• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 8:03 AM
Manchester City wazamisha chombo cha Arsenal na kuanza kunusia taji la EPL

Manchester City wazamisha chombo cha Arsenal na kuanza kunusia taji la EPL

Na MASHIRIKA

KOCHA Pep Guardiola amesema anashangazwa na ubora wa fomu ya kikosi chake cha Manchester City wakati ambapo wapinzani wao wakuu katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) wanasuasua.

Chini ya Guardiola, Man-City hawajawahi kupoteza alama yoyote tangu Disemba 15, 2020 na ushindi wao wa 1-0 dhidi ya Arsenal mnamo Jumapili ugani Emirates uliwasaidia kufungua pengo la alama 10 kileleni mwa jedwali.

Zikisalia mechi 13 pekee kwa kampeni za EPL muhula huu kutamatika rasmi, Man-City kwa sasa wanajivunia alama 59. Manchester United waliowapepeta Newcastle United 3-1 uwanjani Old Trafford wanakamata nafasi ya pili kwa pointi 49 sawa na Leicester City waliovuna ushindi wa 2-1 dhidi ya Aston Villa ugenini katika mechi nyingine ya Februari 21, 2021.

“Yashangaza kuwa wakati ambapo wapinzani wetu wanapoteza alama muhimu ligini, Man-City wamesalia thabiti katika kipindi cha miezi miwili iliyopita. Hili ni jambo ambalo sikulitarajia kabisa,” akasema kocha huyo raia wa Uhispania ambaye pia aliwahi kudhibiti mikoba ya Barcelona na Bayern Munich.

Licha ya kuchezea ugenini, Man-City walijibwaga ugani dhidi ya Arsenal kwa matao ya juu na wakapata bao la pekee na la ushindi katika dakika ya pili kupitia kwa fowadi wa zamani wa Liverpool, Raheem Sterling. Goli hilo lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati ya Sterling na kiungo mvamizi raia wa Algeria, Riyad Mahrez.

Mwishoni mwa dakika 15 za kwanza, Man-City walikuwa wamewaelekezea wenyeji wao makombora manne na ushindi dhidi ya Arsenal ulikuwa wao wa 18 mfululizo katika mapambano yote kufikia sasa msimu huu.

Matokeo hayo yaliwasaza Arsenal katika nafasi ya 10 kwa alama 34, tisa nyuma ya Chelsea wanaofunga mduara wa tano-bora chini ya kocha wa zamani wa PSG na Borussia Dortmund, Thomas Tuchel.

Wepesi wa mafowadi wa Man-City kucheka na nyavu za wapinzani umeshuhudia mabingwa hao wa zamani wa EPL wakipachika wavuni jumla ya mabao 18 kutokana na mechi sita zilizopita.

Kiu ya kutafuta mabao zaidi dhidi ya Arsenal ilimsukuma Guardiola katika ulazima wa kumwondoa uwanjani kiungo Kevin De Bruyne katika kipindi cha pili na nafasi yake kutwaliwa na Gabriel Jesus aliyeshirikiana vilivyo na Ilkay Gundogan, Sterling, Mahrez na Bernardo Silva katika safu ya mbele.

Mechi hiyo ilimpa kipa Ederson Moraes wa Man-City jukwaa la kuendeleza rekodi ya kutofungwa katika mchuano wa 23 msimu huu.

Man-City ambao kwa sasa wameshinda mechi 11 mfululizo za ugenini kutokana na mashindano yote, hawajawahi kujipata nyuma dhidi ya wapinzani wao katika jumla ya mechi 17 zilizopita za EPL.

Arsenal kwa sasa wamepoteza mechi nane zilizopita dhidi ya Man-City ligini ambapo nne kati ya hizo zimewashuhudia wakishindwa kufunga bao.

Kwa upande wao, Man-City hawajawahi kushindwa katika jumla ya mechi 25 zilizopita katika mashindano yote ambayo yamewashuhudia wakishinda mara 22 na kuambulia sare mara tatu.

Tangu mwanzoni mwa msimu huu, hakuna mchezaji yeyote wa EPL ambaye amefunga idadi kubwa ya mabao ya ugenini kuliko Sterling ambaye kwa sasa amecheka na nyavu za wapinzani mara 20.

Huku Man-City kwa sasa wakijiandaa kuvaana na Borussia Monchengladbach ya Ujerumani kwenye mechi ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) itakayowakutanisha jijini Budapest, Hungary mnamo Februari 24, Arsenal watashuka dimbani kupepetana na Benfica kwenye marudiano ya Europa League mnamo Alhamisi ya Februari 25 jijini Athens, Ugiriki.

Arsenal watajibwaga ugani kucheza na Man-City wakitazamia kuendeleza ubabe uliowavunia ushindi wa 4-2 katika mechi ya awali ya EPL dhidi ya Leeds United ugani Emirates.

Hata hivyo, kubwa zaidi lililofanya Man-City kupigiwa upatu wa kuibuka na ushindi, ni ubora wa rekodi yao dhidi ya Arsenal.

Mbali na kufukuzia ufalme wa EPL, masogora wa Guardiola wanawinda mataji mengine matatu katika kampeni za msimu huu. Mbali na taji la EPL wanaliwania kwa mara ya tatu chini ya kipindi cha misimu minne iliyopita, Man-City pia wanafukuzia ufalme wa UEFA na tayari wamefuzu kwa fainali ya Carabao Cup itakayowakutanisha na Tottenham mnamo Aprili 25 uwanjani Wembley, Uingereza.

Man-City wangali pia katika Kombe la FA na watachuana na Everton kwenye robo-fainali itakayochezewa ugani Goodison Park mnamo Machi 21, 2021.

Mechi kati ya Arsenal na Man-City ilikutanisha Arteta kwa mara nyingine na kikosi kilichowahi kumwajiri kuwa kocha msaidizi kwa kipindi cha miaka mitatu chini ya Guardiola.

Baada ya kuvaana na Monchengladbach, Man-City wameratibiwa kuchuana na West Ham, Wolves na Man-United ligini kwa usanjari huo.

Kwa upande wao, Arsenal watakuwa na kibarua kizito ligini dhidi ya Leicester, Tottenham, West Ham na Liverpool kwa usanjari huo baada ya kurudiana na Benfica kwenye Europa League.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Monaco yaduwaza PSG kwa kuipiga 2-0 kwenye Ligue 1

Jeraha la mguu kumweka nje nahodha wa Aston Villa,...