• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 10:50 AM
Mwilu alalamikia rundo la kesi kortini

Mwilu alalamikia rundo la kesi kortini

Na RUSHDIE OUDIA

KAIMU Jaji Mkuu, Philomena Mwilu, ameelezea kutamaushwa kwake na kuongezeka kwa kesi ambazo hazijasikizwa mahakamani.

Jaji Mwilu aliwazomea mahakimu wenye utendakazi duni kwa kukosa kutilia maanani kazi yao, hivyo kusababisha kurundikana kwa kesi mahakamani, licha ya juhudi mbalimbali za Idara ya Mahakama kusikiza kesi ambazo zimejikokota kwa zaidi ya miaka mitano.

Alisema atafanya ziara za ghafla hivi karibuni katika baadhi ya korti kote nchini ambapo amepokea malalamishi.

Kufikia Juni 2020, kulikuwa na kesi 483,864 zilizosalia katika Korti za Mahakimu.

Idadi hii iliongezeka hadi kesi 524,664 zilizosalia kufikia Disemba 2020, alieleza Kaimu Jaji Mkuu huyo.

“Huku kasi ya kumalizia kesi ikiwa jumla ya asilimia 72 katika korti zote za Mahakimu, licha ya mahakimu kujitahidi vilivyo, kesi ambazo hazijasikizwa zimeongezeka,” alisema Jaji Mwilu.

Alisema haya katika warsha ya awamu ya nane inayoendelea ya wasimamizi wa korti mbalimbali nchini, mjini Kisumu, Jumanne.

Warsha hiyo pia inahudhuriwa na Msajili Mkuu wa Idara ya Mahakama, Bi Anne Amadi.

Mkutano huo wa wiki moja ambao kauli mbiu yake ni ‘Uboreshaji wa Utendakazi kupitia Uimarishaji wa Maadili na Nidhamu’ umewaleta pamoja karibu mahakimu wasimamizi 157 kutoka kote nchini.

Kulingana na Ripoti ya Nusu Mwaka kuhusu Takwimu za Mrundiko wa Kesi kutoka Idara ya Mipangilio na Utendakazi wa Mashirika (DPOP), katika bajeti ya 2020-21 kuanzia Julai 2020 hadi Disemba 31, inaonyesha kuwa kati ya jumla ya kesi 141,392 zilizowasilishwa, ni kesi 101,605, zilisuluhishwa katika kipindi hicho.

Kufikia Januari 2017, wakati mradi wa Kustawisha Mageuzi ya Idara ya Mahakama (SJT) (Mwongozo wa Mikakati ya Idara ya Mahakama) ulipozinduliwa, kulikuwa na kesi 106,134 zilizodumu kwa zaidi ya miaka mitano katika mahakama za chini.

Kesi 120, 226 zilisuluhishwa kati ya wakati huo na Disemba 2020.

You can share this post!

Wito kwa vinara wa NASA waungane upya

Sekta ya afya pabaya maskini kwa matajiri wakiathirika