• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 10:15 AM
SAMMY WAWERU: Visa vya askari kujiua na kuangamiza wenzao vichunguzwe

SAMMY WAWERU: Visa vya askari kujiua na kuangamiza wenzao vichunguzwe

Na SAMMY WAWERU

KATIKA siku za hivi karibuni visa vya askari kujiua kwa silaha wanazotumia kuimarisha usalama na pia kuangamiza wenzao vimeonekana kuongezeka.

Mauaji ya kinyama miongoni mwao yameongezeka kwa kasi, suala ambalo linazua wasiwasi kuhusu usalama wa raia.

Kisa cha hivi punde ni cha afisa mmoja wa kituo cha polisi cha Kamukunji, Nairobi aliyemmiminia mwenzake wa kike risasi, mnamo Januari 4, 2021, akimuacha kupigania nafsi yake.

Mwathiriwa, Mourine Achieng hata hivyo alitangazwa kukata roho alipofikishwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH), kupata matibabu ya dharura.

Afisa aliyekuwa na askari huyo wa kike pia anasemekana kuuguza majeraha ya risasi. Mshukiwa wa mauaji hayo, Lawrence Ewoi anasemekana alijiua kwa kujipiga risasi katika oparesheni ya maafisa wa polisi kumkamata.

Kisa sawa na cha Kamukunji kilishuhudiwa katika Kaunti ya Kirinyaga, ambapo afisa wa kiume aliripotiwa kumuua mwenzake, kisha akajiua.

Matukio hayo hayakuwa mageni 2020 na miaka ya awali. Ni matukio ambayo yanazidi kushuhudiwa mwaka huu wa 2021 ukiwa ungali mchanga.

Visa vya kikatili vya aina hiyo vinazua maswali chungu nzima, kitendawili kikiwa: “Wanaotulinda wakigeuka kuwa wanyama kati yao, raia wana uhakika wa usalama wao kweli?”

Askari ni binadamu, kama anavyokariri mara kwa mara Sammy Ondimu Ngare, ambaye ni afisa wa kikosi cha askari tawala, AP na ambaye amekuwa katika mstari wa mbele kuimarisha uhusiano kati ya polisi na raia, katika utendakazi wake.

Huku afisa huyo akitumia mitandao ya kijamii, hasa Facebook kuendesha kampeni ya uhusiano mwema kati ya polisi na raia, pia ni mwimbaji wa nyimbo za injili.

Kwenye ukurasa wake, amekuwa akikashifu maafisa watundu na watovu wa nidhamu na maadili wanaofichuliwa kwa kudhulumu raia.

Inaaminika kiazi kimoja kikioza ni harabu ya vyote, na kulingana na Ondimu kuna maafisa kadha waadilifu na wanaothamini utendakazi wao.

“Hali si shwari, chini ya siku mbili pekee tumewapoteza askari wawili…” @Ondimu akachapisha mnamo Januari 4, 2021.

Kwa hakika, visa vya askari kujiangamiza na kuangamiza wenzao ni vya kusikitisha na vinavyoibua maswali. Huenda baadhi ya maafisa wetu wana matatizo ya ‘kiakili na kimaisha’ na yanayopaswa kuangaziwa.

Mambo yasipuuzwe ni shwari, maafisa pia ni wazazi, ndugu na wana jamaa wanaowategemea kuwakidhi riziki na mahitaji mengine muhimu ya kimsingi.

Licha ya idara ya polisi kutajwa kuwa miongoni mwa zile fisadi zaidi nchini, himizo kwa Inspekta Mkuu wa Polisi, IG Hillary Mutyambai kuchukulia kwa uzito suala la maafisa wake kujitia kitanzi.

Pengine, abuni afisi au kitengo maalum kitakachojukumika kutoa mafunzo na ushauri nasaha kwa maafisa wa polisi mara kwa mara.

Wazo hili linapaswa kuambatana na mabadiliko yanayoendelea kutekelezwa katika idara hiyo.

You can share this post!

Museveni kifua mbele Bobi Wine akipinga matokeo ya mapema

IEBC haina nia ya kuhujumu BBI – Chebukati