• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
JAMVI: Kushindwa BBI Baringo ishara Gideon hatoshi mboga

JAMVI: Kushindwa BBI Baringo ishara Gideon hatoshi mboga

Na LEONARD ONYANGO

HATUA ya Bunge la Kaunti ya Baringo kutupilia mbali Mswada wa Mpango wa Maridhiano (BBI) imedhihirisha kuwa kiongozi wa Kanu Gideon Moi ana kibarua kigumu kumpokonya Naibu wa Rais William Ruto udhibiti wa siasa za eneo la Bonde la Ufa.

Baada ya kugaragazwa nyumbani, Seneta wa Baringo Moi alijiliwaza na Kaunti za Bomet na Kericho zilizopitisha Mswada wa BBI.

Lakini wandani wa Dkt Ruto wanasema kuwa Bw Moi hakuwa na ushawishi wowote kushinikiza kaunti za Bomet na Kericho, ambazo ni ngome ya Naibu wa Rais, kupitisha BBI.

Bw Moi alikuwa wa kwanza kupongeza mabunge ya Kaunti za Bomet na Kericho baada ya kuidhinisha Mswada wa BBI mnamo Februari 23 na Februari 24, mtawalia.

“Tunajivunia Bunge la Kaunti ya Kericho kwa kuidhinisha Mswada wa BBI; tuna deni lenu,” akasema Bw Moi mara baada ya madiwani wa Kericho kuidhinisha mswada huo ambao tayari umewasilishwa Bungeni.

Mara baada ya Bunge la Kaunti ya Baringo kutupilia mbali Mswada wa BBI, Naibu wa Rais Ruto na Bw Moi walikutana Februari 19 katika mazishi ya mwanasiasa mkongwe Hosea Kiplagat kijijini Cheplambus, Baringo ya Kati, ambapo walionyeshana ubabe wa kisiasa.

Katika hotuba yake, Naibu wa Rais alisema kuwa aliongoza ujenzi wa barabara za Ainomoi-Barwessa, Mochongoi-Karandi na tayari serikali imetangaza kandarasi ya ukarabati wa barabara ya Kamukunji-Kisanana-Mugurin – Mogotio.

Lakini Bw Moi alipuuzilia mbali madai hayo ya Dkt Ruto huku akisema kuwa naibu wa rais hajawahi kutekeleza mradi wowote katika eneo hilo.

Siku moja baadaye, Naibu wa Rais alirejea katika Kaunti ya Baringo na kuhutubia maelfu ya wakazi wa maeneo ya Kabarnet katika kile wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa Dkt Ruto alitaka kumwonyesha Bw Moi kuwa yeye ndiye kiongozi wa eneo la Bonde la Ufa.

“Hatua ya Bunge la Kaunti ya Baringo kukataa Mswada wa BBI ni ushindi kwa Naibu wa Rais. Sasa Wakenya wanajua kuwa Bw Moi hana ushawishi wa kisiasa hata katika Kaunti ya Baringo,” anasema wakili Felix Otieno, mdadisi wa masuala ya kisiasa.

Baada ya kuonekana kulemewa katika eneo la Bonde la Ufa, Bw Moi ambaye ni mwenyekiti wa chama cha Kanu, ameelekeza juhudi zake katika maeneo ya kaskazini Mashariki, Magharibi na kaunti za Maasaini.

Bw Moi, wiki iliyopita, alizuru Kaunti ya Kajiado ambapo alikutana na viongozi mbalimbali wa eneo hilo, akiwemo Gavana Ole Lenku.

Seneta wa Baringo pia alikutana na madiwani wa Kajiado wakiongozwa na Kiongozi wa Wengi James Waichangura.

Alhamisi, viongozi wa vyama mbalimbali waliokutana na Rais Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi waliafikiana kuwa watakuwa katika mstari wa mbele katika kuendesha kampeni ya BBI.

Rais Kenyatta alikutana na kiongozi wa ODM Raila Odinga Kalonzo Musyoka (Wiper), Musalia Mudavadi (Amani), Gideon Moi (Kanu), Moses Wetangula (Ford Kenya) na Gavana wa Kitui Charity Ngilu.

Baada ya mkutano huo, Bw Moi alihutubia taifa kwa niaba ya viongozi hao ambapo walishukuru madiwani kwa kuidhinisha mswada wa BBI.

Katika mkutano huo wa saa nne, vinara hao waliafikiana kuwa wataendesha kampeni ya pamoja kupigia debe BBI; hatua ambayo itamfanya Bw Moi kuzuru maeneo mbalimbali ya nchi na kujizolea umaarufu wa siasa.

Wadadisi wa masuala ya siasa wanasema kuwa huenda muungano wa viongozi hao ukaendelea hata baada ya kura ya maamuzi na kutoa mwaniaji wa urais atakayemenyana na Dkt Ruto 2022.

“Vilevile, kampeni hizo za BBI zitampatia Bw Moi fursa ya kuzunguka katika maeneo yote Kenya na kujipigia debe. Naibu wa Rais Ruto, ambaye amesalia vuguvugu kuhusu BBI, itabidi aje na mbinu tofauti ya kumwezesha kuzunguka nchini wakati wa kampeni za kura ya maamuzi,” anasema Bw Mark Bichachi, mdadisi wa masuala ya kisiasa.

You can share this post!

Raia waumia siasa zikivuma

Messi aongoza Barcelona kupepeta Sevilla ligini na...