiri saa chache baada ya kuwaongoza PSG kupepeta Strasbourg 4-0 kwenye mechi ya Ligue 1 uwanjani Parc des Princes jijini Paris, Ufaransa mnamo Disemba 23. Mchuano huo ulikuwa wa nne kwa miamba hao kupoteza kutokana na 17 iliyopita msimu huu.

Ushindi huo uliwawezesha PSG kupunguza pengo la alama kati yao na viongozi wa jedwali Lille na Lyon hadi pointi moja pekee.

Hadi kutimuliwa kwake, mkataba kati ya PSG na Tuchel ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya Borussia Dortmund nchini Ujerumani, ulikuwa umepangiwa kutamatika rasmi mwishoni mwa kampeni za msimu huu.

Tuchel alijiunga na PSG mnamo Mei 2018 kwa mkataba wa miaka miwili baada ya kuaminiwa kuwa mrithi wa Mhispania Unai Emery aliyeyoyomea Arsenal. Alitia saini mkataba mpya wa mwaka mmoja na PSG mnamo Mei 2019.

You can share this post!

COVID-19: Manchester City kukosa masogora watano wa haiba...

Pochettino kushawishi PSG kurefusha mikataba ya Neymar na...