• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
JAMVI: Mikosi ya usaliti kwa miungano ya kisiasa uchaguzi mkuu unapobisha

JAMVI: Mikosi ya usaliti kwa miungano ya kisiasa uchaguzi mkuu unapobisha

Na WANDERI KAMAU

UCHAGUZI Mkuu wa 2022 unapozidi kukaribia, macho yote yatakuwa kwa miungano ya kisiasa inayoendelea kubuniwa nchini, kuhusu ikiwa itahimili mtihani wa kubaki pamoja.

Hili ni ikizingatiwa miungano mingi huwa ni uzao wa usaliti kati ya wanasiasa wenyewe.

Wadadisi wa siasa wanasema kuwa hali ilivyo kwa sasa, huenda kivumbi cha urais kikawa kati ya Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga 2022, ingawa Bw Odinga hajatangaza wazi ikiwa atawania nafasi hiyo.

Hivyo, wanasema miungano itakayobuniwa itawakilisha mwelekeo wa kisiasa kati ya vigogo hao wawili.

Kufikia sasa, mrengo wa Dkt Ruto unaendelea kubuni taswira yake, hasa baada ya kuibuka mshindi kwenye uchaguzi mdogo wa eneobunge la Msambweni (Kaunti ya Kwale) na wadi kadhaa katika ukanda wa Mlima Kenya.

Dkt Ruto amekuwa akiendesha kampeni yake chini ya kaulimbiu ya ‘Hustler Nation’ (Watu Maskini), kupitia kundi la ‘Tangatanga.’

Naye Bw Odinga anaonekana kuendeleza nia yake kichinichini kupitia mchakato wa ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI), ambayo amekuwa akiipigia debe akiwarai Wakenya kuiunga mkono.

Licha ya kutoweka nia yake ya kuwania urais wazi, wadadisi wengi wanafasiri kuwa Bw Odinga anaendeleza nia yake kupitia ripoti hiyo, kwani mojawapo ya mapendekezo yaliyopo ni kubuniwa kwa nyadhifa zaidi za kisiasa katika serikali

Ripoti inapendekeza kubuniwa kwa nafasi ya Waziri Mkuu na manaibu wake wawili, kando na uwepo wa Rais na Naibu Rais.

Ni pendekezo linalotajwa kubuni uhasama mkubwa wa kisiasa kati ya Dkt Ruto na Bw Odinga.

“Pendekezo hilo limebuni mpaka mkubwa wa kisiasa kati ya wawili hao, hali inayotuzalia miungano mikuu miwili ielekeapo 2022. Swali ni; itahimili wimbi la usaliti? Hicho ndicho kitakuwa kibarua kigumu kwa wanasiasa hao wawili na yeyote mwingine atakayejitokeza kuwania urais,” asema Bw Javas Bigambo, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Kulingana na Bw Bigambo, kibarua hicho kinatokana na uhalisia wa miungano ya kisiasa nchini, kwani mingi huwa haidumu na huvunjika mara tu baada ya uchaguzi ama wanasiasa walioibuni wanapokosana.

Tayari, wanasiasa ambao wameonyesha nia ya kuungana na Bw Odinga ni Peter Kenneth, aliyekuwa gavana wa Bomet Isaac Ruto, Seneta Gideon Moi (Baringo) kati ya wengine.

Muungano wa tatu pia unaonekana kuwa kati ya Kiongozi wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi (Amani National Congress), Seneta Moses Wetang’ula (Ford-Kenya) na Gavana Charity Ngilu (Kitui).

Wiki iliyopita, wanne wao walifanya kikao katika mkahawa moja katika Kaunti ya Machakos, ambapo walikubaliana kufanya kazi pamoja “ili kutimiza ndoto ya kuikomboa Kenya.”

“Tumeanza safari ya ukombozi kamili wa kisiasa. Tutatembea pamoja. Hili si wazo la hivi hivi tu. Tumeshirikiana na kutembea pamoja hapo awali. Hii haitakuwa mara ya kwanza,” akasema Bw Wetang’ula.

Bi Ngilu aliwarai viongozi hao kudumisha umoja, akisema hakuna anayeweza kutimiza malengo yake kisiasa bila kushirikiana na wenzake.

Licha ya hakikisho hizo, wadadisi wanasema kitakuwa kibarua kigumu kwa wanasiasa hao wote kudumisha umoja, kwani wote ni waathiriwa wa usaliti wa kisiasa kwa njia moja ama nyingine.

“Uzao wa handisheki, ambao ni ushirikiano wa Rais Kenyatta na Bw Odinga, ni hisia za kusalitiwa kwa Dkt Ruto na washirika wake. Hilo ndilo limechangia kusambaratika kwa Chama cha Jubilee (JP) na ushirikiano kati ya Rais Kenyatta na naibu wake. Ujio wa handisheki ndio ulivunja Jubilee, ambayo ilibuniwa mnamo 2012,” asema Bw Wycliffe Muga, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Anarejelea mifano mingine kama sababu za kubuniwa kwa chama cha FORD (Forum for the Restoration of Democracy) katika miaka ya tisini.

Anasema usaliti wa kisiasa katika Kanu na marehemu Daniel Moi ndio uliowafanya wanasiasa kama Rais Mstaafu Mwai Kibaki, marehemu Jaramogi Oginga Odinga, Stanley Matiba kati ya wengine kuondoka katika Kanu na kubuni FORD.

Vile vile, anasema usaliti huo ulidhihirika mnamo 2002, ambapo kwa mara nyingine, wanasiasa kadhaa waliondoka Kanu na kubuni chama cha Liberal Democratic Party (LDP) baada ya kuhisi kusalitiwa na Bw Moi.

Hilo ni baada ya Bw Moi kumteua Rais Kenyatta kama mgombea urais kwa tiketi ya Kanu.

Wanasiasa hao walijumuisha Bw Odinga, marehemu William Ole Ntimama, George Saitoti, Joseph Kamotho kati ya wengine.

Usaliti huo pia ulidhihirika kati ya 2003 na 2005, baada ya Bw Kibaki kukosana na Bw Odinga kufuatia mkataba wa kisiasa (MoU) ambapo Bw Odinga angehudumu kama Waziri Mkuu. Uzao wa ‘usaliti’ huo ulikuwa hatua ya Bw Odinga na wenzake kubuni chama cha ODM.

Wanasema mwaka huu utakuwa wakati muhimu wa kutathmini ikiwa miungano hiyo itadumu ama itasombwa na mawimbi ya kisiasa yatakayoibuka upya.

You can share this post!

JAMVI: Uhuru alivyosagasaga Sonko, Waititu kisiasa

TAHARIRI: Msimamo wa Cotu ni machozi ya mamba