• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:55 AM
Gor Mahia wapewa Napsa Stars ya Zambia kwenye mchujo wa Kombe la Mashirikisho barani Afrika

Gor Mahia wapewa Napsa Stars ya Zambia kwenye mchujo wa Kombe la Mashirikisho barani Afrika

Na CHRIS ADUNGO

MIAMBA wa soka ya Kenya, Gor Mahia, watavaana na Napsa Stars ya Ligi Kuu ya Zambia (ZSL) kwenye mchujo wa kufuzu kwa hatua ya makundi ya Kombe la Mashirikisho barani Afrika (CAF Confederation Cup) mwaka huu wa 2021.

Hii ni kwa mujibu wa droo iliyofanywa Januari 8, 2021, katika makao makuu ya Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) jijini Cairo, Misri.

Gor Mahia almaarufu K’Ogalo watakuwa wenyeji wa mkondo wa kwanza utakaondaliwa jijini Nairobi mnamo Februari 14 kabla ya mchuano wa mkondo wa pili kuandaliwa jijini Lusaka mnamo Februari 21, 2021.

K’Ogalo walishuka ngazi kuwania taji la Kombe la Mashirikisho baada ya kudenguliwa na CR Belouizdad ya Algeria kwenye mashindano ya Klabu Bingwa barani Afrika (CAF Champions League) kwa jumla ya mabao 8-1.

Awali, walikuwa wamedengua APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 4-3 kwenye raundi ya kwanza ya mchujo wa Champions League.

Chini ya kocha mshikilizi Sammy ‘Pamzo’ Omollo, Gor Mahia walipokezwa kichapo cha 6-0 katika mkondo wa kwanza jijini Algiers mnamo Disemba 26, 2020 kabla ya kupigwa 2-1 kwenye marudiano yaliyofanyika ugani Nyayo, Nairobi mnamo Januari 5, 2021.

Kwa upande wao, Napsa Stars walifuzu kwa hatua ya mchujo wa Kombe la Mashirikisho kwa kanuni ya bao la ugenini baada ya kuambulia sare ya 1-1 dhidi ya UD Songo ya Msumbiji.

Kati ya Wakenya wanaosakatia Napsa Stars ni Shaban Odhoji, Andrew Tololwa na Timothy Otieno.

Gor Mahia wamekuwa na historia ya kusajili matokeo mseto kwenye kampeni za Kombe la Mashirikisho katika kipindi cha misimu mitatu iliyopita.

Mnamo 2018, Gor Mahia walitinga hatua ya makundi ya Kombe la Mashirikisho ila wakashindwa kufuzu kwa robo-fainali baada ya kuambulia nafasi ya tatu kwenye kundi lililowajumuisha pia Rayon Sports ya Rwanda, Yanga SC ya Tanzania na USM Alger ya Algeria waliomaliza kileleni mwa jedwali mbele ya Rayon.

Matokeo ya Gor Mahia kwenye Kombe la Mashirikisho yaliimarika katika mwaka wa 2019 baada ya kutinga hatua ya robo-fainali baada ya kuambulia nafasi ya pili kundini nyuma ya Zamalek SC ya Misri. Kundi hilo lilijumuisha pia NA Hussein Dey ya Algeria na Petro Atletico de Luanda inayoshiriki Ligi Kuu ya Angola.

Ufanisi huo wa Gor Mahia uliwapa tiketi ya kuvaana na mabingwa watetezi RS Berkane kutoka Morocco kwenye hatua ya nane-bora na wakapokezwa kichapo cha jumla ya mabao 7-1 baada ya kupepetwa 2-0 nyumbani kisha kupondwa 5-1 ugenini.

Masaibu ya Gor Mahia katika msimu wa 2020 yalizidi baada ya kudenguliwa na DC Montema Pembe ya DR Congo kwenye mchujo. Kichapo cha 2-1 ugenini baada ya sare ya 1-1 nyumbani kiliwezesha DC Montema kunyima Gor Mahia fursa ya kusonga mbele kwa hatua ya makundi.

Safari ya Gor Mahia kwenye Champions League mnamo 2018 ilianza kwa ushindi dhidi ya Nyasa Big Bullets ya Malawi. Katika mkondo wa kwanza, walisajili ushindi wa 1-0 uwanjani Kasarani kabla ya Big Bullets kusajili matokeo sawa na hayo wakati wa marudiano.

Mshindi wa mechi hiyo aliamuliwa kupitia mikwaju ya penalti ambapo kipa Boniface Oluoch alipangua makombora mawili na kusaidia Gor Mahia kuibuka na ushindi wa 4-3.

Matumaini ya Gor Mahia kusonga mbele kwenye Champions League mnamo Disemba 2018 yalizimwa ghafla na Lobi Stars ya Nigeria waliowapiga 2-0 kwenye mchuano wa raundi ya pili ya mchujo.

Austin Ogunye na Alimi Sikiru walifungia Lobi Stars katika mechi ya marudiano baada ya Gor Mahia kusajili ushindi wa 3-1 nyumbani wakati wa mechi ya mkondo wa kwanza.

Kwa mara nyingine, Gor Mahia walishuka ngazi hadi mechi za Confederation Cup na wakapangwa pamoja na New Star de Doula ya Cameroon kwenye mchujo.

Baada ya kushinda 2-1 nyumbani, walilazimisha sare tasa jijini Doula na wakafuzu kwa hatua ya makundi. Katika Kundi D, walipigwa 2-1 ugenini na Petro Atletico, 1-0 na NA Hussein Dey na 4-0 dhidi ya SC Zamalek.

Hata hivyo, walifaulu kufuzu kwa robo-fainali baada ya kupepeta Zamalek 4-2, Hussein Dey 2-0 na Petro Atletico 1-0 nyumbani. Licha ya kusonga mbele, Gor Mahia walipokezwa kichapo cha mabao 5-1 ugenini na Renaissance Sportive de Berkane ya Morocco waliowacharaza 2-0 nyumbani.

Mnamo 2019-20, Gor Mahia waliwapepeta Aigle Noir ya Burundi 5-1 nyumbani baada ya kuambulia sare tasa ugenini jijini Bujumbura.

DROO YA KOMBE LA MASHIRIKISHO LA CAF:

Gor Mahia (Kenya) na Napsa Stars (Zambia)

Enyimba (Nigeria) na Bloemfontein Celtic (Afrika Kusini) au Rivers Utd (Nigeria)

Platinum (Zimbabwe) na Jaraaf (Senegal)

Raja Casablanca (Morocco) na US Monastir (Tunisia)

Asante Kotoko (Ghana) na Entente Setif (Algeria)

SONIDEP (Niger) na Coton Sport (Cameroon)

Stade Malien (Mali) na JS Kabylie (Algeria)

Jwaneng Galaxy (Botswana) na Orlando Pirates (Afrika Kusini)

Primeiro Agosto (Angola) na Namungo (Tanzania)

CS Sfaxien (Tunisia) na AS Kigali (Rwanda)

Nkana (Zambia) na Tihad Casablanca (Morocco)

Bouenguidi (Gabon) na Salitas (Burundi)

Young Buffaloes (Swaziland) na Etoile Sahel (Tunisia)

Al Ahly Benghazi (Libywa) na DC Motema Pembe (DR Congo)

RC Abidjan (Ivory Coast) na Pyramids (Misri)

You can share this post!

Elijah Manangoi apigwa marufuku ya miaka miwili kwa hatia...

Leicester kukosa huduma za Vardy na Maddison kwenye mechi...