Hotuba ya Uhuru yazidisha nyufa katika ngome yake

Na MWANGI MUIRURI

HOTUBA ya Rais Uhuru Kenyatta kwa wakazi wa ngome yake ya Mlima Kenya mnamo Jumatatu, imepanua migawanyiko ya kisiasa ambayo imekuwa ikishuhudiwa katika eneo hilo.

Hii ni licha ya kuwarai wenyeji kuiunga mkono serikali, handisheki kati yake na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga na ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI).

Mirengo mikuu ya kisiasa katika eneo hilo ni ‘Kieleweke’, ambao unamuunga mkono Rais, na ‘Tangatanga’ unaowajumuisha wanasiasa ambao wamekuwa wakimpigia debe Naibu Rais William Ruto.

Kufuatia mahojiano hayo, wanasiasa wa mrengo wa ‘Kieleweke’ walimsifu Rais kwa kujieleza waziwazi huku wale wa ‘Tangatanga’ wakiyapuuzilia mbali, hasa kwa kuonekana kuwalenga.

Mbunge Nduati Ngugi (Gatanga) alisema: “Kama watu wanaomuunga mkono Rais Kenyatta, ni matumaini yetu kuwa wale wanaompinga kwa maslahi yao binafsi watazingatia wito wake kwetu kuwahudumia wananchi. Vilevile, watazingatia ujumbe wake kwetu kupigania umoja badala ya kuendeleza migawanyiko iliyopo.”

Hata hivyo, mbunge Rigathi Gachagua (Mathira), aliyezungumza kwa niaba ya kundi la Tangatanga, alisema Rais alionekana “kutofahamu uhalisia wa changamoto zinazolikumba eneo la Mlima Kenya, msimamo wa kampeni za ‘Huster’ na pia amechelewa kuwafikia wananchi kwani wengi wao washapoteza matumaini katika uongozi wake”.

Aliyekuwa mbunge wa Maragua, Elias Mbau, aliliomba eneo hilo kuzingatia kauli ya Rais kuwa wale ambao wamekuwa wakimpiga vita serikalini huwa wanapora zaidi ya Sh730 bilioni kwa mwaka.

Hata hivyo, Bw Gachagua alisema Rais Kenyatta anaonekana kutofahamu maslahi ya kisiasa na kiuchumi ya ngome yake.

“Ni kinaya kwa Rais kusema bado anaidhibiti serikali yake ilhali kuna wizi na uporaji ambao umekuwa ukiendelea. Ikiwa hali iko hivyo, basi anasimamia uporaji anaodai umekuwa ukiendelea,” akasema.

Licha ya hayo, alisifu baadhi ya kauli za Rais Kenyatta.

“Nitampongeza Rais kwa mambo kadhaa; kwanza alionyesha unyenyekevu mkubwa. Hakujipiga kifua kuhusu BBI. Alionekana kufahamu kuwa kuna shida, hali iliyomfanya kuhimiza umoja na maridhiano. Hata hivyo, hakubaini kuwa BBI si miongoni mwa masuala muhimu Mlima Kenya,” akaongeza.

Bw Gachagua alisema kuna masuala manne makuu yanayolizonga eneo hilo, ambayo ni: ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana, sera mbaya za serikali ambazo zimeathiri biashara za wenyeji, kudorora kwa sekta ya kilimo na janga la virusi vya corona.

Mbunge Kanini Keega, ambaye anaegemea mrengo wa ‘Kieleweke’, alimtetea Rais kwa “hotuba yake nzuri.”

Mbunge huyo alimlaumu vikali Dkt Ruto kwa “kumwacha mkubwa wake na kuanza kampeni za mapema kwa maslahi yake binafsi.”

Naye Kiranja wa Wengi kwenye Seneti, Irungu Kang’ata alimsifu Rais Kenyatta kwa hotuba yake, akisema ilirejelea masuala aliyoyataja kwenye barua yake aliyomwandikia mnamo Desemba 30.

Alisema alifurahi sana, hasa baada ya Rais kuonekana kufahamu uhalisia kuhusu hali ilivyo katika ngome yake.

Habari zinazohusiana na hii