• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
TAHARIRI: Madai kuhusu SGR yawekwe bayana

TAHARIRI: Madai kuhusu SGR yawekwe bayana

KITENGO CHA UHARIRI

MATAMSHI ya hivi majuzi kutoka kwa Naibu Rais, Dkt William Ruto, kuhusu mradi wa usafirishaji mizigo kutoka Mombasa kwa reli ya SGR yanafaa kuchukuliwa kwa uzito.

Alipokuwa katika ziara Pwani wikendi, Dkt Ruto alikiri kulikuwa na utapeli ambao ulisababisha mpango huo kwenda kombo hadi biashara nyingi za uchukuzi Pwani zikafilisika.

Kulingana naye, mpango wa kujenga bandari kavu eneo la Pwani ulicheleweshwa kusudi na watu ambao hakuwataja, na badala yake ujenzi wa bandari kama hizo ukaharakishwa maeneo ya Nairobi na Naivasha.

Matokeo yake ni kuwa, wafanyabiashara wachache walinufaika huku wengine wengi hasa walio Pwani wakafilisika, uchumi wa ukanda huo ukaathirika na idadi kubwa ya watu wakakosa ajira.

Matamshi haya, kutoka kwa kiongozi aliye wa pili kimamlaka nchini yanafaa kufungua sura mpya kuhusu hatua ambazo zaweza kuchukuliwa kunusuru uchumi wa Pwani. Idara husika katika serikali kuu sasa zinafaa kujitokeza wazi kufafanua kuhusu madai hayo ya Naibu Rais.

Tangu mradi wa SGR ulipoanzishwa, kulikuwa na vilio kutoka kwa viongozi, wakazi na mashirika ya kijamii eneo hilo.

Wakati huo wote, serikali kuu ilipuuza vilio hivyo na badala yake ikadai wanaopinga wanaingiza siasa kwa masuala ya maendeleo.

Kufuatia matamshi ya Naibu Rais, kuna wengi ambao wanaona angesimama kidete wakati ule ambapo wakazi walikuwa wanalalamika, badala ya kujitokeza wakati huu ambapo anakaribia kuhitaji kura za urais kutoka kwa Wapwani.

Naibu Rais, licha ya changamoto zote anazopitia ndani ya serikali, bado ana ushawishi ambao angetumia kurekebisha mambo ili kufufua uchumi wa Pwani.

Ni aibu kwa kiongozi wa tajriba yake kuibua malalamishi sawa na raia wa kawaida wanaomtegemea.Kwa vile sasa amejitokeza wazi, itakuwa ni jukumu la serikali kufafanua ukweli uliopo kuhusu mpango wa usafirishaji mizigo kwa SGR.

Wananchi waelezwe bayana ni kwa nini ujenzi wa bandari kavu uliharakishwa nje ya Pwani, na ifafanue madai ya Dkt Ruto kuwa ujenzi aina hiyo ulicheleweshwa Dongo Kundu.

Masaibu ya wananchi hayafai kamwe kupuuzwa kila mara hadi msimu wa kisiasa wa shida hizo kutumiwa na wanasiasa wanapotafuta kura unapofika.

You can share this post!

Tangatanga Pwani wakata tamaa ya kuunda chama, wataingia UDA

BI TAIFA FEBRUARI 8, 2021