• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 2:25 PM
Diwani akanusha madai kuwa anachochea uhasama Kapedo

Diwani akanusha madai kuwa anachochea uhasama Kapedo

Na RICHARD MAOSI

DIWANI wa wadi wa Silale iliyoko Kaunti ya Baringo Nelson Lotela amejitenga na madai kuwa amekuwa akichochea uhasama unaoshuhudiwa eneo la Kapedo.

Akizungumza katika ofisi za Idara ya Uchunguzi wa Makosa ya Jinai DCI katika Kaunti ya Nakuru, Alhamisi, ameomba serikali kuharakisha operesheni ya kuleta utulivu Kapedo.

Kulingana naye haelewi mbona jina lake limekuwa likitajwa kila mara wahalifu wanapovamia watu na kuiba mifugo.

“Polisi wamekuwa wakiniandama kwa madai ambayo sio ya kweli,” akasema.

Aidha Lotela ameeleza kuwa Silale inapatikana mbali sana na Kapedo, sehemu ambayo imekuwa ikikumbwa na mizozo na ukosefu wa usalama mara kwa mara.

Lotela ameambia Taifa Leo hakuwa na habari kuhusu mikutano ya kupanga namna ya kuwashambulia polisi Kapedo.

“Serikali inaweza kushirikiana na wakazi wa Baringo kurejesha hali ya amani na utulivu badala ya kulenga watu wachache wasiokuwa na hatia,” amesema.

Lotela ameandikisha taarifa katika DCI na hatimaye kuzungumza na wanahabari ambapo amekiri kuwa eneo la Kapedo limejaa wahalifu ingawa hakuwa akishirikiana nao.

Mara ya kwanza Lotela alijisalimisha kwa polisi Jumamosi, baada ya mshirikishi wa eneo la Bonde la Ufa George Natembeya kutoa amri ya viongozi wa Baringo kuchunguzwa.

Kulingana na Natembeya diwani huyo pamoja na Mbunge wa Tiaty William Kamket ni baadhi ya watu wenye ushawishi mkubwa, na huenda wamekuwa wakishirikiana na wahalifu.

Haya yanajiri baada ya Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i kusema serikali inaendeleza uchunguzi ili kubaini wanaochangia mauaji katika eneo la Kapedo, Tiaty na Arabai.

Angalau kufikia sasa serikali imefanikiwa kutwaa silaha ambapo bunduki 35 zimesalimishwa.

Watu saba zaidi wamekamatwa.

You can share this post!

Wakazi Lamu wapendekeza barabara na vichochoro kupewa...

Chama cha ODM chaunga mgombea wa Wiper katika uchaguzi...