• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 3:03 PM
Arsenal wamsajili chipukizi matata Omar Rekik kutoka Hertha Berlin ya Ujerumani

Arsenal wamsajili chipukizi matata Omar Rekik kutoka Hertha Berlin ya Ujerumani

Na MASHIRIKA

ARSENAL wamethibitisha kumsajili tineja Omar Rekik kutoka kambini mwa Hertha Berlin nchini Ujerumani.

Kinda huyo mwenye umri wa miaka 19 ndiye sajili wa kwanza wa Arsenal katika mwaka huu wa 2021. Rekik alirasimisha uhamisho wake hadi Arsenal kwa kima cha Sh76 milioni.

Arsenal walikuwa pua na mdomo kumsajili Rekik mwanzoni mwa msimu huu ila wakashindwa kuwahi makataa ya Hertha Berlin kufikia siku ya mwisho ya uhamisho wa wachezaji katika Ligi Kuu za Uingereza na Ujerumani mnamo Oktoba 5, 2020.

“Rekik ametia saini mkataba wa kitaaluma na Arsenal na atatarajiwa kuchezea mwanzo kikosi cha chipukizi wasiozidi umri wa miaka 23 kabla ya kuanza kupangwa katika kikosi cha kwanza cha watu wazima,” ikasema sehemu ya taarifa ya Arsenal.

Rekik alizaliwa Uholanzi na amewahi kuchezea timu ya chipukizi nchini Tunisia na Uholanzi. Amewahi pia kuvalia jezi za Feyenoord, Manchester City, PSV Eindhoven na Olympique Marseille.

Akivalia jezi za Hertha Berlin msimu huu, Rekik aliwajibishwa na waajiri wake mara nane katika Ligi ya Daraja la Nne na kwa sasa atakuwa chini ya uangalizi wa Per Mertesacker ambaye ni kocha wa makinda wa Arsenal. Mertesacker ndiye alichangia pakubwa uhamisho Rekik hadi ugani Emirates.

Arsenal wamefichua azma ya kupunguza idadi kubwa ya wachezaji wao. Kikosi hicho kinalenga kwa sasa kuagana mabeki Sokratis Papastathopoulos na Shkodran Mustafi baada ya Sead Kolasinc kutumwa Schalke kwa mkopo huku William Saliba akitua kambini mwa Nice nchini Ufaransa.

  • Tags

You can share this post!

UDA chajiuza kama chama kisichobagua Mkenya yeyote

BI TAIFA JANUARI 8, 2021