Huenda maelfu wakafa njaa Tigray, UN yaonya

Na AFP

TIGRAY, Uhabeshi

RIPOTI mpya ya Umoja wa Mataifa imeonya kuhusu “hali ya kuhofisha mno ya utapiamlo” inayochipuka katika eneo la Tigray linalokumbwa na michafuko nchini Uhabeshi.

Imetaja ukosefu wa usalama unaoendelea, dhuluma za kiusimamizi na kuwepo kwa “makundi mbalimbali yaliyojihami” kama vikwazo vikuu dhidi ya juhudi za kusambaza msaada wa kuokoa maisha katika maeneo ya vijijini.

Maeneo hayo hayajafikiwa na wahudumu wa kutoa msaada wa kibinadamu siku 100 tangu ghasia hizo zilipoanza.

“Licha ya maendeleo machache, msaada wa kibinadamu umeendelea kuwa na upungufu ikilinganishwa na kiwango cha mahitaji kote eneo hili,”

“Msaada huo hasa umeendelea kuwa finyu katika maeneo ya vijijini kutokana na changamoto za kufika sehemu hizo, ukosefu wa usalama na kuna pengo kuu na changamoto katika sekta zote,” ilisema ripoti hiyo kutoka kwa Afisi ya Umoja wa Mataifa kuhusu Uelekezi wa Masuala ya Kibinadamu (OHCA).

Taarifa hiyo ilijiri baada ya Shirika la Msalaba Mwekundu Uhabeshi kuonya mapema Februari kwamba, bila mikakati bora ya kufikisha msaada wa kibinadamu katika eneo hilo ambapo asilimia 80 ya raia milioni sita bado hawawezi kufikiwa, maelfu ya watu huenda wakafariki kutokana na njaa baada ya miezi miwili.

Waziri Mkuu Abiy Ahmed aliamrisha vikosi kuingia eneo la Kaskazini mnamo Novemba 4, akisema oparesheni hiyo ililenga kujibu mashambulizi yaliyodaiwa kutekelezwa katika kambi za serikali na kundi la Tigray People’s Liberation Front (TPLF), chama kinachotawala eneo hilo ambacho wakati mmoja kiliongoza serikali nchini humo.

Abiy alitangaza ushindi mnamo Novemba 28 baada ya TPLF kujiondoa kutoka jiji kuu la Mekelle, na miji mikuu eneo hilo, lakini mapigano machache bado yanaendelea.

Baadhi ya wanachama wakuu wa TPLF wangali hawajulikani walipo, ingawa serikali imewakamata au kuwaua maafisa kadhaa wa zamani.

“Kuna ucheleweshaji wa kiwango kikubwa katika kuwafikia watu wanaohitaji msaada,”

“Mahitaji ni mengi mno lakini hatuwezi kujifanya kwamba hatuoni wala kusikia kinachoendelea,” alisema Rais wa Uhabeshi, Sahle-Work Zewde kupitia taarifa mnamo Ijumaa.

Serikali ilitangaza masharti makali ya kufunga eneo la kaskazini huku hatua ya kuzima mawasiliano ikifanya kuwa vigumu mno kwa mashirika ya kutoa msaada wa kibinadamu kufika na kutathmini hali.

Aidha, imekuwa vigumu kwa vyombo vya habari vinavyotaka kuingia eneo hilo kwa lengo la kuchunguza mashambulizi ya kutumia silaha katika maeneo yenye idadi kubwa ya watu.