• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Nimeshinda urais kwa kura nyingi mno – Bobi Wine

Nimeshinda urais kwa kura nyingi mno – Bobi Wine

AFP na CHARLES WASONGA

MGOMBEAJI wa urais nchini Uganda kwa tiketi ya Muungano wa Upinzani Bobi Wine Ijumaa alidai kuwa mshindi katika kinyang’anyiro cha urais huku akipinga matokeo ya awali yalioonyesha Rais Yoweri Museveni alikuwa kifua mbele.

Mwanasiasa huyo alitaja matokeo yalioonyesha Museveni kupata asilimia 63 ya kura zilizohesabiwa kama “mzaha”.

Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 38 ambaye pia ni mwanamuziki, amekuwa mpinzani mkuu wa kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 79 katika uchaguzi wa urais ulioshirikisha wagombeaji wengine 10.

Museveni amekuwa Rais wa Uganda kwa miaka 35 baada ya kuingia mamlakani kupitia mapinduzi ya kijeshi mnamo 1986, na anapania kuongoza kwa muhula wa sita.

“Niko na imani kwamba tumemshinda dikteta huyo kwa kura nyingi. Natoa wito wa raia wa Uganda kukataa vitisho hivyo. Ukweli ni kwamba tumeshinda uchaguzi huu na tumeshinda kwa kura nyingi mno,” akawaambia wanahabari.

“Raia wa Uganda walipiga kura kwa wingi kubadilisha uongozi kutoka udikteta hadi uongozi wa kidemokrasia. Lakini Museveni anajaribu kutoa dhana kwamba anaongoza. Mzaha ulioje jamani!” akaongeza Bw Wine

Kulingana na matokeo hayo ya awali yaliyokuwa yametangazwa na Tume ya Uchaguzi Uganda (UEC) Bobi Wine alikuwa na asilimia 28 pekee za kura za urais zilizokuwa zimehesabiwa.

Mawasiliano na intaneti yalikuwa chini Uganda kuanzia Alhamisi kura zilipopigwa na shughuli ya kuhesabu kura kuanza baada ya vituo vya kupigia kura kufungwa kuanzia saa kumi na moja jioni.

You can share this post!

Jinsi ya kuandaa burger ya nyama ya ng’ombe

Bobi Wine asema majeshi yameteka nyumba yake, serikali...