• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:50 AM
JAMVI: Sonko alivyojipalia makaa mwenyewe

JAMVI: Sonko alivyojipalia makaa mwenyewe

Na BENSON MATHEKA

Aliyekuwa Gavana wa Nairobi, Bw Mike Sonko anajuta kwa vitendo alivyofanya akiwa mamlakani; akiepuka kuadhibiwa kwa sababu ya ushawishi na ukuruba wake na viongozi na maafisa wakuu serikalini.

Tangu alipochaguliwa mbunge wa Makadara, Bw Sonko alionyesha sarakasi za kila aina zilizomfanya ashtakiwe kortini.

Mojawapo ya vituko vyake ni alipompiga afisa wa polisi wa cheo cha Inspekta Mkuu katika uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) akimsindikiza Rais Uhuru Kenyatta akiondoka nchini kuelekea The Hague kwa kesi iliyohusu ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007.

Japo alishtakiwa kortini, kesi hiyo iliondolewa baada ya kuisuluhisha nje ya mahakama. Kila aliposhtakiwa kortini, mamia ya wafuasi wake, wabunge na wanasiasa, walikuwa wakifurika kortini kumuunga mkono.

Aliendeleza sarakasi zake akiwa seneta wa Kaunti ya Nairobi bila kuchukuliwa hatua, ukuruba wake na Rais Uhuru Kenyatta ukiimarika na kupata nguvu.Wakati mmoja, Bw Sonko alimpigia simu Rais Kenyatta moja kwa moja kuwasilisha malalamishi ya wakazi ambao nyumba zao zilipangiwa kubomolewa.

Aliweka mazungumzo yake na Rais wazi, wakazi hao wasikie, jambo ambalo halikuwafurahisha maafisa wakuu wa serikali. Wadadisi wa siasa wanasema kuwa tukio hilo na mengine mengi ambayo aliongoza wakazi kuvamia majengo au ardhi za watu kinyume cha sheria miongoni mwao washirika wa maafisa wakuu wa serikali yalitia doa uwezo wake wa kuongoza.

“Sonko alilewa mamlaka, akaonyesha si mkomavu katika uongozi. Japo vituko vyake vilimfanya kupendwa na watu wa tabaka la chini aliokuwa akiwatetea, watu wenye ushawishi serikalini hawakufurahia, walimuona kama mtu hatari asiyeweza kulinda habari muhimu za serikali na ofisi anazoshikilia,” asema mchanganuzi wa siasa na uongozi Charles Mutahi.

“Kumbuka kisa kimoja alichodai kuwa akiwa gavana wa Nairobi angeweza kushikilia uongozi wa nchi rais na naibu wake wakiwa nje ya nchi. Hii ilionyesha ukosefu wa ukomavu wa uongozi,” asema Mutahi.

Bw Sonko alisema hayo wakati wa mazishi ya mume wa waziri msaidizi wa makao Wavinya Ndeti yaliyofanyika eneo la Athi River.

Akiwa seneta wa Nairobi, Sonko alianzisha kundi la Sonko Rescue Team kutoa huduma muhimu katika Kaunti ya Nairobi ambazo zilimfanya kuwa maarufu zaidi miongoni mwa wakazi.Kupitia kundi hilo ambalo baadaye alilisajili kuwa shirika lisilo la kiserikali, Sonko alisaidia wakazi wa mitaa ya mabanda kuzima moto, huduma za ambulensi na chakula miongoni mwa nyingine.

Wachanganuzi wanasema ingawa alinuia kumpiga vita aliyekuwa gavana wakati huo, Dkt Evans Kidero, shughuli za kundi hilo hazikufurahisha viongozi na maafisa wakuu serikalini.

“Shirika hilo lilikuwa limeendelea kupigwa darubini. Wakati huo, Sonko alikuwa na uhusiano mwema na viongozi wa serikali kwa sababu Kidero alikuwa wa upinzani. Hata hivyo, shughuli za Sonko Rescue Team hasa zilizofadhiliwa zilitiliwa shaka na hakuna serikali inayoweza kuruhusu kundi kama hilo kuhudumu bila kulifuatilia kwa makini,” asema Mutai.

Mchanganuzi huyu anasema hii na sarakasi zake ndizo zilizofanya chama cha Jubilee kuchelea kumpa tiketi ya kugombea ugavana kwenye uchaguzi mkuu wa 2017 hadi dakika ya mwisho.Ingawa inasemekana kuwa ni Naibu Rais, Dkt William Ruto aliyemsaidia kupata tiketi ya Jubilee kutetea ugavana, wadadisi wanasema kwamba Jubilee ingepoteza kiti hicho kama haingempa tiketi.

“Sonko angeshinda hata kama angekuwa mgombeaji huru, umaarufu wake ulikuwa umekita mizizi sio tu Nairobi mbali pia kote nchini,” asema mchanganuzi wa siasa Isaiah Kwesi.

Anasema baada ya kushinda ugavana, Sonko alilewa mamlaka na hata akaanza kuwadharau maafisa wakuu wa serikali na kuropokwa. Aliendeleza sarakasi zake kwa kugonganisha na kulimbikizia lawama maafisa wa serikali na kuvuruga uongozi wa bunge la Kaunti.

“Sonko alianza kuporomoka alipotofautiana na aliyekuwa naibu wake Polycarp Igathe ambaye alitegemewa na wakuu wa serikali kuwakilisha maslahi yao na kuhakikisha usimamizi bora katika serikali ya Kaunti ya Nairobi.Bw Sonko alimhujumu naibu wake huyo hadi akajiuzulu na hapo masaibu yake ndipo yakaanza,” asema Kwesi.

Mchanganuzi huyu asema Sonko alikataa ushauri wa Rais Kenyatta ambaye alikuwa mvumilivu naye.“Kilele cha sarakasi za Sonko kilichochangia kuporomoka kwake ni kudai kuwa familia ya Rais iliingilia masuala ya uongozi wa Kaunti kwa kumchagulia aliyefaa kuteua kama naibu gavana.

Pili, alijikaanga kwa madai yake kwamba maafisa wakuu wa serikali kama vile Katibu wa Usalama wa Ndani, Dkt Karanja Kibicho alihusika katika kupanga ghasia za baada ya uchaguzi wa 2017 na kuusingizia muungano wa upinzani wa NASA,” asema Kwesi.“Alivuka mipaka kwa kutoa madai hayo.

Ni kama kuhusisha serikali na ghasia hizo ambazo watu kadhaa waliuawa. Kufanya hivi ni sawa na kuchochea raia dhidi ya maafisa wa serikali. Sarakasi zake hazingevumiliwa zaidi,” asema.

Wadadisi wanasema ikizingatiwa kuwa ana tabia ya kurekodi mawasiliano yake na viongozi hata wakati wa shughuli rasmi, Sonko lazima angekomeshwa hasa baada ya kujiunga na mrengo wa Dkt Ruto.

You can share this post!

Mipango mikubwa ya rais wa ngumi duniani anayo kwa Kenya

Madiwani watiwa presha kupitisha BBI