• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 1:15 PM
DINI: Fursa hubisha hodi mara moja, ikumbatie

DINI: Fursa hubisha hodi mara moja, ikumbatie

NA PADRE FAUSTIN KAMUGISHA

Fursa haiji ikipigiwa ving’ora. “Fursa ni ngumu kutambuliwa; kwa kawaida tunaitegemea kutushtua kwa milio na mabango ya matangazo,” alisema William Arthur Ward.

Fursa haiji ikinguruma. Fursa haina honi wala kipaza sauti. Vile vile, haina mwanga mkali wa kushtua. Mpendwa msomaji, huna budi kutafakari sana au kufikiria sana kuigundua fursa.

“Tunapoacha kufikiria, mara nyingi tunapoteza fursa,” alisema Publilius Syrus, mwandishi kwa kutumia lugha ya Kilatini aliyezaliwa Syria (85-43 K.K) na kupelekwa Italia kama mtumwa.

Kufikiri ni kuwaza kwa kutumia akili ili kuelewa kitu. Kufikiri ni kutafakari. Kufikiri ni kutilia maanani.Kwa Kigiriki, fursa ni Kairos. Ni wakati muafaka au sahihi wa kufanya jambo fulani. Yesu alisema, “Wakati umefika” (Marko 1:14).

Ni wakati wa kutenda. Ni wakati wa kubadilika. Ni wakati wa kugutuka kutoka usingizini. “Saa ya kuamka katika usingizi imewadia” (Warumi 13:11). Fursa ni saa ya kuamka kutoka usingizini.

“Siku inayopambazuka ni siku ile tu tunapokuwa tumeamka,” alisema Henry David Thoreau (1817-1862), mwanafalsafa wa Amerika. Watu wanapochangamkia fursa mara nyingi husema, “tulikuwa tumelala.” Utasikia watu wanasema, “Afrika ni jitu kubwa sana lililolala.”

Wanamaanisha kuna fursa ambazo waafrika hawajazichangamkia. Kama huzioni, fursa ni kama umelala. Kama huchangamkii fursa, uko usingizini. Utapitwa na mambo mazuri kama kuku anavyopitwa na mende mdomoni wakati wa giza.

Kwa Kiingereza, fursa ni “opportunity.” Hilo neno linatokana na maneno ya Kilatini “ob portum veniens” yaani kuelekea kwenye bandari. Maneno hayo yanarejea kwenye upepo pendwa unaoisukuma meli kuelekea kwenye bandari. Fursa ni upepo pendwa. Maji ya bahari yanakupwa na kujaa.

Wakati wa kupwa meli zinakuwa hazijatia nanga bandarini zinakuwa karibu mabaharia wakingoja maji kujaa. Shakespeare aliandika katika kitabu chake Julius Caesar, “Kuna kupwa na kujaa katika maisha ya watu, fursa hiyo inapotumiwa wakati wa mafuriko, inakuelekeza kwenye bahati; isipotumiwa safari zote katika bahari ya maisha inaishia kwenye maji mafupi na matatizo chungu nzima.”

Fursa ile ile inawaacha baadhi ya watu wamefanikiwa kwa kuitumia vizuri na wengine inawaacha wameshindwa.Kwa lugha ya Kihaya, lugha ya wahaya wa Tanzania, fursa ni obushango au akashango.

Jambo ambalo linatokea pasipokutarajiwa. Kwa msingi huo, wahaya wana methali isemayo, “Kidondokacho hakina miadi (Ekigwa tikiraga).” Kwa msingi huo, kuna msemo husemao, “Kunguru huruka amefungua kinywa.”

Fursa ya chakula inaweza ikajitokeza pasipo kutarajiwa, ijitokezapo kinywa kiwe kimefunguliwa kupokea chakula. Hapa tunajifunza kuwa bahati ni maandalizi yanapokutana na fursa. Jiendeleze kimasomo hili fursa ya ajira ijapo uwe umejiandaa kimasomo. Weka akiba ili fursa ya biashara ijitokezapo uwe na mtaji.

Kuwa na hati ya ardhi ili fursa ya kukopa ijitokezapo uwe na hati.Fursa huonekana ni ndogo wakati inakuja na kuonekana kubwa wakati inatoweka. Ichangamkie.

Wagiriki walikuwa na sanamu ya muungu wa fursa. Sanamu hiyo ilikuwa na nywele nyingi kwenye paji na uso. Nyuma ya kichwa hapakuwepo nywele bali kipara.

Kuonesha kuwa fursa ikitokea ivute kwako ikishaondoka hauipati tena. Kupoteza fursa ambayo ingebadili maisha yako ni jambo baya sana.Fursa zipo katika mambo ambayo yanaonekana ni balaa.

“Katikati ya jambo gumu kuna fursa,” alisema Albert Einstein. Kwenye baa la njaa, kuna fursa ya kununua chakula kutoka mahali penye chakula tele na kuuza vyakula penye baa la njaa. Kuna methali ya Tanzania isemayo, “Kisababishacho baa la njaa, kinakuelekeza pia mahali pa kupata chakula.”

Wakati wa baa la njaa, akili itafanya kazi kwa namna ya pekee, utaumiza kichwa na kutafuta suluhisho. Kuna tofauti ndogo kati ya vikwazo na fursa, pingamizi na fursa, matatizo na fursa, balaa na fursa, magumu na fursa, shida na fursa, mgogoro na fursa, karaha na fursa.

Yabadili yote mabaya kwa faida yako.

You can share this post!

Serikali yamrukia gavana kuhusu usalama

Sababu za kudhibiti filamu wanazotazama watoto