• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Madiwani watiwa presha kupitisha BBI

Madiwani watiwa presha kupitisha BBI

Na GEORGE ODIWUOR

MADIWANI katika kaunti zinazounga mkono handisheki wanashinikizwa kupitisha mswada kuhusu ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI) kufikia Ijumaa.

Kiongozi wa ODM, Raila Odinga, alikuwa ameyaomba mabunge kwenye kaunti 24 zinazomuunga mkono kupitisha mswada huo kufikia mwishoni mwa mwezi huu.Hata hivyo, baadhi ya wanachama wa ODM wametoa maoni tofauti, kwani wanataka mswada huo kupitishwa kwa muda wa wiki moja ijayo.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), imewapa madiwani muda wa miezi mitatu kujadili kuhusu ripoti na kuwasilisha maoni yao kwa maspika wa Bunge la Kitaifa na Seneti.Bunge la Kaunti ya Siaya ndilo lilikuwa la kwanza kuupitisha mswada huo kati ya kaunti 47 kote nchini.

Shinikizo sasa zimeelekezwa kwa kaunti zingine tatu katika eneo la Nyanza kuiga madiwani katika Bunge la Kaunti ya Siaya.Kaunti hizo ni Homa Bay, Migori, Kisumu na zingine 20 zinazomuunga mkono Bw Odinga.

Madiwani walielekezewa shinikizo hizo na viongozi wa ODM Ijumaa, wakati wa mazishi ya Bi Priscah Ondigo, nyanyake Seneta Moses Kajwang’ wa Homa Bay.

Mazishi hayo yalifanyika katika kijiji cha Gongo, wadi ya Kagan, eneobunge la Rangwe.Bunge la Kaunti ya Homa Bay tayari limeonekana kukumbatia mwito huo.

Awali, bunge hilo lilikuwa limewaomba wenyeji kuwasilisha maoni yao kuhusu mswada kufikia Ijumaa ama mapema, ambapo baadaye ungewasilishwa rasmi bungeni na kujadiliwa.

Hata hivyo, bunge lilibadilisha ratiba hiyo ambapo kinyume na awali, mswada huo umepangiwa kujadiliwa na kupitishwa Alhamisi.Hayo yanajiri huku malalamishi yakiibuka kwamba huenda wenyeji wakakosa kupata muda wa kutosha kuisoma ripoti hiyo.

Wakosoaji wa handisheki wameeleza tashwishi kuhusu kasi ambayo madiwani wanapanga kuupitisha mswada kama vile Kaunti ya Siaya, ambapo madiwani waliipitisha kwa muda wa wiki moja pekee.

Hata hivyo, mbunge TJ Kajwang wa Ruaraka alipuuzilia mbali madai hayo, akisema Wakenya wamepewa muda wa kutosha kuisoma na kuielewa ripoti hiyo.

“Kuwashirikisha wananchi kwenye mchakato huo hakulengi kuibadilisha ripoti. Wakenya wengi wanajua yaliyomo ndani,” akaeleza mbunge huyo.Mbunge wa Rangwe, Dkt Lilian Gogo, aliwaambia wenyeji kuwa ripoti itasaidia kumaliza ghasia ambazo huwa zinaathiri maendeleo nyakati za uchaguzi.

Seneta Kajwang’ aliipigia debe ripoti, akisema itaongeza mgao wa fedha ambazo zinatumwa na serikali kwa kaunti.Ripoti inapendekeza kaunti kupata mgao wa angaa asilimia 35 ya pato la jumla la taifa, kinyume na sasa ambazo huwa zinapata asilimia 15 ya mgao wa fedha hizo.

You can share this post!

JAMVI: Sonko alivyojipalia makaa mwenyewe

EACC yaelezea hofu ya fedha za serikali kuporwa uchaguzi...