Messi aweka rekodi katika sare ya 1-1 kati ya Barcelona na Cadiz kwenye La Liga

Na MASHIRIKA

LIONEL Messi aliivunja rekodi ya jagina Xavier Hernandez na kuwa mchezaji ambaye kwa sasa amewajibishwa na Barcelona mara nyingi zaidi katika kampeni za Ligi Kuu ya Uhispania.

Fowadi na nahodha huyo raia wa Argentina alifunga bao akiwasakatia Barcelona mchuano wake wa 506 mnamo Jumapili ila miamba hao wakalazimishiwa na Cadiz sare ya 1-1 uwanjani Camp Nou.

Chini ya kocha Ronald Koeman, Barcelona walikuwa wakilenga kutumia mchuano huo kama jukwaa la kujinyanyua siku nne baada ya Paris Saint-Germain (PSG) kuwapepeta 4-1 kwenye soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) ugani Camp Nou.

Mnamo Februari 21, Messi aliwaweka Barcelona kifua mbele kunako dakika ya 32 kupitia penalti kabla ya Alex Fernandez kusawazisha mambo kupitia penalti ya mwisho wa kipindi cha pili.

Goli hilo la Cadiz lilitamatisha rekodi nzuri ya Barcelona waliokuwa wameshinda jumla ya mechi saba mfululizo kwenye kampeni za La Liga.

Barcelona kwa sasa huenda wakashuka hadi nafasi ya nne jedwalini iwapo Sevilla watawachabanga Osasuna kwenye mchuano wa La Liga utakaowakutanisha leo Jumatatu usiku uwanjani El Sadar.

Ushindi kwa Barcelona dhidi ya Cadiz waliokuwa wamepoteza mechi nne za awali kwa mpigo, ungaliwashuhudia wakipunguza pengo la alama kati yao na viongozi wa jedwali Atletico Madrid hadi pointi sita pekee.

Chini ya kocha Diego Simeone, Atletico walipigwa breki na Levante mnamo Februari 20 kwa kichapo cha 2-0 uwanjani Wanda Metropolitano. Kikosi hicho kwa sasa kinajivunia alama 55, tatu pekee kuliko mabingwa watetezi Real Madrid waliocharaza Real Valladolid 1-0 ugenini.

Real wamepangiwa kuvaana na Atalanta ya Italia kwenye UEFA mnamo Februari 24 na watakosa huduma za wanasoka Karim Benzema, Sergio Ramos, Eden Hazard, Marcelo na Dani Carvajal wanaouguza majeraha.

Ushindi wa Levante ulikuwa wao wa kwanza dhidi ya Atletico ligini na ilikuwa mara ya kwanza tangu Disemba 2019 kwa wanasoka wa kocha Simeone kuzidiwa maarifa katika uwanja wao wa nyumbani.

Kipa Jeremias Ledesma aliyekuwa tegemeo kubwa la Cadiz katika ushindi 2-1 waliousajili dhidi ya Barcelona katika mkondo wa kwanza mnamo Disemba 2020, alisalia imara kwa mara nyingine langoni huku akipangua idadi kubwa ya makombora aliyoelekezewa na Messi, Ousmane Dembele na Antoine Griezmann.

Mabao ya Frenkie de Jong na Pedri Gonzalez wa Barcelona hayakuhesabiwa na refa kwa madai kwamba yalifumwa wavuni wawili hao wakiwa wameotea.

MATOKEO YA LA LIGA (Februari 21):

Barcelona 1-1 Cadiz

Real Sociedad 4-0 Alaves

Huesca 3-2 Granada

Elche 1-0 Eibar

Valencia 2-0 Celta Vigo

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO