• Nairobi
  • Last Updated December 5th, 2023 10:25 PM
Leicester kukosa huduma za Vardy na Maddison kwenye mechi ya Kombe la FA dhidi ya Stoke City

Leicester kukosa huduma za Vardy na Maddison kwenye mechi ya Kombe la FA dhidi ya Stoke City

Na MASHIRIKA

LEICESTER City watakosa huduma za fowadi Jamie Vardy na kiungo James Maddison katika mechi ya raundi ya tatu ya Kombe la FA itakayowakutanisha na Stoke City leo Jumamosi.

Vardy alipata jeraha la paja huku Maddison akiumia goti katika mchuano wao wa awali uliowashuhudia wakipepeta Newcastle United 2-1 kwenye gozi la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Hata hivyo, afueni kubwa kwa Leicester ni marejeo ya beki raia wa Uturuki, Caglar Soyuncu aliyewajibishwa kwa dakika chache za mwisho dhidi ya Newcastle wikendi iliyopita uwanjani St James Park.

Kwa upande wao, Stoke wanaoshiriki Ligi ya Daraja la Pili nchini Uingereza, watakuwa bila mshambuliaji Steven Fletcher.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 33 anauguza jeraha la kinena alilolipata baada ya kuanguka vibaya wakati wa mechi iliyokamilika kwa wao kupokezwa kichapo cha 1-0 kutoka kwa Bournemouth wikendi iliyopita.

Chini ya kocha Michael O’Neill, Stoke almaarufu ‘The Potters’ tayari wanakosa maarifa ya washambuliaji Tyrese Campbell (goti) na Lee Gregory (kinena).

Aidha, kipa Angus Gunn angali mkekani kwa pamoja na mabeki Adam Davies na Morgan Fox wanaouguza majeraha ya mapaja.

Stoke waliwahi kukutana na Leicester kwenye raundi ya tatu ya Kombe la FA mnamo 2013-14 na wakasajili ushindi wa 2-1 chini ya mkufunzi Mark Hughes.

Mechi zote tatu za mwisho kati ya Stoke na Leicester uwanjani bet365 Stadium zilikamilika kwa sare ya 2-2 na zote zilikuwa za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na zilisakatwa kati ya Septemba 2015 na Novemba 2017.

You can share this post!

Gor Mahia wapewa Napsa Stars ya Zambia kwenye mchujo wa...

COVID-19: Tuzo za washindi wa Kombe la FA zapunguzwa kwa...