• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Rais awaongoza vigogo wa siasa kumwomboleza Nyachae

Rais awaongoza vigogo wa siasa kumwomboleza Nyachae

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta Jumatatu aliwaongoza viongozi wakuu nchini kumwomboleza aliyekuwa Waziri wa Fedha Simeon Nyachae akimtaja kama kiongozi ambaye alichangia maendeleo katika taifa hili.

Mzee Nyachae,88, alifariki katika Hospitali ya Nairobi ambako amekuwa akipokea matibabu kwa kipindi kirefu.

Rais Kenyatta alisema kwa kufaulu kuhudumu katika utumishi wa umma hadi ulingo wa biashara na siasa, Mzee Nyachae ameonyesha kuwa bidii na ukakamavu ina faida katika maisha ya mwanadamu.

“Nimehuzunishwa na kifo cha Mzee Simeon Nyachae, Mkenya mashuhuri, rafiki na ambaye mchango wake katika ujenzi wa taifa la Kenya utakumbukwa daima.

“Kwa miaka aliyohudumia taifa hili, kuanzia wakati wake katika utawala wa mkoa hadi sekta ya biashara na ulimwengu wa siasa, Mzee Nyachae alionyesha msukumo wa kufaulu. Na anapoondoka ulimwenguni, ameacha kumbukumbu ya ufanisi,” Rais Kenyatta akasema.

Naye Naibu Rais William Ruto alimtaja marehemu Nyachae kama kiongozi aliyejitolea kuwatumikia watu wake na taifa hili katika nyanja za utumishi wa umma, siasa na shughuli za kuunganisha wananchi.

“Mzee Nyachae alikuwa kiongozi mwenye kipawa cha usemi ambapo mchango wake katika siasa za nchi hii utakumbukwa daima. Pia alikuwa kiongozi mkarimu ambaye aliwasaidia watu wengi wasiojiweza katika jamii,” akasema Dkt Ruto.

Kwa upande wake, kiongozi wa ODM Raila Odinga alituma risala zake za rambirambi akisema jamii ya Abagusii imempoteza mmoja wa kiongozi na mtetezi sugu wa masilahi yao.

“Natuma risala zangu za dhati kwa familia ya waziri wa zamani, mbunge na mtumishi wa umma, Simeon Nyachae. Mungu aiweke roho yake pema penye amani,” Odinga akasema kupitia Twitter.

You can share this post!

Sonko aandamana na wakili wake hadi afisi za DCI

Jaji aliyemzima Mwilu amrudisha kuwa Kaimu Jaji Mkuu