Serikali yatoa hela za ujenzi wa shule zilizoathiriwa na mafuriko

Na WAANDISHI WETU

SERIKALI imetoa pesa za kufadhili ujenzi wa shule ambazo ziliharibiwa na mafuriko katika kaunti nne kufuati mvua kubwa iliyoshuhudiwa maeneo mbalimbali nchini mwanzoni mwa mwaka huu wa 2021.

Kwingineko, wanafunzi 10,000 kutoka shule za kibinafsi wamehamishwa hadi shule za umma kufuatia makali ya kiuchumi yaliyosababishwa na janga la Covid- 19.

Kuhusu shule zitakazokarabatiwa, waziri wa elimu George Magoha alisema shule zitakazofaidi ni zile zinazopatikana katika kaunti za Baringo, Kisumu, Elgeyo Marakwet na Pokot Magharibi.

Aliwataka walimu wakuu na bodi za usimamizi za shule husika kutumia pesa hizo kwa njia nzuri ili zifaidi wanafunzi.

Akiongea katika shule ya upili ya Ombaka katika eneobunge la Nyando, Ijumaa, Profesa Magoha alisema wizara yake itahakikisha kuwa masomo yanaendelea katika mazingira bora na salama.

Wanafunzi wa shule hiyo iliyoathirika na mafuriko sasa wanasomea kwenye mahema katika shule jirani ya Msingi ya Ombaka.

Serikali pia imeipa Shule ya Upili ya Kandaria Sh10 milioni huku shule za msingi za Ogenya na Kandaria zikipokea Sh4 milioni kila moja kufadhili ujenzi wa madarasa na miundomsingi mingine.

Kwa mara nyingine Profesa Magoha alionya kuwa wizara yake itawachukulia hatua kali walimu wakuu wa shule za umma ambao watawarejesha nyumbani wanafunzi kwa sababu ya kutolipa karo.

Hata hivyo, waziri aliwataka wazazi ambao hawawezi kumudu kulipa karo wakati huu kujadiliana na walimu wakuu ili wakubaliane kuhusu ni lini wataweza kulipa karo hitajika.

Katika kaunti ya Kisii Katibu wa Wizara ya Afya Susan Mochache alisema kuwa angalau wanafunzi 123 wa Shule ya Msingi ya KARI hawajaripoti shuleni, siku nne baada ya shule kufunguliwa.

Habari zinazohusiana na hii

Hakuna kupumua shuleni

Waziri mtatanishi