BBI: Karua atawezana?

Na MWANGI MUIRURI

KINARA wa Narc Kenya Martha Karua amejipata kona mbaya kutoka kwa mrengo wa Rais Uhuru Kenyatta katika serikali, baada ya kujitokeza kuongoza upinzani dhidi ya mpango wa BBI.

Siku moja tu baada ya kutoa tangazo hilo wakereketwa wa upande wa serikali wameanza kumpaka tope shujaa huyo wa kupigania mageuzi na utawala bora, wakimtaja kama anayetumiwa na Naibu Rais William Ruto kuongoza kampeni ya ‘La’ dhidi ya BBI.

“Bi Karua ni kivuli cha Ruto ambaye ndiye mkuu wa pingamizi dhidi ya BBI. Karua hana uwezo wowote wa kuongoza upinzani dhidi ya BBI lakini anapigwa jeki na waasi katika serikali,” Naibu Mwenyekiti wa Jubilee, David Murathe aliambia Taifa Leo jana.

Kombora hilo ni mwanzo tu wa vita vikali ambavyo Bi Karua anatarajiwa kukabiliana navyo kutokana na msimamo wake dhidi ya BBI yake Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Wachanganuzi wa siasa wanasema mbunge huyo wa zamani wa Gichugu, Kaunti ya Kirinyaga atakumbana na changamoto za kifedha kuendesha kampeni zake kote nchini, propaganda za kumvunja moyo na kumchafulia sifa pamoja na kutumiwa kwa taasisi kama vile polisi kuhujumu juhudi zake.

Serikali pia iko tayari kutumia kila mbinu kusukuma BBI, ambapo tayari imewaahidi MCA kuwapa Sh2 bilioni kila mmoja za kununua magari ili wapitishe BBI.

Changamoto nyingine inayomkabili mwanasiasa huyo ni kuwa anaoshirikiana nao kwenye juhudi zake hawana umaarufu wa kisiasa katika ngazi ya kitaifa.

Tatizo ni kwamba licha ya Bi Karua kuwa mweledi wa kujadili masuala nyeti kwa ufasaha, atakuwa na wakati mgumu kuwashawishi wananchi kupigia BBI kura ya ‘La’, ikizingatiwa wengi wa Wakenya wamezoea kushabikia siasa duni za kikabila na kuhongwa na wanasiasa.

Lakini Bi Karua anashikilia kuwa hatarudi nyuma na hasukumwi na yeyote katika kupinga BBI: “Niko na haki ya kusimama kwa imani yangu ya kisiasa bila kushambuliwa kama anayesukumwa na wengine.

“Nilipambana kuokoa utawala wa Mzee Kibaki baada ya uchaguzi wa 2007. Wakati huo wote mimi sikuwa kivuli cha yeyote bali nilikuwa shujaa. Mbona leo naitwa kivuli?” akateta Bi Karua.

Mbunge wa Gatanga Nduati Ngugi na aliyekuwa Mbunge wa Maragwa, Elias Mbau naa wanapuzilia mbali juhudi za Bi Karua wakidai kuwa anatafuta umaarufu wa kuwania ugavana wa Kaunti ya Kirinyaga mwaka ujao, wakisema hana makali ya kuzima BBI.

“Hatupingi BBI ili kujipatia umaarufu bali tunalenga kuhamasisha Wakenya wagutuke kuhusu njama inayoendelezwa na walio madarakani. Nikiwa na imani kuwa BBI haitufai kwa sasa na sio suala la dharura, nimeamua kujaza pengo la kuongoza walio na imani kuwa wanatapeliwa na kuhadaiwa kisiasa na Rais Kenyatta na Raila.”

Bi Karua anataja BBI kama njama ya viongozi wachache wenye ushawishi kisiasa kuendeleza maslahi yao ya ubinafsi, na kuwa haina mchango kwa maisha ya Wakenya walio wengi.

“Huwezi ukabomoa uchumi kupitia uharibifu wa biashara, kukopa fedha kiholela, kukosa kupambana na ufisadi na kuongeza raia ushuru wa juu kupindukia, kisha uje kutwambia makosa uliyofanya yatarekebishwa na BBI. Hata hauna heshima kwa Katiba tuliyo nayo kisha unaambia Wakenya kuwa inahitaji kurekebishwa! Huu ni unafiki!”

Seneta wa Murang’a Irungu Kang’ata anamtetea Bi Karua akisema kuwa anaeleza tu maoni ya wengi na ana ukakamavu wa kutosha kufanikiwa.

Mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua naye anasema wanaomkashifu Bi Karua ni wanasiasa wanaolenga kunufaika na BBI kibinafsi.

Bw Mark Bichachi, ambaye alihudumu kama mtaalamu wa mikakati ya siasa wa Bi Karua, anamtaja mwanasiasa huyo kuwa miongoni mwa watu wachache nchini walio na msimamo thabiti kuhusu imani yao. Alisema Bi Karua sio mgeni katika siasa za kutetea yaliyo ya haki kwa Wakenya.

Bw Bichachi anataka harakati za Bi Karua kusukumana na aliyekuwa Rais Daniel Moi katika vita vya ukombozi wa kidemokrasia.

Habari zinazohusiana na hii

BBI YAINGIA ICU

Kwani kuliendaje?