KINYUA BIN KING’ORI: Mabunge ya kaunti yasiwe na pupa kupitisha BBI

Na KINYUA BIN KING’ORI

BAADA ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuthibitisha saini za kuunga mkono ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI), unaopendekeza marekebisho ya Katiba, sasa Tume imepeleka Mswada katika mabunge ya kaunti ili kujadliliwa.

Mabunge hayo, kwa mujibu wa sheria, yatakuwa na muda wa siku 90 kukataa au kupitisha Mswada huo.

Wakenya wanatarajia wawakilishi wadi (MCA) kusoma na kutathmini Mswada huo kwa umakini bila kuegemea mirengo ya Tangatanga wala Kieleweke.

Inavunja moyo kusikia kuwa mabunge fulani yataharakisha zoezi hilo bila kuzingatia ufaafu wa BBI kwa wananchi waliowachagua; bali nia yao ni kudhihirisha ufuasi kwa vigogo wao wa kisiasa nchini.

Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa ODM, Bw Raila Odinga, wamekuwa wakitumia muda wao mwingi kukutana na makundi mbalimbali yakiwemo ya makabila kutafuta uungwaji mkono wa BBI wakati wa kura ya maoni.

Sasa wamepiga hema kwa wawakilishi wadi, yaani madiwani, kuwaahidi matamu ikiwa watapitisha Mswada wa BBI katika mabunge ya kaunti zao.

Kikao cha hivi karibuni kiliandaliwa na Rais Kenyatta katika ikulu ndogo ya Sagana, Kaunti ya Nyeri, ambapo alipigia debe BBI kwa viongozi kutoka Mlima Kenya.

Nahofia madiwani watatumia Mswada huu kujipendekeza kwa Rais na Odinga katika mrengo wao wa Kieleweke; au Naibu Rais William Ruto na mrengo wa Tangatanga wanaopinga kuandaliwa kwa kura ya maoni kabla ya 2022.

Wawakilishi wadi wanafaa kufahamu wajibu wao ni muhimu mno; kuwa mstari wa mbele kutetea ugatuzi.

Hivyo, wanahitaji kufanya uamuzi wao kuunga au kupinga Mswada kwa misingi ya maslahi ya taifa, kaunti na ugatuzi bila kusahau nafasi ya mwananchi mlalahoi.

Vinginevyo, watakuwa wamewafelisha Wakenya. Aidha, watumie fursa hiyo kulinda Katiba ya 2010 dhidi ya mapendekezo yatakayoihujumu, ikizingatiwa kuwa haijatekelezwa kikamilifu huku nao wanasiasa fulani wakiwa na msukumo wa kuifanyia mageuzi kwa manufaa yao.

Ni vyema wasikubali kutumiwa kuingilia siasa za urais 2022. Kile wananchi wanataka ni kushirikishwa katika mchakato mzima, wakitarajia madiwani wataandaa vikao vya umma mashinani ili kutafuta maoni na mapendekezo yao kufanya Mswada huo kuwa bora.

BBI ikiwa na vipengee vyenye manufaa kwa kaunti na Wakenya kwa jumla, wawakilishi wadi waipitishe bila kujali vitisho vya viongozi wakuu.

Iwapo haina la kuwapa Wakenya tabasamu na matumaini, basi hawana buni kuikataa kama ukoma bila kuogopa viongozi hao wakuu watasemaje.

Ukweli ni kwamba, ikiwa mabunge ya kaunti yatafanya maamuzi yao kwa pupa, yatakuwa yametia msumari moto katika taifa letu.

Huenda pupa yao itatia mapungufu zaidi kwenye Katiba yetu ya 2010.

Isitoshe, wakiruhusu ulafi kuwatawala huenda wakawasha moto utakaochoma ugatuzi na serikali za kaunti, na hivyo kusambaratisha nia njema ya kufanikisha ugatuzi mashinani.

Misimamo ya Rais Kenyatta, Dkt Ruto, Bw Odinga, kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka, kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi na viongozi wa kidini isije kupewa kipaumbele; bali MCAs wazingatie haki watakapokuwa wakichanganua na kupigia kura hatima ya BBI.

Habari zinazohusiana na hii

BBI YAINGIA ICU

Kwani kuliendaje?