• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Baadhi ya wazee wa jamii ya Talai ni wakora – Kinara

Baadhi ya wazee wa jamii ya Talai ni wakora – Kinara

ONYANGO K’ONYANGO na TOM MATOKE

IMEFICHUKA kwamba migawanyiko inayoendelea kushuhudiwa ndani ya ukoo mmoja ambao umekuwa ukitawaza viongozi wakuu nchini wakiwemo marais wanne, unachochewa na maslahi ya kifedha.

Ukoo wa Talai unaopatikana katika eneo la Kapsisiywa, Kaunti ya Nandi na Kaunti za Kericho, Bomet na Trans Nzoia, umegawanyika kuhusu namna shughuli hiyo ya kitamaduni inavyopaswa kuendeshwa huku maslahi ya kisiasa na kibinafsi yakiibuka miongoni mwa viongozi wake.

Watu wa ukoo huo ni wa kizazi cha aliyekuwa kiongozi wa Wanandi, jagina Koitalel arap Samoei na mwanawe Barsirian arap Manyei.

Wamegawanyika katika koo tano ndogo – Kapturgat, Kapchesang, Kapsonet, Kapsogon na Kapmamursoi.

Lakini ukoo mdogo wa Kapturgat anaotoka naibu mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Talai, Christopher Koyogi, unadai kuwa na kipawa cha utawazaji.

Mwaka jana, Mzee Koyogi alipokonywa wadhifa huo kwa kupinga kutawazwa kwa Naibu Rais William Ruto kama msemaji wa kisiasa wa jamii ya Wakalenjin. Madai ya ukoo huo yameibua pingamizi kutoka kwa watu kutoka koo nyingine nne na baadhi ya wanachama wa baraza la wazee wa Talai.

Inadaiwa kuwa Arap Manyei, alimtawaza mwanzilishi wa taifa la Kenya Hayati Mzee Jomo Kenyatta na kumkabithi vifaa vya uongozi kama vile Sambut miongoni mwa vingine.

Marais wengine wa zamani kama vile marehemu Daniel Toroitich arap Moi, rais mstaafu Mwai Kibaki na Rais Uhuru Kenyatta pia walipokea baraka na utawazo kutoka kwa ukoo huu.

Viongozi wengine kama vile Dkt Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga wamesaka baraka kutoka kwa ukoo huu na hivyo kuupa hadhi na heshima kuu katika ngazi za kisiasa na kitamaduni

Mwenyekiti wa baraza hilo ambaye aliongoza hafla ya kumtawaza Dkt Ruto, alfajiri ya Juni 5, 2020, Kasisi James Bassy, Jumanne aliusuta mrengo pinzani kwa kutumia vibaya ‘kipawa’ cha ukoo huo kwa manufaa ya kifedha.

Alisema hiyo ni kinyume cha sheria na kanuni za ukoo mzima wa Talai.

Akiongea jana katika kijiji cha Kapsisiywa, Bw Bassy alitetea kutawazwa kwa Naibu Rais Dkt Ruto, akisema hatua hiyo iliungwa mkono na mbari zote tano za ukoo huo.

Kuhusu hafla iliyotibuka ya kumtawaza Seneta wa Baringo, Bw Gideon Moi, iliyopangwa na Bw Koyogi, Bw Bassy alikariri kuwa jamii hiyo haitaruhusi shughuli yoyote kama hiyo kuendeshwa hapo Kapsisiywa na mzee yeyote wa Talai.

Alisema baada ya mtu mmoja kutawazwa, kanuni yao hairuhusu mtu mwingine kutunukiwa heshima kama hiyo tena.

“Tunamheshimu zaidi Gideon kwa sababu ni mtoto wa Rais aliyetuongoza tangu mwaka wa 1956. Hatuna chuki zozote za kibinafsi dhidi yake. Lakini hatuwezi kumtawaza mtu mwingine hata kama ni Gideon kwa sababu hapo tutakuwa tukijidanganya,” akasema Bw Bassy.

“Tulipomtawaza Naibu Rais Dkt Ruto mnamo Juni 5, mwaka jana, hatukuwa pekee yetu. Tuliandamana na watu kutoka jamii ya Nandi na ukoo wa Talai, Gavana Stephen Sang’ na wabunge; Julius Meli (Tinderet), Cornelly Serem (Aldai) na Wilson Kogo (Chesumei). Vile vile, walihudhuria zaidi ya viongozi 20 wa kidini na wawakilishi kutoka kwa koo tano ndogo ya ukoo wa Talai,” akaeleza.

You can share this post!

Wataalam watarajiwa China kuchunguza kiini cha corona

BI TAIFA JANUARI 6, 2021