• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 7:55 AM
KPA na Equity Bank kuwakilisha Kenya kwenye vikapu Afrika

KPA na Equity Bank kuwakilisha Kenya kwenye vikapu Afrika

Na CHRIS ADUNGO

MABINGWA wa kitaifa Equity Bank Hawks na Halmashauri ya Bandari ya Kenya (KPA) watapeperusha bendera ya Kenya kwenye fainali za mchezo wa vikapu za Klabu Bingwa Afrika zitakazoandaliwa nchini Misri kuanzia Machi 2021.

Hayo ni kwa mujibu wa Katibu Msaidizi wa Shirikisho la Vikapu la Kenya (KBF), Ambrose Kisoi ambaye amethibitisha kwamba vikosi hivyo viwili vimepata idhini ya kunogesha mashindano hayo.

“Equity Bank na KPA watakuwa sehemu ya klabu zitakazopeperusha bendera ya Kenya kwenye mapambano hayo ya kimataifa yatakayofanyika kati ya Machi 1-8 nchini Misri badala ya Tanzania jinsi ilivyoratibiwa awali,” akasema Kisoi kwa kufichua kwamba vikosi hivyo vimepata barua za kuidhinisha ushiriki wao kutoka Shirikisho la Vikapu la Afrika (Fiba).

KPA ambao walizidiwa ujanja na Equity Bank kwenye Ligi Kuu ya Kenya mnamo 2019-20, wamejisuka upya kwa minajili ya msimu huu wa 2020-21 baada ya kusajili idadi kubwa ya wanavikapu wapya.

Chini ya kocha Anthony Ojukwu, KPA waliingia kambini mnamo Jumamosi kuanza kujifua kwa kampeni za msimu mpya utakaoanza mwezi ujao.

KPA waliambulia nafasi ya pili kwenye fainali za Klabu Bingwa Afrika mwaka jana jijini Dar es Salaam, Tanzania baada ya kuzidiwa maarifa na JKL Dolphins ya Uganda. Equity Bank waliridhika na nafasi ya tatu.

Vikosi viwili vya kwanza katika mapambano hayo vitawakilisha eneo la Zone Five katika fainali za Klabu Bingwa barani Afrika (Fiba Women’s Africa Club Championships).

Hii ni mara ya kwanza kwa fainali za wanawake kutenganishwa na zile za wanaume ambazo kwa sasa zimemezwa na kipute cha Basketball Africa League (BAL). Mabingwa wa kitaifa, Ulinzi Warriors, watapeperusha bendera ya Kenya kwenye kivumbi hicho cha BAL nchini Uganda.

Wanavikapu wa Kenya wametiwa katika Kundi C kwa pamoja na Zimbabwe, Tanzania, Sudan Kusini, Algeria, Equatorial Guinea, Libya, Rwanda, Algeria na Guinea Bissau kwenye fainali za FIBA Africa Zone Five kwa upande wa wanaume.

Wakati uo huo, fowadi Tyler Ongwae wa timu ya taifa ya vikapu almaarufu Kenya Morans, amejumuishwa kwenye orodha ya wachezaji 10-bora walionogesha awamu ya kwanza ya mechi za kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (Fiba Afro-Basket) 2021 jijini Kigali, Rwanda.

Mkondo wa pili wa michuano hiyo itakayoamua washiriki 16 wa mwisho umepangiwa kufanyika kati ya Februari 18-20 katika nchi itakayofichuliwa na vinara wa Shirikisho la Vikapu la Afrika (FIBA) wiki hii.

Kenya iko katika Kundi B kwa pamoja na Senegal, Angola na Msumbiji ambao wamefichua azma ya kuandaa mkondo wa pili wa mashindano hayo yaliyoshuhudia mkondo wa kwanza ukifanyika jijini Kigali, Rwanda mnamo Novemba 2020.

Morans ambao walivuna medali ya fedha kwenye Kombe la Afrika la wanavikapu wanaochezea klabu za humu barani (AfroCan) mnamo 2019, ilipoteza dhidi ya Senegal (92-54) na Angola (83-66) kabla ya kubwaga Msumbiji (79-62) katika mchuano wa mwisho wa Kundi B mnamo Novemba mwaka jana.

Matokeo hayo yalidumisha Morans katika nafasi ya tatu na mwisho ya kufuzu. Senegal inaongoza kwa alama sita ikifuatiwa na Angola (tano), Kenya (nne) na Msumbiji (tatu).

Washindi watatu wa kwanza kutoka kila kundi watafuzu kushiriki AfroBasket nchini Rwanda mnamo Agosti/ Septemba 2021. Kenya haijawahi kunogesha kivumbi cha AfroBasket tangu iandae fainali za 1993.

Baada ya kushinda Msumbiji, Kenya ilipanda orodha ya Shirikisho la Vikapu Duniani kwa nafasi saba hadi 115. Chini ya kocha Cliff Owuor ambaye kwa sasa anadhibiti mikoba ya APR nchini Rwanda, Morans walitua jijini Kigali kwa minajili ya mechi za mkondo wa kwanza wakikamata nafasi ya chini zaidi kwenye Kundi B. Wakati huo, walikuwa wakishikilia nambari 122 duniani huku Angola, Senegal na Msumbiji wakiwa katika nafasi za 32, 35 na 93 mtawalia.

  • Tags

You can share this post!

PSG warejea kileleni mwa jedwali l

Fowadi matata Onyango atupwa nje ya timu ya taifa ya hoki