BBI: Raila apinga wazo la kura ya maamuzi kuandaliwa pamoja na uchaguzi mkuu

Na CHARLES WASONGA

ALIYEKUWA Waziri Mkuu Raila Odinga amepuuzilia mbali pendekezo kutoka kwa baadhi ya wanasiasa kwamba kura ya maamuzi ifanyike pamoja na uchaguzi mkuu.

Akiongea katika ukumbi wa jumba la Ufangamano alipokutana na ujumbe wa vijana kutoka kaunti za Meru na Tharaka Nithi, Bw Odinga amesema Jumatano hatua hiyo itawakanganya wapigakura wakati wa uchaguzi mkuu.

Aliongeza kuwa pendekezo hilo pia litachelewesha utekelezaji wa baadhi ya mapendekezo mazuri katika Mswada wa BBI , kama vile usawa wa kijinsia.

Bw Odinga alisema wale ambao wanatoa pendekezo hilo ni wale ambao wako mrengo wa “LA” lakini wanaogopa kujitokeza waziwazi kujitambulisha na kundi la wanaopinga Mswada huo wa BBI.

“Tukifanya kura ya maamuzi pamoja na uchaguzi mkuu wa 2022, ni lini tutatekeleza hitaji la Katiba kuhusu usawa wa kijinsia? Hii ina manaa kuwa huenda hitaji hilo la usawa wa kijinsia likatekelezwa mnamo 2027 na wanawake hawako tayari kusubiri hadi wakati huo,” kiongozi huyo wa ODM akaeleza.

Wanasiasa wa mrengo wa ‘Tangatanga’ wamekuwa wakisisitiza kuwa kura ya maamuzi inapaswa kufanyika pamoja na uchaguzi mkuu wa 2022 ili kupunguza gharama.

“IEBC imesema kuwa watahitaji Sh14 bilioni kuandaa kura ya maamuzi. Hizi pesa ni nyingi zaidi na zinatosha kugharimia mahitaji mengine ya dharura kama vile chanjo ya corona. Ikiwa ni lazima kura ya maamuzi ifanyike, basi ifanywe pamoja na uchaguzi mkuu ujao ili kuokoa pesa hizi,” Mbunge wa Soy Caleb Kositany alisema Januari.

Jumatano, Bw Odinga ametoa wito kwa vijana hao kuvumisha Mswada wa BBI katika maeneo yao ili Wakenya waweze kujitokeza kwa wingi kuupitisha katika kura ya maamuzi.

“Ninafahamu kuwa Wakenya wameongea kupitia madiwani katika mabunge 40 ambayo yamepitisha Mswada wa BBI kufikia sasa. Lakini hiyo haitoshi. Sasa ni wajibu wa wapigakura, haswa ninyi vijana kupitisha mswada huo katika kura ya maamuzi kwa kujitokeza kwa wingi na kuupigia kura,” akaeleza.

Habari zinazohusiana na hii

UHURU AMTULIZA RAILA

Wababaisha ‘Baba’

ODM: Raila anachezwa

Kingi amzima Raila

Kichwa kinauma

Raila akausha marafiki